Luka 20 - New Testament in Swahili (Zanzibar) Revised Edition 19211 IKAWA siku moja, alipokuwa akiwafundisha watu hekaluni na kuikhubiri Injili, makuhani wakuu na waandishi, na pamoja nao wazee, wakamtokea ghafula, 2 wakasema nae, wakinena, Kwa mamlaka gani unatenda haya? Na ni nani aliyekupa mamlaka hii? 3 Akajibu, akawaambia, Nami nitawauliza ninyi neno moja, kaniambieni. 4 Ubatizo wa Yohana, ulitoka mbinguni au kwa wana Adamu? 5 Wakasemezana wao kwa wao, wakinena, Kama tukisema, Toka mbinguni, atasema, Mbona hamkumwamini bassi? 6 Bali tukisema, Kwa wana Adamu, watu wote watatupiga mawe: kwa sababu wamesadiki ya kuwa Yohana ni nabii. 7 Wakajibu kwamba, Hatujui atokako. 8 Yesu akawaambia, Wala mimi siwaambii ninyi ni kwa mamlaka gani ninatenda haya. 9 Akaanza kuwaambia watu mfano huu: Mtu alipanda mizabibu, akapangisha wakulima, akaenda inchi nyingine kwa muda wa siku nyingi. 10 Na wakati wa mavuno akatuma mtumishi kwa wale wakulima illi wampe baadhi ya matunda ya mizabibu, wakulima wakampiga, wakamtoa hana kitu. 11 Akaongeza akampeleka mtumishi mwingine, wakampiga huyu wakamfedhehesha, wakamtoa hana kitu. 12 Akaongeza akampeleka wa tatu, wakamtia jeraha, wakamfukuza. 13 Yule Bwana wa mizabibu akasema, Nifanyeje? Nitampeleka mwana wangu, mpendwa wangu, labuda wakimwona yeye watamheshimu. 14 Lakini wale wakulima, walipomwona, wakafanya shauri wao kwa wao, wakinena, Huyu ndiye mrithi; na tumwue bassi, urithi upate kuwa wetu. 15 Wakamtupa nje ya shamba la mizabibu wakamwua. Bassi yule bwana wa shamba la mizabibu atawatendani? 16 Atakuja na kuwaangamiza wale wakulima, na lile shamba la mizabibu atawapa wengine. 17 Waliposikia wakasema, Mungu na apishe mbali. Akawakazia macho, akasema, Maana yake nini, bassi, neno hili lililoandikwa, Jiwe walilolikataa waashi Hili limekuwa jiwe kuu la pembeni? 18 Killa mtu aangukae juu ya jiwe hilo atavunjikavunjika, nae ambae litamwangukia litamsagasaga. 19 Makuhani wakuu na waandishi wakatafuta kumkamata saa hiyo hiyo, wakawaogopa watu: maana walitambua ya kuwa ule mfano amewanena wao. 20 Wakamvizia wakatuma wapelelezi, nao wakajifanya kuwa wenye haki, illi wamnase kwa neno lake, kusudi wamtie katika enzi na mamlaka ya liwali. 21 Wakamwuliza, wakinena, Mwalimu, twajua ya kuwa wanena yaliyo kweli na kuyafundisha, wala hujali cheo cha mtu, bali katika kweli waifundisha njia ya Mungu: 22 Je! ni halali kumpa Kaisari kodi au sivyo? 23 Lakini akatambua ujanja wao, akawaambia, 24 Nionyesheni dinari: ina sura ya nani? ina anwaui ya nani? Wakasema, ya Kaisari. 25 Akawaambia, Bassi, mpeni Kaisari yaliyo ya Kaisari, na Mungu yaliyo ya Mungu. 26 Wala hawakuweza kumshika kwa neno lake mbele ya watu: wakastaajabia jawabu lake, wakanyamaza. 27 Kiisha baadhi ya Masadukayo wakamwendea, watu wanenao ya kwamba hakuna kiyama: wakamwuliza, wakinena, 28 Mwalimu, Musa alituandikia ya kama ndugu ya mtu akifa, nae ana mke, na mtu huyo akifa hana mtoto, ni lazima ndugu yake amtwae yule mke, akampatie ndugu yake mzao. 29 Bassi, palikuwa na ndugu saba: wa kwanza akatwaa mke akafa, hana mtoto, 30 wa pili akamtwaa yule mke, akafa nae, hana mtoto. 31 Hatta wa tatu akamtwaa, na kadhalika hawa saba hawakuacha watoto, wakafa. 32 Mwisho wa hawo wote yule mwanamke akafa nae. 33 Bassi katika kiyama, atakuwa mke wa nani katika hawo? maana wale saba walikuwa nae. 34 Yesu akajibu akawaambia, Wana wa ulimwengu huu huoa, na kuozwa, 35 bali wao watakaohesabiwa wamestahili kuupata ulimwengu ule, na ufufuo wa wafu, hawaoi wala hawaozwi, 36 kwa kuwa hawawezi kufa tena, maana huwa sawasawa na malaika; tena ni wana wa Mungu kwa kuwa wana wa ule ufufuo. 37 Walakini ya kuwa wafu wafufuka, Musa nae alionyesha katika sura ya Kijiti, hapo amtajapo Bwana kuwa ni Mungu wa Ibrahimu, na Mungu wa Isaak, na Mungu wa Yakobo. 38 Bassi, yeye siye Muugu wa wafu, bali Mungu wa wahayi, maana wote ni wahayi kwake. 39 Baadhi ya waandishi wakajibu wakasema, Mwalimu, umesema vema. 40 Wala hakuthubutu mtu kumwuliza neno baada ya haya. 41 Akawaambia, Kwa maana gani hunena ya kwamba Kristo yu mwana wa Daud? 42 Na Daud mwenyewe asema katika chuo cha Zaburi, Bwana alimwambia Bwana wangu, Keti mkono wangu wa kuume, 43 Hatta niwafanyapo adui zako kuwa chini ya miguu yako. 44 Daud, bassi, amwita Bwana, na amekuwaje Mwana wake? 45 Hatta watu wote walipokuwa wakimsikiliza, akawaambia wanafunzi wake, 46 Jihadharini na waandishi wapendao kutembea wamevaa mavazi marefu, na kusalimiwa masokoni, na kuketi mbele katika sunagogi, na mahali palipo mbele katika karamu. 47 Wanakula nyumba za wajane: na kwa unafiki husali sala ndefu. Hawo watapokea hukumu iliyo kubwa zaidi. |
Swahili New Testament © Bible Society of Tanzania, 1921.
Bible Society of Tanzania