Biblia Todo Logo
Biblia ya mtandaoni

- Matangazo -

Luka 22 - New Testament in Swahili (Zanzibar) Revised Edition 1921

1 IKAKARIBIA siku kuu ya mikate isiyochachwa, iitwayo Pasaka.

2 Makuhani wakuu na waandishi wakatafuta njia ya kumwua, kwa maana walikuwa wakiwaogopa watu.

3 Shetani akamwingia Yuda, aitwae Iskariote, nae alikuwa katika hesabu ya wale thenashara.

4 Akaenda zake akasema na makuhani wakuu na majemadari jinsi ya kumtia katika mikono yao.

5 Wakafurahi, wakapatana kumpa fedha.

6 Akaahidi, akatafuta nafasi kumsaliti kwao pasipo kuwapo makutano.

7 Ikawadia siku ya mikate isiyochachwa, ilipopasa kuchinja pasaka.

8 Akapeleka Petro na Yohana, akisema, Enendeni, mkatuandikie pasaka, illi tuile.

9 Wakamwambia, Wapi utakapo tuiandalie?

10 Akawaambia, Tazama, mtakapoingia mjini, atakutana nanyi mtu mume achukuae mtungi wa maji: mfuateni mpaka nyumba atakayoingia.

11 Na mtamwambia mwenye nyumba, Mwalimu akuambia, Ki wapi chumba cha wageni, nipate kula Pasaka humo pamoja na wanafunzi wangu?

12 Na mtu yule atawaonyesha orofa kubwa iliyopambwa; huko andalieni.

13 Wakaenda wakaona kama alivyowaambia, wakaiandalia Pasaka.

14 Bassi saa ilipowadia, akaketi, na mitume pamoja nae.

15 Akawaambia, Nimetamani sana kula pasaka hii pamoja nanyi, kabla va kuteswa:

16 kwa maana nawaambieni, Sitaila kabisa hatta itakapotimizwa katika ufalme wa Mungu.

17 Akakipokea kikombe, akashukuru, akasema: Twaeni hiki mkagawanye ninyi kwa ninyi;

18 Maana nawaambieni, Sitakunywa tangu sasa mazao ya mzabibu hatta ufalme wa Mungu utakapokuja.

19 Akatwaa mkate, akashukuru, akaumega, akawapa, akisema, Huu ni mwili wangu unaotolewa kwa ajili yenu; fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu.

20 Nacho kikombe vivyo hivyo baada ya kula, akinena, Kikombe hiki ni agano jipya katika damu yangu, inayomwagika kwa ajili yenu.

21 Illa angalieni, mkono wake anisalitiye u pamoja nami mezani.

22 Kwa maana Mwana wa Adamu aenda zake kama ilivyoamriwa; lakini ole wake mtu yule ambae anasalitiwa nae!

23 Nao wakaanza kuulizana wao kwa wao, ni nani katika wao atakaetenda neno hili.

24 Kulikuwa na mashindano kwao, ni nani anaehesabiwa kuwa mkubwa.

25 Akawaambia, Wafalme wa Mataifa huwatawala, na wenye mamlaka juu yao huitwa wafadhili.

26 Lakini kwenu ninyi sivyo; bali aliye mkubwa wenu awe kama aliye mdogo; nafe atanguliae kama akhudumuye.

27 Maana nani mkubwa, aketiye chakulani, ama akhudumuye?

28 Siye aketiye chakulani? Lakini mimi kati mwenu kama akhudumuye.

29 Nanyi ndinyi mliodumu pamoja nami katika majaribu yangu. Nami nawawekea ninyi ufalme, kama alivyoniwekea Baba yangu;

30 mpate kula na kunywa mezani pangu katika ufalme wangu, na kuketi katika viti vya enzi, mkiwahukumu kabila thenashara za Israeli.

31 Bwana akasema, Simon, Simon, tazama, Shetani amewataka ninyi awapepete kama nganu:

32 lakini nimekuombea, illi imani yako isipunguke; nawe uongokapo, wathubutishe ndugu zako.

33 Akamwambia, Bwana, pamoja nawe mimi ni tayari kwenda gerezani na kufa.

34 Akasema, Nakuambia, Petro, jogoo hatawika leo, kabla hujanikana marra tatu kwamba hunijui.

35 Akawaambia, Nilipowatuma bila mifuko na mkoba na viatu, mlipunguka kitu? Wakasema, Hapana.

36 Akawaambia, Bali sasa mwenye kifuko akitwae, na mkoba vivyo hivyo; nae asiye na upanga, auze joho yake, akanunue mmoja.

