Mathayo 17 - New Testament in Swahili (Zanzibar) Revised Edition 19211 NA baada ya siku sita Yesu akawachukua Petro, na Yakobo, na Yohana ndugu yake, akawaleta juu ya mlima mrefu peke yao; 2 akageuka sura yake mbele yao: uso wake ukangʼaa kama jua, mavazi yake yakawa meupe kama nuru. 3 Wakawatokea Musa na Eliya, wakizumgumza nae. 4 Petro akajibu akamwambia Yesu, Bwana, ni vizuri sisi kuwapo hapa; ukitaka tutafanya hapa vibanda vitatu, kimoja chako wewe, na kimoja cha Musa, na kimoja cha Eliya. 5 Alipokuwa akisema, wingu jeupe likawatia uvuli; sauti ikatoka katika lile wingu, ikinena, Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, niliyependezwa nae; msikieni yeye. 6 Na wale wanafunzi waliposikia, wakaanguka kifudifudi, wakaogopa sana. 7 Yesu akaja, akawagusa, akasema, Ondokeni, msiogope. 8 Wakainua macho yao, wasione mtu illa Yesu peke yake. 9 Na walipokuwa wakishuka mlimani, Yesu akawaagiza, akinena, Msimwambie mtu khabari ya mambo hayo, hatta Mwana wa Adamu atakapofufuka katika wafu. 10 Wanafunzi wake wakamwuliza, wakinena, Mbona bassi waandishi hunena ya kwamba imempasa Eliya kuja kwanza? 11 Yesu akajibu, akawaambia, Kweli Eliya yuaja kwanza, nae atatengeneza yote; 12 lakini nawaambieni, ya kwamba Eliya amekwisha kuja, wasimtambue, wakamtenda yote waliyotaka. Vivyo hivyo Mwana wa Adamu nae atateswa nao. 13 Ndipo wakafahamu wale wanafunzi ya kuwa amesema nao khabari za Yohana Mbatizaji. 14 Nao walipoufikia mkutano, mtu akamjia, akampigia magoti, akinena, 15 Bwana, mrehemu mwana wangu, kwa kuwa hushikwa na kifafa, na kuteswa vibaya: maana marra nyingi huanguka motoni, na marra nyingi majini. 16 Nikamleta kwa wanafunzi wako, nao hawakuweza kumponya. 17 Yesu akajibu, akasema, Enyi kizazi kisichoamini na kipotofu, nitakuwa pamoja nanyi hatta lini? Nitachukuliana nanyi hatta lini? Mleteni huku kwangu. 18 Yesu akamkaripia pepo, akamtoka; yule kijana akapona tangu saa ile. 19 Kiisha wale wanafunzi wakaniwendea Yesu kwa feragha, wakasema, Mbona sisi hatukuweza kumfukuza? 20 Yesu akawaambia, Kwa sababu ya kutokuamini kwenu. Kwa maana, amin, nawaambieni, Mkiwa na imani kama punje ya kharadali mtauambia mlima huu, Ondoka hapa hatta kule; nao utaondoka; wala halitakuwako neno lisilowezekana kwenu. 21 Lakini namna hii haitoki illa kwa kusali na kufunga. 22 Walipokuwa wakikaa Galilaya, Yesu akawaambia, Mwana wa Adamu karibu atatiwa mikononi mwa watu, 23 nao watamwua, na siku ya tatu atafufuka. Wakasikitika sana. 24 Hatta walipofika Kapernaum, wale watozao nussu shekeli wakamwendea Petro, wakasema, Je! Mwalimu wenu hatoi nussu shekeli? 25 Akanena, Hutoa. Nae alipoingia nyumbani, Yesu akatangulia kumwuliza, akinena, Waonaje, Simon? Wafalme wa dunia hutwaa kodi ama ushuru kwa watu gani? kwa wana wao au kwa wageni? 26 Petro akamwambia, Kwa wageni. Yesu akamwambia, Bassi, kama ni hivyo, wana ni huru. 27 Lakini tusije tukawachukiza, enenda baharini ukatumbukize ndoana, ukatwae samaki yule azukae kwanza; na ukifunua mdomo wake utaona shekeli; ichukue hiyo ukawape kwa ajili yangu na kwa ajili yako. |
Swahili New Testament © Bible Society of Tanzania, 1921.
Bible Society of Tanzania