Matendo 7 - New Testament in Swahili (Zanzibar) Revised Edition 19211 KUHANI mkuu akasema, Je! Mambo hayo ndivyo yalivyo? 2 Nae akasema, Ndugu zangu na baba zangu, sikilizeni: Mungu wa utukufu alimtokea baba yetu Ibrahimu, alipokuwa katika Mesopotamia, kabla hajakaa Kharran, akamwambia, 3 Toka katika inchi yako na katika jamaa zako, ukaende hatta inchi nitakayokuonyesha. 4 Ndipo alitoka katika inchi ya Wakaldayo, akakaa Kharran, akatoka huko baada ya kufa baba yake, Mungu akamhamisha hatta inchi hii mnayokaa ninyi sasa. 5 Wala hakumpa urithi humu hatta kiasi cha kuweka mguu: akaahidi kwamba atampa, iwe milki yake, na ya, uzao wake baadae, alipokuwa hana mtoto. 6 Mungu akanena hivi, ya kama wazao wake watakuwa wageni katika inchi ya watu wengine, nao watawafanya kuwa watumwa wao, na kuwatenda mabaya kwa muda wa miaka aroba mia. 7 Na lile taifa watakaowafanya watumwa nitawahukumu mimi, alisema Mungu; na baada ya hayo watatoka, nao wataniabudu mahali hapa. 8 Akampa agano la Tohara; bassi Ibrahimu akazaa Isaak, akamtahiri siku ya nane. Isaak akamzaa Yakobo, Yakobo akawazaa wale thenashara, wazee wetu. 9 Wale wazee wetu wakamwonea wivu Yusuf, wakamwuza aende Misri. Mungu akawa pamoja nae, 10 akamtoa katika misiba yake yote, akampa kibali na hekima mbele ya Farao, mfalme wa Misri: nae akamfanya msimamizi wa Misri na nyumba yake yote. 11 Bassi kukawa njaa juu ya inchi yote ya Misri na Kanaan, na dhiki nyingi, wala baba zetu hawakupata chakula cha kuwatosha. 12 Hatta Yakobo aliposikla ya kwamba huko Misri kuna nafaka, akawatuma baba zetu marra ya kwanza. 13 Hatta safari ya pili Yusuf akajitambulisha kwa ndugu zake, jamaa ya Yusuf ikawa dhahiri kwa Farao. 14 Yusuf akatuma watu akamwita Yakobo baba yake na jamaa zake wote pia, watu sabaini na watano. 15 Yakobo akashuka hatta Misri, akafariki yeye na baba zetu; 16 wakachukuliwa hatta Sukem wakazikwa katika kaburi lile, ambalo Ibrahimu alilinunua kwa kimo cha fedha kwa wana wa Emmor, huko Sukem. 17 Bassi wakati wa ile ahadi ambayo Mungu alimpa Ibrahimu ulipokuwa unakaribia, wale watu wakazidi na kuongezeka sana huko Misri, 18 mpaka mfalme mwingine akaondoka, asiyemfahamu Yusuf. 19 Huyo akawafanyia hila baba zetu, na kuwatenda mabaya baba zetu, akiwaamuru watupe watoto wao wachanga, illi wasiishi. 20 Wakati huo akazaliwa Musa, nae alikuwa mzuri sana, akalelewa muda wa miezi mitatu katika nyumba ya baba yake. 21 Hatta alipotupwa, binti Farao akamtwaa, akamlea awe kama mwana wake. 22 Musa akafundishwa hekima yote ya Misri, akawa hodari wa maneno na matendo. 23 Umri wake ulipopata kama miaka arubaini akaazimu moyoni kwenda kuwatazama ndugu zake wana wa Israeli. 24 Akamwona mmoja akidhulumiwa, akamhami, akamlipia kisasi yule aliyekuwa akionewa, akampiga Mmisri. 25 Alidhani kwamba ndugu zake watafahamu ya kuwa Mungu anawapa wokofu kwa mkono wake, lakini hawakufahamu. 26 Siku ya pili yake akawatokea walipokuwa wakishindana, akataka kuwapatanisha, akisema, Enyi bwana zangu, ninyi m ndugu: Mbona mnadhulumiana? 27 Lakini yeye aliyemdhulumu mwenziwe akamsukumia mbali, akisema, Ni nani aliyekuweka kuwa mkuu wetu, na mwamuzi wetu? 28 Je! wataka kuniua mimi kama ulivyomwua yule Mmisri jana? 29 Musa akakimbia kwa neno hilo, akakaa hali ya mgeni katika inchi ya Madiani, akazaa wana wawili huko. 30 Hatta miaka arubaini ilipotimia, malaika wa Bwana akamtokea katika jangwa la mlima Sinai katika mwali wa moto, kijitini. 31 Musa alipouona, akastaajabia maono yale, na alipokaribia illi atazame, sauti ya Bwana ikamjia, 32 Mimi ni Mungu wa baba zako, Mungu wa Ibrahimu, na Mungu wa Isaak, na Mungu wa Yakobo. 