37 Kwa maana nawaambieni, Hili lililoandikwa halina buddi kutimizwa kwangu, Alihesabiwa pamoja na maasi; kwa maana linipasalo lina mwisho.

38 Wakasema, Bwana, tazama, panga mbili hizi. Akawaambia, Zatosha.

39 Akatoka, akaenda zake hatta mlima wa mizeituni, kama ilivyo kawaida yake: wanafunzi wake wakamfuata.

40 Alipofika pahali pale, akawaambia, Ombeni, msiingie majaribuni.

41 Akiisha akajitenga nao kadiri ya mtupo wa jiwe, akapiga magoti, akaomba, akisema,

42 Baba, ukipenda, uniondolee kikombe hiki: lakini si kama nitakavyo mimi, illa utakavyo wewe vifanyike.

43 Akamtokea malaika toka mbinguni akimtia nguvu.

44 Nae kwa kuwa alikuwa na huzuni sana, akazidi kuomba kwa bidii. Hari yake ikawa kama matone ya damu yakidondoka hatta inchi.

45 Alipoondoka katika kuomba, akawajia wanafunzi wake, akawakuta wamelala kwa huzuni, akawaambia,

46 Mbona mnielala? Ondokeni, mkaombe, msipate kuingia majaribuni.

47 Nae alipokuwa akisema, tazama, makutano, nae aitwae Yuda, mmoja wa wathenashara, akitangulia mbele yao, akamkaribia Yesu kumbusu.

48 Yesu akamwambia, Yuda, wamsaliti Mwana wa Adamu kwa kumbusu?

49 Nao waliokuwa pamoja nae walipoona yatakayokuwa, wakasema, Bwana, na tupige kwa upanga?

50 Mmoja wao akampiga mtumishi wa kuhani mkuu, akamkata sikio la kuume.

51 Yesu akajibu, akasema, Acheni kadiri hii. Akamgusa sikio, akamponya.

52 Yesu akawaambia waliomjia, makuhani wakuu, na majemadari wa hekalu, na wazee, Kama juu ya mnyanyangʼanyi mmetoka kwa panga na marungu?

53 Killa siku nilipokuwa pamoja nanyi hekaluni hamkuninyoshea mikono; lakini saa yenu hii, na mamlaka ya giza.

54 Wakamkamata, wakamchukua, wakamleta nyumbani kwa kuhani mkuu; na Petro akafuata mbali.

55 Hatta walipowasha moto kati yasebule wakaketi pamoja, akaketi Petro kati yao.

56 Bassi, mjakazi mmoja akamwona ameketi mwangani, akamkazia macho akisema, Huyu nae alikuwa pamoja nae.

57 Akakana, akisema, Mwanamke, simjui.

58 Na punde baadae mwingine akamwona, akasema, Na wewe u mmoja wao. Petro akasema, Ewe mtu, sio mimi.

59 Hatta khalafu, kaciiri ya saa moja, mtu mwingine akahakikisha, akisema, Hakika na huyu alikuwa pamoja nae: kwa maana ni Mgalilaya.

60 Petro akasema, Ewe mtu, sijui unenalo. Papo hapo alipokuwa akisema yeye, jogoo akawika.

61 Bwana akageuka, akamtazamisha Petro: Petro akalikumbuka neno la Bwana, jinsi alivyomwambia, Kabla hajawika jogoo leo, utanikana marra tatu.

62 Akatoka nje, akalia kwa uchungu.

63 Na wale watu waliomshika Yesu, wakamdhihaki, wakampiga.

64 Wakamfunika macho, wakamwuliza, wakisema, Fanya unabii, ni nani aliyekupiga?

65 Wakamnena na mengine mengi kwa kufuru.

66 Hatta ulipokuwa mchana wakakusanyika jamii ya wazee wa watu, na makuhani wakuu, na waandishi, wakamleta kwa haraza yao, wakisema,

67 Kama wewe u Kristo, tuambie. Akawaambia, Nijapowaambieni, hamtaamini kabisa:

68 nami nikiwaulizeni, hamtanijibu wala kuniachilia.

69 Lakini tangu sasa Mwana wa Adamu atakuwa ameketi mkono wa kuume wa ukuu wa Mungu.

70 Wakasema wote, Bassi, wewe ndiwe Mwana wa Mungu? Akawaambia, Ninyi mnasema kama mimi ndiye.

71 Wakasema, Bassi, mbona tunahitaji ushuhuda? Kwa maana sisi wenyewe tumesikia kwa kinywa chake.

Swahili New Testament © Bible Society of Tanzania, 1921.

Bible Society of Tanzania
Tufuate:



Matangazo