Wema wa Mungu na Israeli kukosa shukrani Utenzi wa Asafu.1 Enyi watu wangu, sikilizeni sheria yangu, Tegeni masikio kwa maneno ya kinywa changu. 2 Nitafumbua kinywa changu kwa mithali, Niyatamke mafumbo ya kale. 3 Mambo tuliyoyasikia na kuyafahamu, Ambayo baba zetu walituambia. 4 Hayo hatutawaficha wana wao, Huku tukiwaambia kizazi kingine, Sifa za BWANA, na nguvu zake, Na mambo yake ya ajabu aliyoyafanya. 5 Maana alikaza ushuhuda katika Yakobo, Na sheria aliiweka katika Israeli. Aliyowaamuru baba zetu Wawajulishe wana wao, 6 Ili kizazi kingine wawe na habari, Ndio hao wana watakaozaliwa. Wasimame na kuwaambia wana wao. 7 Wamwekee Mungu tumaini lao. Wala wasiyasahau matendo ya Mungu, Bali wazishike amri zake. 8 Naam, wasiwe kama baba zao, Kizazi cha ukaidi na uasi. Kizazi kisichojitengeneza moyo, Wala roho yake haikuwa amini kwa Mungu. 9 Wale Waefraimu, wenye silaha, wapiga upinde, Walirudi nyuma siku ya vita. 10 Hawakulishika agano la Mungu; Wakakataa kufuata sheria yake; 11 Wakayasahau matendo yake, Na mambo yake ya ajabu aliyowaonesha. 12 Mbele ya baba zao alifanya mambo ya ajabu, Katika nchi ya Misri, konde la Soani. 13 Aliipasua bahari akawavusha; Aliyafanya maji yasimame kama ukuta. 14 Akawaongoza kwa wingu mchana, Na usiku kucha kwa nuru ya moto. 15 Akapasua miamba jangwani; Akawanywesha maji mengi kama maji ya vilindi. 16 Akafanya vijito vitokeze katika mwamba, Na kufanya maji yatiririke kama mito. 17 Lakini wakazidi kumtenda dhambi, Walipomwasi Aliye Juu katika jangwa. 18 Wakamjaribu Mungu mioyoni mwao Kwa kutaka chakula kwa tamaa zao. 19 Naam, walimwambia Mungu, wakasema, Je! Mungu aweza kuandaa meza jangwani? 20 Tazama, aliupiga mwamba; Maji yakabubujika, ikafurika mito. Pia aweza kutupa chakula? Atawaandalia watu wake nyama? 21 Hivyo BWANA aliposikia akaghadhibika; Moto ukawashwa juu ya Yakobo, Hasira nayo ikapanda juu ya Israeli. 22 Kwa kuwa hawakumwamini Mungu, Wala hawakuutumainia wokovu wake. 23 Lakini aliyaamuru mawingu juu; Akaifungua milango ya mbinguni; 24 Akawanyeshea mana ili wale; Akawapa nafaka ya mbinguni. 25 Mwanadamu akala chakula walacho malaika; Akawapelekea chakula cha kuwashibisha. 26 Aliuelekeza upepo wa mashariki kuvuma toka mbinguni; Na kwa uweza wake akauongoza upepo wa kusini. 27 Akawanyeshea nyama kama mavumbi, Na ndege wenye mbawa, Kama mchanga wa bahari. 28 Akawaangusha kati ya matuo yao, Pande zote za maskani zao. 29 Wakala wakashiba sana; Maana aliwaletea walivyovitamani; 30 Lakini kabla ya kuitosheleza shauku yao, Huku chakula kikiwa bado kinywani mwao, 31 Hasira ya Mungu ikapanda juu yao, Akawaua waliokuwa wanono; Akawaangusha chini vijana wa Israeli. 32 Pamoja na hayo wakazidi kutenda dhambi, Wala hawakuyaamini matendo yake ya ajabu. 33 Kwa hiyo akazikomesha siku zao kama pumzi, Na miaka yao kwa hofu ya kuwastusha. 34 Alipowaua ndipo walipokuwa wakimtafuta; Wakarudi wakamtaka Mungu kwa bidii. 