Sala ya msaada katika wakati wa kukata tamaa Wimbo. Zaburi ya Wakorahi. Kwa mwimbishaji: kwa mtindo wa Mahalathi. Utenzi wa Hemani Mwezrahi.1 Ee BWANA, Mungu wa wokovu wangu Mchana na usiku nimelia mbele zako. 2 Maombi yangu yafike mbele zako, Ukitegee kilio changu sikio lako. 3 Maana nafsi yangu imeshiba taabu, Na uhai wangu umekaribia kuzimu. 4 Nimehesabiwa pamoja nao washukao shimoni; Nimekuwa kama mtu asiye na msaada. 5 Miongoni mwao waliokufa nimetupwa, Kama waliouawa walalao makaburini. Hao ambao Wewe huwakumbuki tena, Wametengwa mbali na mkono wako. 6 Mimi umenilaza chini katika shimo, Katika mahali penye giza vilindini. 7 Ghadhabu yako imenilemea, Umenitesa kwa mawimbi yako yote. 8 Wanijuao umewatenga nami; Umenifanya kuwa chukizo kwao; Nimefungwa wala siwezi kutoka. 9 Jicho langu limefifia kwa ajili ya mateso BWANA, ninakuita kila siku; Ninakunyoshea Wewe mikono yangu. 10 Je! Wafu utawafanyia miujiza? Au waliofariki watasimama na kukuhimidi? 11 Fadhili zako zitasimuliwa kaburini? Au uaminifu wako katika uharibifu? 12 Miujiza yako itajulikana gizani? Au haki yako katika nchi ya usahaulifu? 13 Lakini mimi nimekulilia Wewe, BWANA, Na asubuhi maombi yangu yatakuwasilia. 14 BWANA, kwa nini kuitupa nafsi yangu, Na kunificha uso wako? 15 Nimeteswa tangu ujana wangu na niko karibu kufa, Nimeumia kwa mapigo yako; nami nimekata tamaa. 16 Hasira zako kali zimenizidia, Mapigo yako yatishayo yameniangamiza. 17 Yamenizunguka kama mafuriko mchana kutwa, Yamenisonga kwa kila upande. 18 Mpenzi na rafiki umewatenga nami, Nao wanijuao wamo gizani. |
Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Bible Society of Kenya