Matumizi ya sadaka takatifu1 Kisha BWANA akanena na Musa, na kumwambia, 2 Nena na Haruni na wanawe, ili washughulikie kwa uangalifu vitu vitakatifu vya wana wa Israeli ambavyo wanitakasia mimi, tena wasilinajisi jina langu takatifu; mimi ndimi BWANA. 3 Waambie, Mtu yeyote wa kizazi chenu chote katika vizazi vyenu, atakayevikaribia vile vitu vitakatifu, ambavyo wana wa Israeli wamtakasia BWANA, naye ana unajisi, mtu huyo atatengwa asiwe mbele zangu; mimi ndimi BWANA. 4 Mtu yeyote wa kizazi cha Haruni aliye na ukoma, au kisonono; asile katika vitu vitakatifu, hata atakapokuwa safi. Tena mtu yeyote atakayekinusa kitu kilicho na unajisi kwa sababu ya wafu, au mtu ambaye shahawa humtoka; 5 au mtu amgusaye mnyama atambaaye, wa kumpatia unajisi, au kwamba amgusa mtu wa kumpatia unajisi, kwa unajisi wowote ule alio nao; 6 huyo mtu atakayegusa kitu chochote namna hiyo atakuwa najisi hata jioni, naye hatakula katika vitu vitakatifu, asipooga mwili wake majini. 7 Jua likiisha kuchwa atakuwa safi; kisha baadaye atakula katika vitu vitakatifu, maana ni chakula chake. 8 Nyamafu au mnyama aliyeraruliwa na wanyama asile, asijitie unajisi kwa hiyo nyama; mimi ndimi BWANA. 9 Basi kwa hiyo watayashika maagizo yangu, wasije wakachukua dhambi kwa hayo, nao wakafa humo, wakiyanajisi; mimi ndimi BWANA niwatakasaye. 10 Mgeni yeyote asile katika kitu kitakatifu; mgeni wa kuhani akaaye kwake, au mtumishi aliyeajiriwa, asile katika kitu kitakatifu. 11 Lakini kuhani akinunua mtu yeyote kwa fedha zake, yeye atakula katika hicho; na hao waliozaliwa nyumbani mwake watakula katika chakula chake. 12 Na binti ya kuhani ikiwa ameolewa na mgeni, asile katika sadaka ya kuinuliwa katika vitu vile vitakatifu. 13 Lakini ikiwa binti ya kuhani ni mjane, au ameachwa na mumewe, wala hana mtoto, kisha amerudi na kuishi katika nyumba ya baba yake, kama vile katika ujana wake, yeye atakula katika chakula cha baba yake; lakini mgeni yeyote asile katika chakula hicho. 14 Tena kama mtu yeyote akila katika kitu kilicho kitakatifu pasipo kukijua, ndipo ataongeza sehemu ya tano juu ya kitu hicho, na kumpa kuhani kitu hicho kitakatifu. 15 Wala wasivinajisi vitu vitakatifu vya wana wa Israeli, wavisongezavyo kwa BWANA; 16 hata wakawatwika ule uovu uletao hatia, hapo walapo vitu vyao vitakatifu; kwa kuwa mimi ndimi BWANA niwatakasaye. Sadaka zinazokubalika17 Kisha BWANA akanena na Musa, na kumwambia, 18 Nena na Haruni na wanawe, na wana wa Israeli wote, uwaambie, Mtu yeyote wa nyumba ya Israeli, au wa wageni walio katika Israeli, atakayetoa matoleo yake, kama ni mojawapo ya nadhiri zao, au kama ni sadaka yoyote ya hiari, watakayomtolea BWANA kuwa sadaka ya kuteketezwa; 19 ili mpate kukubaliwa, mtaleta dume mkamilifu, katika ng'ombe, au katika kondoo, au katika mbuzi. 20 Lakini mnyama yeyote aliye na kilema msimtoe; kwa kuwa hatakubaliwa kwa ajili yenu. 21 Na mtu yeyote atakayemtolea BWANA dhabihu katika sadaka za amani, ili kuondoa nadhiri, au sadaka ya moyo wa kupenda, katika ng'ombe, au katika kondoo, atakuwa mkamilifu, apate kukubaliwa; pasiwe na kilema chochote ndani yake. 22 Kipofu, au aliyevunjika mahali, au kiwete au aliye na vidonda, au aliye na upele, au aliye na upele, hamtamtolea BWANA wanyama hao, wala msiwasongeze kwa BWANA kwa njia ya moto juu ya madhabahu. 23 Ng'ombe, au mwana-kondoo aliye na kitu kilichozidi, au aliyepungukiwa na kitu katika vitu vya mwilini mwake, mna ruhusa kutoa kuwa sadaka ya moyo wa kupenda; lakini kwa ajili ya nadhiri hatakubaliwa. 24 Mnyama aliyeumia mapumbu yake, au kusetwa, au kuvunjwa, au kukatwa, msimtolee BWANA; wala msifanye hivi katika nchi yenu. 25 Wala msisongeze chakula cha Mungu wenu katika wanyama hao mmojawapo kitokacho mkononi mwa mgeni; kwa sababu uharibifu wao uko ndani yao, wana kilema ndani yao; hawatakubaliwa kwa ajili yenu. 26 Kisha BWANA akanena na Musa, na kumwambia, 27 Hapo ng'ombe, kondoo au mbuzi, akizaliwa, atakuwa pamoja na mamaye muda wa siku saba; na siku ya nane na baadaye atakubaliwa kuwa ni sadaka ya kutolewa kwa BWANA kwa njia ya moto. 28 Tena kama ni ng'ombe, au kondoo, msimchinje huyo na mwanawe, wote wawili kwa siku moja. 29 Tena mtakapomchinjia BWANA dhabihu ya shukrani, mtamchinja ili mpate kukubaliwa. 30 Italiwa siku iyo hiyo; msisaze kitu chake hata asubuhi; mimi ndimi BWANA. 31 Kwa hiyo mtayashika maagizo yangu, na kuyafanya; mimi ndimi BWANA. 32 Wala msilinajisi jina langu takatifu; lakini nitatakaswa mimi katika wana wa Israeli; mimi ndimi BWANA niwatakasaye ninyi, 33 niliyewaleta mtoke nchi ya Misri, ili niwe Mungu wenu; mimi ndimi BWANA. |
Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Bible Society of Kenya