Matendo 9 - New Testament in Swahili (Zanzibar) Revised Edition 19211 LAKINI Saul, akizidi kutisha na kuwaza kuwaua wanafunzi wa Bwana, akamwendea kuhani mkuu, 2 akataka ampe khati za kwenda Dameski zilizoandikwa kwa masunagogi, illi akiona watu wa Njia hii, waume kwa wake, awafunge na kuwaleta Yerusalemi. 3 Hatta alipokuwa akisafiri akawa anakaribia Dameski; ghafula ikamwangaza nuru kutoka mbinguni. 4 Akaanguka chini, akasikia sauti ikimwambia, Saul, Saul, mbona wanifukuza? 5 Akasema, U nani Bwana? Akasema, Mimi ndimi Yesu unaeniudhi wewe. 6 Lakini simama, uingie mjini, utaambiwa yatakayokupasa kutenda. 7 Na watu waliosafiri pamoja nae wakasimama kimya, wakiisikia sauti, wasione mtu. 8 Saul akaondoka katika inchi, na macho yake yalipofumbuka, hakuona kitu: wakamshika mkono wakamleta hatta Dameski. 9 Akawa siku tatu haoni, wala hali, wala hanywi. 10 Bassi palikuwapo mwanafunzi Dameski, jina lake Anania. Bwana akamwambia katika njozi, Anania. Akasema, Mimi hapa, Bwana. 11 Bwana akamwambia, Simama, enenda zako katika njia iitwayo Sawa, ukatafute ndani ya nyumba ya Yuda mtu jina lake Saul, wa Tarso: maana yuko anasali: 12 nae amemwona mtu, jina lake Anania, akiingia, akiweka mikono juu yake, apate kuona tena. 13 Lakini Anania akajibu, Bwana, nimesikia khabari za mtu huyu kwa watu wengi, mabaya mengi aliyowatenda watakatifu wako Yerusalemi: 14 hatta hapa ana mamlaka kwa makuhani wakuu awafunge wote wakuitiao Jina lako. 15 Lakini Bwana akamwambia, Shika njia; kwa maana huyu ni chombo kiteule kwangu, alichukue Jina langu mbele ya mataifa, na wafalme, na wana wa Israeli. 16 Maana nitamwonyesba mambo mengi makuu yatakayompasa kuteswa kwa ajili ya Jina langu. 17 Anania akaenda zake, akaingia mle nyumbani; akamwekea mikono akisema, Ndugu Saul, Bwana amenipeleka, Yesu, yeye aliyekutokea katika njia uliyoijia, upate kuona tena, ukajazwe Roho Mtakatifu. 18 Marra yakaanguka machoni pake kama magamba, akapata kuona akasimama, akabatizwa; 19 akala chakula, akapata nguvu. Akawa huko siku kadhawakadha pamoja na wanafunzi walioko Dameski. 20 Marra akamkhubiri Yesu katika masunagogi, kwamba yeye ni Mwana wa Mungu. 21 Na wote waliosikia wakashangaa, wakasema, Siye huyu aliyewateka walioliita Jina hili Yerusalemi? Na hapa amekuja kusudi hili, awafunge na kuwapeleka kwa makuhani wakuu? 22 Saul akazidi kuwa hodari, akawatia fadhaa Wayahudi waliokaa Dameski, akithubutisha ya kuwa huyu udiye Kristo. 23 Hatta siku nyingi zilipopita, Wayahudi wakafanya shauri illi wamwue: 24 lakini hila yao ikajulikana na Saul. Wakamvizia malangoni mchana na usiku wapate kumwua. 25 Wanafunzi wakamtwaa usiku wakamshusha ukutani, wakimtelemsha katika kapu. 26 Na Saul alipofika Yerusalemi, alijaribu kujiunga na wanafunzi, nao walikuwa wakimwogopa wote, wasisadiki ya kuwa yeye ni mwanafunzi. 27 Barnaba akamtwaa, akampeleka kwa mitume, akawaeleza jinsi alivyomwona Bwana njiani, na ya kwamba alisema nae, na jinsi alivyokhubiri pasipo khofu katika Dameski kwa jina lake Yesu. 28 Nae akawa pamoja nao katika Yerusalemi akiingia na kutoka. 29 Akaneua kwa jina lake Yesu pasipo khofu, akinena na kushindana na Wahelenisti. Nao wakajaribu kumwua. 30 Lakini ndugu walipopata khabari wakamchukua hatta Kaisaria wakampeleka Tarso. 31 Bassi makanisa wakapata raha katika Yahudi yote na Galilaya na Samaria, wakajengewa, wakiendelea katika kicho cha Bwana, na faraja ya Roho Mtakatifu. 32 Hatta Petro alipokuwa akizungukazunguka pande zote akawatelemkia watakatifu waliokaa Ludda. 33 Akamwona mtu mmoja huko, jina lake Ainea mtu huyo amelala kitandani miaka minane; maana alikuwa amepooza. 34 Petro akamwambia, Ainea, Yesu Kristo akuponya: ondoka, ukatandike kitanda chako. 35 Marra akaondoka. Na watu wote waliokaa Ludda na Saron wakamwona, wakamgeukia Bwana. 36 Na mwanafunzi mmoja alikuwako Yoppa, jina lake Tabitha, (tafsiri yake ni paa:) mwanamke huyu alikuwa amejaa matendo mema na sadaka alizozitoa. 37 Ikawa siku zile akaugua, akafa: hatta walipokwisha kumwosha, wakamweka orofani. 38 Na kwa kuwa Ludda ulikuwa karibu na Yoppa, nao wamesikia ya kwamha Petro yuko huko, wakatuma watu wawili kwake, kumsihi asikawie kuja kwao. 39 Petro akaondoka akafuatana nao. Alipofika wakampeleka juu orofani: wajane wote wakasimama karibu nae, wakilia na kuniwonyesha zile kanzu na nguo alizozifanya Paa wakati ule alipokuwa pamoja nao. 40 Petro akawatoa wote, akapiga magoti, akaomba, akaielekea mayiti, akanena, Tabitha, ondoka. Nae akafumbua macho yake, na alipomwona Petro akajiinua, akaketi. 41 Akampa mkono, akamwinua; hatta akiisha kuwaita wale watakatifu na wajane akamweka mbele yao, yu hayi. 42 Ikajulikana katika Yoppa, katika mji mzima, watu wengi wakamwamini Bwana. 43 Hatta Petro akakaa siku kadha wa kadha huko Yoppa, nyumbani mwa mtu mmoja, jina lake Simon, mtengenezaji wa ngozi. |
Swahili New Testament © Bible Society of Tanzania, 1921.
Bible Society of Tanzania