Matendo 18 - New Testament in Swahili (Zanzibar) Revised Edition 19211 BAADA ya mambo haya Paolo akatoka Athene akalika Korintho. 2 Akamwona Myahudi mmoja, jina lake Akula, mzalia wa Ponto; nae amekuja kutoka inchi ya italia siku za karibu, pamoja na Priskilla mkewe, kwa sababu Klaudio amewaamuru Wayahudi wote watoke Rumi. 3 Akafika kwao; na kwa kuwa kazi yake na kazi yao ni moja, akakaa kwao, akafanya kazi yake, kwa maana walikuwa mafundi wa kufanyiza khema. 4 Akatoa hoja zake katika sunagogi killa sabato akawavuta Wayahudi na Wayunani waamini. 5 Hatta Sila na Timotheo walipotelemka kutoka Makedonia, Paolo akashurutishwa rohoni mwake, akiwashuhudia Wayahudi ya kwamba Yesu ni Kristo. 6 Walipopingamana nae na kutukana, akakungʼuta mavazi yake, akawaambia, Damu yenu na iwe juu ya vichwa vyenu: mimi ni safi: langu sasa nitakwenda kwa watu wa mataifa. 7 Akaondoka huko akaingia katika nyumba ya mtu mmoja jina lake Yusto, mcha Mungu, ambae nyumba yake ilikuwa mpaka mmoja na sunagogi. 8 Na Krispo, mkuu wa sunagogi, akamwamini Bwana pamoja na nyumba yake yote. Wakorintho wengi wakasikia, wakaamini, wakabatizwa. 9 Bwana akamwambia Paolo kwa njozi nsiku, Usiogope, bali nena, wala usinyamaze, 10 kwa kuwa mimi ni pamoja nawe, wala hapana mtu atakaekushambulia illi kukudhuru; kwa matina mimi nina watu wengi katika mji huu. 11 Akakaa huko muda wa mwaka mmoja na miezi sita akawafundisha neno la Mungu. 12 Hatta Gallio alipokuwa Prokonsuli wa Akaya, Wayahudi wakamwendea Paolo kwa nia moja, wakamleta mbele ya kiti cha hukumu, 13 wakisema, Mtu huyu huwavuta watu illi wamwabudu Mungu kinyume cha sharia yetu. 14 Na Paolo alipotaka kufunua kinywa chake, Gallio akawaambia Wayahudi, Kama lingetendeka tendo la dhuluma au la hila mbaya, enyi Wayahudi, ingekuwa haki kuchukuliana nanyi; 15 bali ikiwa ni hoja juu ya maneno na majina na sharia yenu, liangalieni ninyi wenyewe, maana mimi sitaki kuwa mwamuzi wa mambo hayo. 16 Akawafukuza mbele ya kiti cha hukumu. 17 Na Wayunani wote wakamshika Sosthene, mkuu wa sunagogi, wakampiga mbele ya kiti cha hukumu. Na Gallio hakuyaona mambo hayo kuwa kitu. 18 Paolo akazidi kukaa huko siku nyingi, kiisha akaagana na ndugu akatweka kwenda Shami; na Priskilla na Akula wakaenda pamoja nae, alipokwisha kunyoa kichwa chake katika Kenkrea; maana alikuwa ana nadhiri. 19 Wakalika Efeso, akawaacha huko. Yeye mwenyewe akaingia katika sunagogi, akahujiana na Wayahudi. 20 Walipotaka akae wakati mwingi zaidi, hakukubali: 21 bali aliagana nao, akisema. Sina buddi kufanya siku kuu hii inayokuja Yerusalemi: lakini nitarejea kwenu, Mungu akinijalia. 22 Akatweka, akatoka Efeso, na alipokwisha kushuka Kaisaria, akapanda juu, akawasalimu Kanisa, akatelemkia Antiokia. 23 Hatta akiisha kukaa huko siku kadha wa kadha akaondoka, akapita kati ya inchi ya Galatia na Frugia, mji kwa mji, akiwatia moyo wanafunzi. 24 Bassi Myahudi mmoja, jina lake Apollo, mzalia wa Iskanderia, mtu wa elimu, akalika Efeso; nae alikuwa hodari wa maandiko. 25 Mtu huyu alikuwa amefundishwa njia ya Bwana; na kwa kuwa roho yake ilikuwa ikiwaka, alianza kunena na kufundisha kwa usahihi khabari za Bwana; nae alijua ubatizo wa Yohana tu. 26 Akaanza kunena bila khofu katika sunagogi: hatta Akula na Priskilla walipomsikia wakamchukua kwao, wakamweleza njia ya Bwana kwa usahihi zaidi. 27 Na alipotaka kuvuka bahari aende hatta Akaya, ndugu wakamhimiza, wakamwandikia barua kwa wanafunzi wale wamkaribishe; nae alipofika akawasaidia sana wale waliokwisha kuamini kwa neema ya Mungu. 28 Kwa maana aliwashinda Wayahudi kabisa kabisa mbele ya watu wote, akiwaonyesha kwa maneno ya maandiko ya kuwa Yesu ni Kristo. |
Swahili New Testament © Bible Society of Tanzania, 1921.
Bible Society of Tanzania