Mwito wa kuabudu na kutii1 Njoni, tumwimbie BWANA, Tumfanyie shangwe mwamba wa wokovu wetu. 2 Tuje mbele zake kwa shukrani, Tumfanyie shangwe kwa zaburi. 3 Kwa kuwa BWANA ni Mungu mkuu, Na Mfalme mkuu juu ya miungu yote. 4 Mkononi mwake zimo bonde za dunia, Hata vilele vya milima ni vyake. 5 Bahari ni yake, ndiye aliyeifanya, Na mikono yake iliumba nchi kavu. 6 Njoni, tuabudu, tusujudu, Tupige magoti mbele za BWANA aliyetuumba. 7 Kwa maana ndiye Mungu wetu, Na sisi tu watu wa malisho yake, Na kondoo za mkono wake. Ingekuwa heri leo msikie sauti yake! 8 Msifanye mioyo yenu kuwa migumu; Kama ilivyokuwa huko Meriba Kama siku ile katika Masa jangwani. 9 Hapo waliponijaribu baba zenu, Wakanipima, wakayaona matendo yangu. 10 Miaka arubaini nilichukizwa na kizazi kile, Nikasema, Hawa ni watu wenye mioyo inayopotoka, Na wanaopuuza njia zangu. 11 Ndipo Nikaapa kwa hasira yangu Hawataingia katika pumziko langu. |
Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Bible Society of Kenya