35 Wakakumbuka kuwa Mungu ni mwamba wao, Na Mungu Aliye Juu ni mkombozi wao. 36 Lakini walimdanganya kwa vinywa vyao, Wakamwambia uongo kwa ndimi zao. 37 Kwa maana mioyo yao haikuwa thabiti kwake, Wala hawakuwa waaminifu katika agano lake. 38 Lakini Yeye, kwa kuwa anayo rehema, Husamehe uovu wala haangamizi. Mara nyingi huipishia mbali ghadhabu yake, Wala haiwashi hasira yake yote. 39 Akakumbuka ya kuwa wao ni kiwiliwili, Upepo upitao wala haurudi. 40 Walimwasi jangwani mara ngapi? Na kumhuzunisha nyikani! 41 Wakamjaribu Mungu tena na tena; Na kumkasirisha Mtakatifu wa Israeli. 42 Hawakuukumbuka mkono wake, Wala siku ile alipowakomboa na mtesi. 43 Alivyoziweka ishara zake katika Misri, Na miujiza yake katika uwanda wa Soani. 44 Aligeuza mito yao kuwa damu, Ili wasipate kunywa maji kutoka vijito vyao. 45 Aliwapelekea mainzi wakawala, Na vyura wakawaharibu. 46 Akawapa tunutu mazao yao, Na nzige matunda ya kazi yao. 47 Aliiharibu mizabibu yao kwa mvua ya mawe, Na mikuyu yao kwa mawe ya barafu. 48 Akaacha ng'ombe zao wapigwe kwa mvua ya mawe, Na makundi yao kwa umeme. 49 Akawapelekea ukali wa hasira yake, Ghadhabu, na uchungu, na taabu, Kundi la malaika waletao mabaya. 50 Akaifanyia njia hasira yake; Wala hakuziepusha roho zao kutoka kwa mauti, Bali aliiachia tauni uhai wao; 51 Akampiga kila mzaliwa wa kwanza wa Misri, Malimbuko ya nguvu katika hema za Hamu. 52 Kisha akawaongoza watu wake kama kondoo, Akawachunga kama kundi jangwani. 53 Hao akawachukua salama wala hawakuogopa, Bali bahari iliwafunika adui zao. 54 Akawapeleka hadi mpaka wake mtakatifu, Mlima alioununua kwa mkono wake wa kulia. 55 Akawafukuza mataifa mbele yao, Akawapimia urithi kwa kamba, Na kuwakalisha makabila ya Israeli katika hema zao. 56 Lakini walimjaribu Mungu Aliye Juu, wakamwasi, Wala hawakuzishika shuhuda zake. 57 Bali walirudi nyuma, wakahaini kama baba zao; Wakayumba kama upinde usiofaa. 58 Wakamkasirisha kwa mahali pao pa juu, Wakamtia wivu kwa sanamu zao. 59 Mungu alisikia, akaghadhibika, Akamkataa Israeli kabisa. 60 Akaiacha maskani ya Shilo, Hema aliyoiweka katikati ya wanadamu; 61 Akaziacha nguvu zake kutekwa, Na fahari yake mkononi mwa mtesi. 62 Akawatoa watu wake wapigwe kwa upanga; Akaughadhibikia urithi wake. 63 Moto ukawala vijana wao, Wanawali wao hawakuimbiwa nyimbo za arusi, 64 Makuhani wao walianguka kwa upanga, Wala wajane wao hawakuomboleza. 65 Ndipo Bwana alipoamka kama aliyelala usingizi, Kama shujaa apigaye kelele kwa sababu ya mvinyo; 66 Akawapiga watesi wake akawarudisha nyuma, Akawatia aibu ya milele. 67 Ila akaikataa hema ya Yusufu; Wala hakuichagua kabila la Efraimu. 68 Bali aliichagua kabila la Yuda, Mlima Sayuni alioupenda. 69 Akajenga patakatifu pake kama vilele, Kama dunia aliyoiweka imara milele. 70 Akamchagua Daudi, mtumishi wake, Akamwondoa katika mazizi ya kondoo. 71 Nyuma ya kondoo wanyonyeshao alimwondoa, Awachunge Yakobo watu wake, na Israeli urithi wake. 72 Akawahudumia kwa ukamilifu wa moyo wake, Na kuwaongoza kwa busara ya mikono yake. |
Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Bible Society of Kenya