Kusubiri wokovu wa Mungu Wimbo wa kupanda mlima.1 Ee BWANA, toka vilindini nimekulilia. 2 Bwana, uisikie sauti yangu. Masikio yako na yaisikilize Sauti ya dua zangu. 3 BWANA, kama Wewe ungehesabu maovu, Ee Bwana, nani angesimama? 4 Lakini kwako kuna msamaha, Ili Wewe uogopwe. 5 Nimemngoja BWANA, roho yangu imengoja, Na neno lake nimelitumainia. 6 Nafsi yangu inamngoja Bwana, Kuliko walinzi waingojavyo asubuhi, Naam, walinzi waingojao asubuhi. 7 Ee Israeli, umtarajie BWANA; Maana kwa BWANA kuna fadhili, Na kwake kuna ukombozi mwingi. 8 Yeye atamkomboa Israeli na maovu yake yote. |
Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Bible Society of Kenya