2 Wakorintho 11 - New Testament in Swahili (Zanzibar) Revised Edition 19211 INGEKUWA kheri kama mngenisamehe kidogo upumbavu wangu; naam, kanisameheni. 2 Maana nawaonea wivu, wivu wa Mungu; maana naliwaposea mume mmoja, nimletee Kristo bikira safi. 3 Lakini naogopa; kama yule nyoka alivyomdanganya Hawa kwa hila yake, asije akawaharibu fikara zenu, mkauacha unyofu wenu kwa Kristo. 4 Maana yeye ajae akikhubiri Yesu mwingine ambae sisi hatukumkhubiri, au mkipokea Roho nyingine msiyoipokea, au injili nyingine msiyoikubali, mnatenda vema kuvumilia nae. 5 Maana nadhani ya kuwa mimi sikupungukiwa kitu walicho nacho mitume walio wakuu. 6 Lakini nijapokuwa mimi ni mtu asiojua kunena, illakini hii si hali yangu katika ilmu; lakini katika killa neno tumedhihirishwa kwenu. 7 Je! nalifanya dhambi kwa kujinyenyekea illi ninyi mtukuzwe, kwa sababu naliwakhubiri Injili ya Kristo bila ujira? 8 Naliwanyangʼanya makanisa mengine mali yao, nikitwaa posho langu niwakhudumie ninyi. 9 Nami nilipokuwa pamoja nanyi na kuhitaji sikumlemea mtu. Maana ndugu walipokuja kutoka Makedonia walinipa kadiri ya mahitaji yangu; na katika mambo yote nalijilinda nafsi yangu nisiwalemee hatta kidogo; tena nitajilinda. 10 Kama vile kweli ya Kristo ilivyo ndani yangu, hapana mtu atakaenifumba kinywa katika kujisifu huku, katika mipaka ya Akaya. 11 Kwa nini? kwa sababu siwapendi ninyi? Mungu anajua. 12 Lakini nifanyalo nitalifunya, illi niwapinge watafutao nafasi wasipate nafasi; illi katika neno hilo wajisifulo waonekane kuwa kama sisi. 13 Maana hawo ni mitume wa uwongo, watendao kazi kwa hila, wanaojigeuza wawe mfano wa mitume ya Kristo. 14 Wala si ajabu. Maana Shetani mwenyewe hujigeuza awe mfano wa malaika wa nuru. 15 Bassi si neno kubwa wakhudumu wake nao wakijigeuza wawe mfano wa wakhudumu wa haki. Mwisho wao utakuwa sawasawa na kazi zao. 16 Nasema tena mtu asidhani ya kuwa mimi ni mpumbavu; lakini mjaponidhania hivi, mnikubali kama mpumbavu; mimi nami nipate kujisifu kidogo. 17 Nisemalo silisemi agizo la Bwana, bali kama kwa upumbavu, katika ujasiri huu wa kujisifu. 18 Iwapo wengi wanajisifu kwa jinsi ya mwili mimi nami nitajisifu. 19 Ninyi, kwa kuwa mna akili, mnavumilia na wajinga kwa furaha. 20 Maana mwavumilia na mtu akiwatieni utumwani, akiwameza, akiwateka, akijikuza, akiwapiga usoni. 21 Nanena kwa jinsi ya kujidhili kana kwamba sisi tulikuwa dhaifu. Illakini, akiwa mtu anao ujasiri kwa lo lote, (nanena kipuuzi), na mimi niuao ujasiri. 22 Wao Waebrania? Na mimi. Wao Waisraeli? Na mimi. Wao uzao wa Ibrahimu? Na mimi. 23 Wao wakhudumu wa Kristo? (nanena kiwazimu), mimi zaidi; kwa kazi kuzidi sana; kwa mapigo kupita kiasi; kwa vifungo kuzidi sana; kwa mauti marra nyingi. 24 Kwa Wayahudi marra tano nalipata mapigo arubaini kasoro moja. 25 Marra tatu nalipigwa bakora; marra moja nalipigwa mawe; marra tatu nalivunjikiwa jahazi; kuchwa kucha nimepata kukaa kilindini; 26 kwa kusafiri marra nyingi; khatari za mito; khatari za wanyangʼanyi; khatari kwa jamaa; khatari kwa mataifa; khatari za mijini; khatari za jangwani; khatari za baharini; khatari kwa ndugu za uwongo; 27 kwa kazi na kusumbuka; kwa kukesha marra nyingi; kwa njaa na kiu; kwa kufunga marra nyingi; kwa baridi na kuwa uchi. 28 Baghairi ya mambo ya nje, yako yanijiayo killa siku, ndio maangalizi ya makanisa yote. 29 Nani aliye dhaifu, nisiwe dhaifu na mimi? Nani aliyechukizwa na mimi nisiwake? 30 Ikinibidi kujisifu, nitajisifia mambo ya udhaifu wangu. 31 Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, aliye mtukufu hatta milele, ajua va kuwa sisemi nwongo. 32 Katika Dameski liwali wa Areta mfalme alikuwa akiulinda mji wa Wadameski, akitaka kunikamata; 33 nikashushwa ndani ya kapu, katika dirisha la ukutani, nikaokoka na mikono yake. |
Swahili New Testament © Bible Society of Tanzania, 1921.
Bible Society of Tanzania