Matendo 1 - New Testament in Swahili (Zanzibar) Revised Edition 19211 KITABU kile cha kwanza nalikifanya, Theofilo, katika khabari ya mambo yote aliyoanza kufanya Yesu na kufundisha, 2 hatta siku ile alipowaagiza kwa Roho Mtakatifu mitume aliowachagua, akachukuliwa juu: 3 na baada ya kuteswa kwake, akawadhihirisbia ya kwamba yu hayi, kwa dalili nyingi, akiwatokea muda wa siku arubaini, na kuyanena mambo yaliyonkhusu ufalme wa Mungu. 4 Hatta, akikutana nao, akawaagiza wasitoke katika Yerusalemi, bali waingoje ahadi ya Baba, ambayo mlisikia khabari zake kwangu; 5 ya kwamba Yohana alibatiza kwa maji, bali ninyi mtabatizwa katika Roho Mtakatifu baada ya siku hizi si nyingi. 6 Bassi walipokutanika, wakamwuliza, wakisema, Bwana, wakati huu ndipo unapomrudishia Israeli ufalme wake? 7 Akawaambia, Si kazi yenu kujua nyakati wala majira, Baba aliyoyaweka katika mamlaka yake mwenyewe. 8 Lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemi, na katika Yahudi yote, na Samaria, na hatta mwisho wa inchi. 9 Akiisha kusema haya, walipokuwa wakitazama, akainuliwa, wingu likampokea kutoka machoni pao. 10 Walipokuwa wakikaza macho mbinguni, yeye alipokuwa akienda zake, watu wawili wakasimama karibu nao, wenye nguo nyeupe, 11 wakasema, Watu wa Galilaya, mbona mmesimama mkitazama mbinguni? Huyu Yesu aliyechukuliwa kutoka kwenu kwenda juu mbinguni, atakuja jinsi hiyo hiyo mlivyomwona akienda zake mbinguni. 12 Kiisha wakarudi kwenda Yerusalemi kutoka mlima ulioitwa wa mizeituni, ulio karibu na Yerusalemi, wapata mwendo wa sabato. 13 Hatta walipoingia, wakapanda orofani, walipokuwa wakikaa; Petro, na Yakobo, na Yohana, na Andrea, Filipo na Tomaso, Bartolomayo na Mattayo, Yakobo wa Alfayo, na Simon Zelote, na Yuda wa Yakobo. 14 Hawa wote walikuwa wakidumu kwa moyo mmoja katika kuomba, pamoja nao wanawake, na Mariamu mama wake Yesu, na ndugu zake. 15 Siku zile akasimama Petro kati ya wanafunzi, akasema (jumla ya majina ilipata mia na ishirini), 16 Ndugu imepasa andiko litimizwe, alilolinena Roho Mtakatifu zamani kwa kinywa cha Daud, katika khabari za Yuda, aliyekuwa kiongozi wao waliomkamata Yesu: kwa sababu alikuwa amehesabiwa pamoja na sisi, 17 akapata sehemu ya khuduma hii. 18 (Bassi huyu alinunua konde kwa ijara ya ndhalimu; akaanguka kifudifudi akapasuka, matumbo yake yote yakatoka. 19 Ikajulikana na watu wote wakaao Yerusalemi; hatta konde lile likaitwa kwa lugha yao Akeldama, maana yake, konde la damu.) 20 Kwa maana imeandikwa katika kitabu cha Zaburi, Kikao chake kiwe ukiwa, wala asiwepo mtu mwenye kukaa humo; tena, Usimamizi wake autwae mwingine. 21 Bassi katika watu waliofuatana nasi wakati wote ambapo Bwana Yesu alikuwa akiingia kwetu na kutoka kwetu, 22 akianza tangu ubatizo wa Yohana, hatta siku ile alipochukuliwa kwetu kwenda juu, lazima mmoja wao afanywe shahidi wa kufufuka kwake pamoja nasi. 23 Wakaweka wawili, Yusuf, aitwae Barsaba, aliyepewa jina la pili Yusto, na Mattiya. 24 Wakasali, wakasema, Wewe, Bwana, ujuae mioyo ya watu wote, tuonyeshe ni nani uliyemchagua katika hawa wawili, 25 atwae sehemu yake ya khuduma hii na utume huu, alioukosa Yuda aende zake mahali pake. 26 Wakawapigia kura: kura ikamtoa Mattiya; akachaguliwa kuwa pamoja na mitume edashara. |
Swahili New Testament © Bible Society of Tanzania, 1921.
Bible Society of Tanzania