Biblia Todo Logo
Biblia ya mtandaoni
- Matangazo -

Mathayo 22 - BIBLIA KISWAHILI


Mfano wa Karamu ya harusi

1 Yesu akajibu, akawaambia tena kwa mifano, akisema,

2 Ufalme wa mbinguni unafanana na mfalme mmoja aliyemfanyia mwanawe harusi.

3 Akawatuma watumwa wake wawaite walioalikwa kuja harusini; nao wakakataa kuja.

4 Akatuma tena watu kwa wengine, akisema, Waambieni wale walioalikwa, Tazameni, nimeandaa karamu yangu; ng'ombe zangu na vinono vimekwisha kuchinjwa, na vyote vimekuwa tayari, njoni harusini.

5 Lakini hawakujali, wakaenda zao, mmoja shambani kwake, mmoja kwenye biashara yake;

6 nao waliosalia wakawakamata watumwa wake, wakawadhulumu na kuwaua.

7 Basi yule mfalme akaghadhibika; akatuma majeshi yake, akawaangamiza wauaji wale, akauteketeza mji wao.

8 Kisha akawaambia watumwa wake, Harusi iko tayari, lakini wale walioalikwa hawakustahili.

9 Basi Nendeni hata njia panda za barabara, na wote mwaonao waiteni harusini.

10 Watumwa wale wakatoka wakaenda njia kuu, wakakusanya wote waliowaona, waovu kwa wema; harusi ikajaa wageni.

11 Lakini alipoingia yule mfalme ili kuwatazama wageni wake, akaona mle mtu mmoja asiyevaa vazi la harusi.

12 Akamwambia, Rafiki, uliingiaje humu nawe huna vazi la harusi? Naye akatekewa.

13 Mfalme akawaambia watumishi, Mfungeni mikono na miguu, mchukueni mkamtupe katika giza la nje; ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno.

14 Kwa maana waitwao ni wengi, bali wateule ni wachache.


Swali juu ya kulipa kodi

15 Ndipo Mafarisayo wakaenda zao, wakafanya shauri, jinsi ya kumtega kwa maneno.

16 Wakatuma kwake wanafunzi wao pamoja na Maherodi, wakasema, Mwalimu, tunajua ya kuwa wewe u mtu wa kweli, na njia ya Mungu waifundisha katika kweli, wala hujali cheo cha mtu awaye yote, kwa maana hutazami sura za watu.

17 Basi utuambie, Waonaje? Ni halali kumpa Kaisari kodi, ama sivyo?

18 Lakini Yesu akaufahamu uovu wao, akasema, Mbona mnanijaribu, enyi wanafiki?

19 Nionesheni fedha ya kodi. Nao wakamletea dinari.

20 Akawaambia, Ni ya nani sanamu hii, na anwani hii?

21 Wakamwambia, Ni ya Kaisari. Akawaambia, Basi, mpeni Kaisari yaliyo ya Kaisari, na Mungu yaliyo ya Mungu.

22 Waliposikia, walistaajabu, wakamwacha, wakaenda zao.


Swali kuhusu ufufuo

23 Siku ile Masadukayo, watu wasemao ya kwamba hakuna kiyama, wakamwendea, wakamwuliza,

24 wakisema, Mwalimu, Musa alisema, Mtu akifa, akiwa hana watoto, ndugu yake na amwoe yule mkewe, ili ampatie nduguye mzao.

25 Basi, kwetu kulikuwa na ndugu saba; wa kwanza akaoa, akafariki, na kwa kuwa hana mzao, akamwachia nduguye mke wake.

26 Vivyo hivyo wa pili naye, na wa tatu, hata wote saba.

27 Mwisho wa wote yule mwanamke akafa naye.

28 Basi, katika kiyama, atakuwa mke wa yupi kati ya wale saba? Maana wote walikuwa naye.

29 Yesu akajibu, akawaambia, Mnapotea, kwa kuwa hamyajui maandiko wala uweza wa Mungu.

30 Kwa maana katika kiyama hawaoi wala hawaolewi, bali huwa kama malaika mbinguni.

31 Tena kuhusu kiyama ya wafu, hamjalisoma neno lililonenwa na Mungu, akisema,

32 Mimi ni Mungu wa Abrahamu, na Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo? Mungu si Mungu wa wafu, bali wa walio hai.

33 Na makutano waliposikia, walishangaa kwa mafunzo yake.


Amri iliyo kuu zaidi

34 Na Mafarisayo waliposikia ya kwamba amewafumba kinywa wale Masadukayo, walifanya shauri pamoja.

35 Mmoja wao, mwanasheria, akamwuliza, akimjaribu;

36 Mwalimu, katika torati ni amri ipi iliyo kuu?

37 Akamwambia, Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote.

38 Hii ndiyo amri iliyo kuu, tena ni ya kwanza.

39 Na ya pili yafanana nayo, nayo ni hii, Mpende jirani yako kama nafsi yako.

40 Katika amri hizi mbili hutegemea Torati yote na vitabu vya Manabii.


Swali kuhusu Mwana wa Daudi

41 Na Mafarisayo walipokusanyika, Yesu aliwauliza, akisema, Mnaonaje kuhusu Kristo?

42 Ni mwana wa nani? Wakamwambia, Ni wa Daudi.

43 Akawauliza, Imekuwaje basi Daudi katika Roho kumwita Bwana, akisema,

44 Bwana alimwambia Bwana wangu, Uketi katika mkono wangu wa kulia, Hata niwawekapo adui zako Kuwa chini ya miguu yako?

45 Basi, Daudi akimwita Bwana, amekuwaje ni mwanawe?

46 Wala hakuweza mtu kumjibu neno; wala hakuthubutu mtu yeyote tangu siku ile kumwuliza neno tena.

The Holy Bible in Kiswahili, Revised Union Version © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 2013. 

Bible Society of Tanzania
Tufuate:



Matangazo