33 Musa akatetemeka, asithubutu kutazama. Bwana akamwambia, Vua viatu vyako, kwa maana mahali hapa unaposimama ni inchi takatifu. 34 Yakini nimeona mateso ya watu wangu waliomo Misri, nimesikia kuugua kwao, nimeshuka niwatoe. Bassi sasa, nitakutuma hatta Misri. 35 Musa huyo waliyemkataa, wakisema, Ni nani aliyekuweka kuwa mkuu na mwamuzi? ndiye aliyetumwa na Mungu kuwa mkuu na mkombozi, kwa mkono wa yule malaika aliyemtokea katika kile kijiti. 36 Huyo ndiye aliyewatoa, akifanya ajabu na ishara katika inchi ya Misri, na katika bahari ya Sham, na katika jangwa muda wa miaka arubaini. 37 Musa huyo ndiye aliyewaambia wana wa Israeli, Bwana Mungu wenu atawainulieni nabii katika ndugu zenu, kama mimi: mtamsikia huyo. 38 Yeye ndiye aliyekuwa katika kanisa jangwani pamoja na yule malaika aliyesema nae katika mlima Sinai, tena pamoja na baba zetu: ndiye aliyepokea maneno ya uzima atupe sisi. 39 Mtu huyo baba zetu hawakutaka kumtii, bali wakamsukumia mbali, na kwa mioyo yao wakarudi Misri, 40 wakamwambia Haruni, Tufanyie miungu, watakaotutangulia: maana huyo Musa, aliyetutoa katika inchi ya Misri, hatujui lililompata. 41 Wakafanya ndama siku zile, wakaleta dhabihu kwa sanamu ile, wakafurahia kazi ya mikono yao. 42 Bassi Mungu akaghairi, akawaacha, wakaliabudu jeshi la mbinguni, kama ilivyoandikwa katika kitabu cha manabii, Je! mlinitolea dhabihu na sadaka Miaka arubaini katika jangwa, enyi nyumba ya Israeli? 43 Nanyi mlichukua khema ya Molok, Na nyota za mungu wenu Refan, Sanamu mlizozifanya illi kuziabudu: Nami nitawabamisha mwende mbali hatta Babel. 44 Ile khema ya shahada ilikuwa pamoja na baba zetu jangwani, kama alivyoagiza yeye aliyesema na Musa, ya kwamba aifanye sawa sawa na mfano ule aliouona; 45 ambayo baba zetu waliipokea; wakaiingiza pamoja na Yoshua katika milki ya mataifa wale, ambao Mungu aliwafukuza mbele ya baba zetu, mpaka siku za Daud: 46 aliyepata kibali mbele ya Mungu, nae aliomba ampatie Mungu wa Yakobo maskani. 47 Lakini Sulemani alimjengea nyumba. 48 Illakini yeye aliye juu hakai katika nyumba zilizofanyika kwa mikono, kama vile asemavyo nabii: 49 Mbingu ni kiti changu cha enzi, Na inchi ni mahali pa kutia miguu yangu: Ni nyumba gani mtakayonijengea? asema Bwana: Au ni mahali gani nitakapostarebe? 50 Sio mkono wangu uliofanya haya yote? 51 Enyi wenye shingo gumu, msiotahiriwa mioyo wala masikio, siku zote mnampinga Roho Mtakatifu; kama baba zenu walivyofanya na ninyi vivyo hivyo. 52 Ni yupi katika manabii ambae baba zenu hawakumwudhi? nao waliwaua wale waliotabiri khabari za kuja kwake yule mwenye haki; ambae ninyi sasa mmemsaliti mkamwua; 53 ninyi mlioipokea torati kwa khuduma ya malaika wala hamkuishika. 54 Bassi waliposikia maneno haya, wakachomwa mioyo, wakamsagia meno. 55 Nae akijaa Roho Mtakatifu, akakaza macho yake, akitazama mbinguni, akauona utukufu wa Mungu, na Yesu akisimama mkono wa kuume wa Mungu. 56 Akasema, Tazama! naona mbingu zimefunuliwa, na Mwana wa Adamu amesimama mkono wa Mungu. 57 Wakapiga kelele kwa sauti kuu, wakaziba masikio yao, wakamrukia kwa nia moja, 58 wakamtoa nje ya mji, wakampiga mawe. Nao mashahidi wakaweka nguo zao miguuni pa kijana mmoja aliyekwitwa Saul. 59 Wakampiga mawe Stefano, nae akiomba, akisema, Bwana Yesu, pokea roho yangu. 60 Akapiga magoti, akalia kwa sauti kuu, Bwana, usiwahesabie dhambi hii. Akiisha kusema haya akalala. |
Swahili New Testament © Bible Society of Tanzania, 1921.
Bible Society of Tanzania