1 Timotheo 3 - New Testament in Swahili (Zanzibar) Revised Edition 19211 AMINI neno hili, Mtu akitaka uaskofu, atamani kazi nzuri. 2 Bassi imempasa askofu kuwa mtu asiyelaumiwa, mume wa mke mmoja, mwenye kiasi na busara, mtu wa utaratibu, mkaribishaji, mfundishaji; 3 si mtu wa kuzoelea mvinyo, si mpigaji, si mtu apendae fedha; bali awe mpole, asiwe mtu wa kujadiliana, asitamani fedha; 4 mwenye kusimamia vema nyumba yake, ajuae kuwatiisha watoto wake pamoja na kustahiwa; 5 (mtu asiyejua kuisimamia nyumba yake mwenyewe, atalitunzaje kanisa la Mungu?) 6 si mtu aliyeongoka karibu, asije akajivuna, akaanguka katika hukumu ya Shetani. 7 Imempasa tena kushuhudiwa mazuri na watu walio nje; asitumbukie katika lawama na mtego wa Shetani. 8 Vivi hivi mashemasi, wawe watu wa utaratibu, si wenye nia mbili, si watu wa kutumia mvinyo nyingi, wawe watu wasiotamani fedha ya aibu; 9 wakiishika siri ya imani katika dhamiri safi. 10 Na hawa pia wajaribiwe kwanza; baadae watumie daraja ya ushemasi, wakiisha kuonekana hawana khatiya. 11 Vivi hivi wanawake wawe watu wa utaratibu, si wasingiziaji, watu wa kiasi, waaminifu katika mambo yote. 12 Mashemasi wawe na mke mmoja, wakiwasimamia watoto wao vizuri, na nyumba zao. 13 Kwa maana watendao kazi ya ushemasi vema hujipatia daraja nzuri, na ujasiri mwingi katika imani iliyo katika Kristo Yesu. 14 Nakuandikia haya, nikitaraja kuja kwako karibu. 15 Lakini nikikawia, upate kujua sana jinsi iwapasavyo watu kuenenda katika nyumba ya Mungu iliyo kanisa la Mungu aliye hayi, nguzo na msingi wa kweli. 16 Na bila shaka siri ya utawa ni kuu. Mungu alidhibirishwa katika mwili, alihesabiwa kuwa na wema katika roho, alionekana na malaika, alikhubiriwa katika mataifa, aliaminiwa katika ulimwengu, alichukuliwa juu katika utukufu. |
Swahili New Testament © Bible Society of Tanzania, 1921.
Bible Society of Tanzania