Israeli na Yuda waahidiwa kurudishwa1 Neno hili ndilo lililomjia Yeremia, kutoka kwa BWANA, kusema, 2 BWANA Mungu wa Israeli, asema hivi, ya kwamba, Uyaandike kitabuni maneno hayo yote niliyokuambia. 3 Kwa maana, tazama, siku zinakuja, asema BWANA, nitakapowarejesha watu wangu wa Israeli na Yuda waliofungwa, asema BWANA; nami nitawarudisha hadi katika nchi niliyowapa baba zao, nao wataimiliki. 4 Na haya ndiyo maneno aliyosema BWANA, kuhusu Israeli, na kuhusu Yuda. 5 Maana BWANA asema hivi, Tumesikia sauti ya tetemeko, na ya hofu, wala si ya amani. 6 Ulizeni sasa, mkaone kwamba mwanamume aona uchungu wa uzazi; mbona, basi, ninaona kila mtu anaweka mikono yake viunoni, kama mwanamke aliye na uchungu, na nyuso zote zimegeuka rangi? 7 Ole! Maana siku ile ni kuu, hata hapana inayofanana nayo, maana ni wakati wa taabu yake Yakobo; lakini ataokolewa kutoka kwayo. 8 Na itakuwa katika siku ile, asema BWANA wa majeshi, nitaivunja nira yake itoke shingoni mwako, nami nitavipasua vifungo vyako; wala wageni hawatamtumikisha tena; 9 bali watamtumikia BWANA, Mungu wao, na Daudi, mfalme wao, nitakayemwinua kwa ajili yao. 10 Kwa sababu hiyo usiogope, Ee Yakobo, mtumishi wangu, asema BWANA; wala usifadhaike, Ee Israeli; kwa maana, tazama, nitakuokoa toka mbali, na wazao wako toka nchi ya uhamisho wao; na Yakobo atarudi, naye atatulia na kustarehe, wala hapana mtu atakayemtia hofu. 11 Maana mimi ni pamoja nawe, asema BWANA, nikuokoe; maana nitawakomesha kabisa mataifa yote huko nilikokutawanya, bali sitakukomesha wewe kabisa; lakini nitakurudi kwa hukumu, wala sitakuacha bila adhabu. 12 Maana BWANA asema hivi, Maumivu yako hayaponyeki, na jeraha lako ni kubwa. 13 Hapana mtu wa kukutetea; kwa jeraha lako huna dawa ziponyazo. 14 Wote wakupendao wamekusahau; hawakutafuti; maana nimekujeruhi kwa jeraha la adui, kwa adhabu ya mtu mkatili; kwa sababu ya ukubwa wa uovu wako, kwa sababu dhambi zako zilikuwa zimeongezeka. 15 Mbona unalilia maumivu yako? Maumivu yako hayaponyeki; kwa sababu ya ukubwa wa uovu wako, kwa sababu dhambi zako zimeongezeka, nimekutenda haya. 16 Basi, watu wote wakulao wataliwa; na adui zako wote watakwenda kufungwa; kila mmoja wao; na hao waliokuteka nyara watatekwa; na wote waliokuwinda nitawafanya kuwa mawindo. 17 Maana nitakurudishia afya, nami nitakuponya majeraha yako, asema BWANA, kwa sababu wamekuita, mwenye kutupwa, wakisema, Ni Sayuni, mji ambao hakuna mtu autakaye. 18 BWANA asema hivi, Tazama, nitarudisha tena hema za Yakobo zilizohamishwa, na kuyahurumia makao yake; nao mji huo utajengwa juu ya magofu yake wenyewe, nalo jumba litakaliwa, kama ilivyokuwa desturi yake. 19 Tena kwao itasikiwa shukrani, na sauti yao wachangamkao; nami nitawazidisha, wala hawatakuwa wachache; tena nitawatukuza, wala hawatakuwa wanyonge. 20 Watoto wao nao watakuwa kama zamani, na kusanyiko lao litathibitika mbele zangu, nami nitawaadhibu wote wanaowaonea. 21 Na mkuu wao atakuwa mtu wa kwao wenyewe, naye mwenye kuwatawala atakuwa mtu wa jamaa yao; nami nitamkaribisha, naye atanikaribia; maana ni nani aliye na moyo wa kuthubutu kunikaribia? Asema BWANA. 22 Nanyi mtakuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu wenu. 23 Tazama, tufani ya BWANA, yaani, ghadhabu yake, imetokea tufani ya kudumu; itawaangukia waovu vichwani. 24 Hasira kali ya BWANA haitarudi, hadi atakapokwisha kutenda na kuyatimiza makusudi ya moyo wake; katika siku za mwisho mtayafahamu haya. |
Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Bible Society of Kenya