1 Wakorintho 12 - New Testament in Swahili (Zanzibar) Revised Edition 19211 KWA khabari za karama za roho, ndugu, sitaki mkose kufahamu. 2 Mwajua ya kuwa mlipokuwa Mataifa mlichukuliwa kwa sanamu zisizonena, kama mlivyoongozwa. 3 Kwa hiyo nawaarifu, ya kwamba hapana mtu asemae katika Roho ya Mungu, anenae, Yesu ni anathema; wala hawezi mtu kusema, Yesu ni Bwana, isipokuwa katika Roho Mtakatifu. 4 Pana tofauti za karama; bali Roho yule yule. 5 Pana tofauti za khuduma, na Bwana vule yule; 6 pana tofauti za kutenda kazi, bali Mungu yule yule azitendae kazi zote katika wote. 7 Lakini killa mmoja hupewa ufunuo wa Roho illi kufaidia. 8 Maana mtu mmoja kwa Roho apewa neno la hekima; na mwingine neno la maarifa, ipendavyo Roho yule yule; 9 mwingine imani katika Roho yule yule; na mwingine karama za kuponya katika Roho yule mmoja; 10 na mwingine kutenda kazi za miujiza; na mwingine unabii; na mwingine kupambanua roho; mwingine aina za lugha; na mwingine tafsiri za lugha; 11 lakini kazi hizi zote huzitenda Roho huyo mmoja, yule yule, akimgawia killa mmoja peke yake kama apendavyo yeye. 12 Maana kama vile mwili ni mmoja, nao nna viungo vingi, na viungo vyote vya mwili ule mmoja, navyo ni vingi, ni mwili mmoja; vivyo hivyo na Kristo. 13 Kwa maana katika Roho mmoja sisi sote tulibatizwa tukaingia katika mwili mmoja, ikiwa tu Wayahudi, au ikiwa tu Wayunani; ikiwa tu watumwa au ikiwa tu huru; nasi sote tulinyweshwa Roho mmoja. 14 Kwa maana mwili hauwi kiungo kimoja, bali vingi. 15 Mguu ukisema, Kwa kuwa mimi si mkono, mimi si wa mwili; je! si wa mwili kwa sababu hiyo? 16 Na sikio likisema, Mimi si jicho, mimi si wa mwili; je! si wa mwili kwa sababu hiyo? 17 Kama mwili wote ukiwa jicho, ku wapi kusikia? kama wote ni sikio ku wapi kuona? 18 Bali Mungu amevitia viungo killa kimoja katika mwili kama alivyotaka. 19 Lakini kama vyote vingekuwa kiungo kimoja, mwili ungekuwa wapi? 20 Lakini sasa viungo ni vingi, na mwili ni mmoja. 21 Na jicho haliwezi kuuambia mkono, Sina haja na wewe; wala tena kichwa hakiwezi kuiambia miguu, Sina baja na ninyi. 22 Bali zaidi sana vile viungo vya mwili vidhaniwavyo kuwa vinyonge zaidi vyahitajiwa zaidi. 23 Na vile vidhaniwavyo kuwa havina heshima, viungo vile twavipa heshima zaidi; na viungo vyetu visivyo na uzuri vina uzuri zaidi sana. 24 Kwa maana viungo vyetu vilivyo na uzuri havina uhitaji; hali Mungu ameuungamanisha mwili, na kukipa heshima kile kiungo kilichopungukiwa; 25 illi kusiwe fitina katika mwili, hali viungo vitunzane. 26 Na kiungo kimoja kikiumia, viungo vyote huumia navyo, na kiungo kimoja kikitukuzwa, viungo vyote hufurahi pamoja. 27 Na ninyi m mwili wa Kristo, na viungo vya mwili huo, mmoja hiki na mmoja hiki. 28 Na Mungu ameweka wengine katika Kanisa, wa kwanza mitume, wa pili manabii, wa tatu waalimu, kiisha miujiza, kiisha karama za kuponya wagonjwa, na masaidiano, na kutawala, na aina za lugha. 29 Je! wote ni mitume? wote ni manabii? wote ni waalimu? wote wanatenda miujiza? 30 wote wana karama za kuponya wagonjwa? wote wanena lugha? wote wafasiri? Takeni sana karama zilizo njema zaidi. 31 Na tena nawaonyesha njia iliyo bora sana. |
Swahili New Testament © Bible Society of Tanzania, 1921.
Bible Society of Tanzania