Ombi la msaada wakati wa dhiki Kwa mwimbishaji: kwa kufuata Sheminithi. Zaburi ya Daudi.1 Tuokoe, ee BWANA, maana hamna tena amchaye Mungu Maana waaminifu wametoweka katika wanadamu. 2 Husemezana yasiyofaa kila mtu na mwenziwe, Wenye midomo ya kujipendekeza; Husemezana kwa mioyo ya unafiki; 3 BWANA ataikata midomo yote ya kujipendekeza, Na ulimi unenao maneno ya kiburi; 4 Waliosema, Kwa ndimi zetu tutashinda; Midomo yetu ni yetu wenyewe, Ni nani aliye bwana juu yetu? 5 Kwa ajili ya kuonewa kwao wanyonge, Kwa ajili ya kuugua kwao wahitaji, Sasa nitasimama, asema BWANA, Nitamweka salama yeye wanayemfyonya. 6 Maneno ya BWANA ni maneno safi, Ni fedha iliyojaribiwa kalibuni juu ya nchi; Iliyosafishwa mara saba. 7 Wewe, BWANA, ndiwe utakayetuhifadhi, Utatulinda na kizazi hiki milele. 8 Wasio haki hutembea pande zote, Huku ufisadi ukitukuka kati ya wanadamu. |
Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Bible Society of Kenya