Mathayo 14 - New Testament in Swahili (Zanzibar) Revised Edition 19211 WAKATI ule Herode tetrarka alisikia khabari za Yesu, 2 akawaambia watumishi wake, Huyu ndiye Yohana Mbatizaji; amefufuka katika wafu; na kwa sababu hii nguvu hizo zinatenda kazi ndani yake. 3 Maana Herode alikuwa amemkamata Yohana, akamfunga, akamtia gerezani, kwa ajili ya Herodias, mke wa Filipo ndugu yake. 4 Kwa sababu Yohana alimwambia, Ni haramu kwako kukaa uae. 5 Na alipotaka kumwua, aliwaogopa watu, maana walimwona kuwa nabii. 6 Hatta panapo siku kuu ya kuzaliwa kwake Herode, binti Herodias alicheza kati ya watu, akampendeza Herode. 7 Hatta akakiri kwa kiapo atampa lo lote atakaloliomba. 8 Nae, akishawishwa na mama yake, akasema, Nipe hapa katika kombe kichwa cha Yohana Mbatizaji. 9 Mfalme akasikitika; lakini kwa ajili ya nyapo zake, na kwa ajili ya wale walioketi chakulani pamoja nae, akaamuru apewe; 10 akatuma mtu, akamkata kichwa Yohana mle gerezani. 11 Kichwa chake kikaletwa katika kombe, akapewa yule kijana: akakichukua kwa mama yake. 12 Wanafunzi wake wakaenda, wakauchukua mwili wake, wakauzika; wakaenda wakampasha Yesu khabari. 13 Yesu aliposikia, akatoka huku katika chombo, akaenda mahali pasipo watu, kwa faragha. Na makutano waliposikia, wakamfuata kwa miguu toka miji yao. 14 Yesu akatoka, akaona makutano mengi, akawahurumia, akawaponya wagonjwa wao. 15 Hatta ilipokuwa jioni, wanafunzi wake wakamwendea, wakanena, Mahali hapa nyika tupu, na saa imekwisha pita; waage makutano, waende zao vijijini, wakajinunulie vyakula. 16 Yesu akawaambia, Hawana haja kwenda zao, wapeni ninyi kula. 17 Wakamwambia, Hatuna kitu hapa illa mikate mitano na samaki mbili. 18 Akasema, Nileteeni vitu vile hapa. 19 Akawaagiza makutano waketi katika majani; akaitwaa ile mikate mitano na zile samaki mbili, akatazama juu mbinguni, akabariki, akamega, akawapa wanafunzi ile mikate, wanafunzi wakawapa makutano. 20 Wakala wote wakashiba: wakayaokota masazo ya vipande vya mikate, vikapu thenashara, vimejaa. 21 Nao waliokula walikuwa wanaume wapata elfu tano, bila wanawake na watoto. 22 Marra Yesu akawalazimisha wamifunzi wake wapande chomboni na kutangulia mbele yake kwenda ngʼambu, wakati yeye alipokuwa akiwaaga makutano. 23 Alipokwisha kuwaaga makutano, akapanda mlimani kwa faragha, kwenda kusali. Na ilipokuwa jioni, alikuwako huko peke yake. 24 Na kile chombo kimekwisha kufika katikati ya bahari, kinataabika sana na mawimbi; maana upepo ulikuwa wa mbisho. 25 Hatta zamu ya nne ya usiku Yesu akawaendea, akitembea juu ya bahari. 26 Wanafunzi walipomwona akitembea juu ya bahari, wakafadhaika, wakinena. Ni kivuli; wakapiga yowe kwa khofu. 27 Marra Yesu akasema nao, akinena, Jipeni moyo; ni mimi; msiogope. 28 Petro akamjibu, akasema, Bwana, ikiwa ni wewe, niamuru nije kwako juu ya maji. 29 Akasema, Njoo. Petro akashuka chomboni, akatembea juu ya maji, illi kumwendea Yesu. 30 Lakini alipoona upepo wa nguvu, akaogopa: akaanza kuzama, akapiga yowe, akinena, Bwana, niokoe. 31 Marra Yesu akanyosha mkono wake, akamshika, akamwambia, Ewe mwenye imani haba, mbona uliona shaka? 32 Walipopanda chomboni, upepo ukakoma. 33 Nao waliokuwa ndani ya chombo wakamwendea, wakamsujudia, wakinena, Hakika wewe u Mwana wa Mungu. 34 Na walipokwisha kuvuka, wakafika inchi ya Genesareti. 35 Na watu wa mahali pale walipomtambua, wakatuma watu kwenda inchi zile zote zilizo kandokando, wakamletea wote waliokuwa hawawezi; 36 wakamsihi waguse hatta pindo la vazi lake; na wote waliogusa wakaponywa kabisa. |
Swahili New Testament © Bible Society of Tanzania, 1921.
Bible Society of Tanzania