Biblia ya mtandaoni

Matangazo

Biblia nzima Agano la Kale Agano Jipya


Waamuzi 18 - Swahili Revised Union Version - SRUVDC Swahili Revised Union Version - SRUVDC
Waamuzi 18

Kuhama kwa Dani

1 Siku hizo hapakuwa na mfalme katika Israeli; tena katika siku hizo kabila la Wadani wakajitafutia urithi wapate mahali pa kukaa; maana hawakuwa wamepata urithi wao kati ya makabila ya Israeli.

2 Basi wana wa Dani wakatuma watu watano kutoka kwa koo zao zote, watu mashujaa, kutoka Sora, na kutoka Eshtaoli, ili kuipeleleza hiyo nchi, kuikagua; wakawaambia, Haya, endeni mkaikague nchi hii; basi wakaifikia nchi ya vilima vilima ya Efraimu, hadi nyumba ya huyo Mika, Wakalala huko.

3 Basi hapo walipokuwa karibu na nyumba ya Mika, wakatambua sauti yake huyo kijana Mlawi; ndipo wakageuka wakaenda kuko, na kumwuliza, Je! Ni nani aliyekuleta wewe huku? Unafanya nini mahali hapa? Una kazi gani hapa?

4 Naye akawaambia, Hivi na hivi ndivyo alivyonifanyia Mika, ameniajiri, nami nimekuwa kuhani wake.

5 Nao wakamwambia, Tafadhali tutakie shauri la Mungu, ili tupate kujua kama njia yetu tuiendeayo itafanikiwa.

6 Kuhani akawaambia, Haya endeni na amani; njia mnayoiendea iko mbele za BWANA.

7 Ndipo hao watu watano wakaenda zao, wakafika Laisha, wakawaona wale watu waliokuwamo ndani yake, jinsi walivyokaa kwa amani, kama ilivyokuwa desturi ya Wasidoni, watu watulivu na wasioshuku, wasiopungukiwa na chochote duniani, na waliokuwa na miliki; Nao walikuwa mbali na hao Wasidoni, wala hawakutangamana na watu wengine.

8 Kisha wakawarudia ndugu zao huko Sora na Eshtaoli; ndugu zao wakawauliza; Haya, mna habari gani?

9 Wakasema, Haya, inukeni, twende tukapigane nao; kwa maana tumeiona hiyo nchi nayo ni nchi nzuri sana; nanyi, je! Hamtafanya chochote? Msiwe wavivu kwenda, na kuingia, ili mpate kuimiliki nchi hiyo.

10 Hapo mtakapokwenda mtawafikia watu wakaao kwa amani, na hiyo nchi nayo ni kubwa; kwa kuwa Mungu ameitia mikononi mwenu; ni mahali ambapo hapapungukiwi na kitu chochote kilichoko duniani.

11 Basi wakatoka hapo watu mia sita waliovaa silaha za vita, wa jamaa ya Wadani, kutoka Sora, na kutoka Eshtaoli.

12 Wakakwea juu na kupiga kambi huko Kiriath-yearimu, katika Yuda; kwa sababu hiyo wakapaita mahali pale jina lake Mahane-dani hata hivi leo; tazama, ni hapo nyuma ya Kiriath-yearimu.

13 Nao wakapita huko hadi hiyo nchi ya vilima vilima ya Efraimu, wakafikia nyumba ya huyo Mika.

14 Ndipo hao watu watano waliokwenda kuipeleleza nchi ya Laisha wakawaambia ndugu zao, Je! Ninyi mwajua ya kwamba mna naivera ndani ya nyumba hizi, na kinyago na sanamu ya kuchonga, na sanamu ya kusubu? Basi sasa fikirini iwapasayo kufanya.

15 Basi wakageuka wakaenda kuko, wakafika katika nyumba ya huyo kijana Mlawi, huko nyumbani kwa Mika, kumwamkia.

16 Hao watu mia sita wenye kuvaa silaha zao za vita, waliokuwa ni wana wa Dani, wakasimama penye maingilio ya lango.

17 Na hao watu watano waliokwenda kuipeleleza hiyo nchi wakakwea juu, wakaingia ndani, na kuitwaa hiyo sanamu ya kuchonga, na hiyo naivera, na kile kinyago, na hiyo sanamu ya kusubu; na huyo kuhani akasimama penye maingilio ya lango pamoja na hao wanaume mia sita waliojihami.

18 Nao hapo walipoingia ndani ya nyumba ya Mika, na kuileta hiyo sanamu ya kuchonga, na hiyo naivera, na kile kinyago, na hiyo sanamu ya kusubu, huyo kuhani akawauliza, Je! Mwafanya nini ninyi?

19 Wao wakamwambia, Nyamaza wewe, weka mkono wako kinywani mwako, uende pamoja nasi, uwe kwetu baba, tena kuhani; je! Ni vema kwako kuwa kuhani kwa ajili ya nyumba ya mtu mmoja, au kuwa kuhani kwa ajili ya kabila na jamaa katika Israeli?

20 Huyo kuhani moyo wake ukafurahi, naye akaitwaa hiyo naivera, na kile kinyago, na hiyo sanamu ya kuchonga, akaenda katikati ya hao watu.

21 Basi wakageuka wakaenda zao, lakini watoto wadogo na wanyama wao wa kufugwa, na vyombo vyao, wakawatanguliza mbele yao.

22 Walipokuwa wamekwenda kitambo kizima kutoka nyumba ya Mika, wale watu waliokuwa katika nyumba zilizokuwa karibu na nyumba ya Mika walikutana, wakawaandama na kuwapata hao wana wa Dani.

23 Wakawapigia kelele wana wa Dani. Nao wakageuza nyuso zao na kumwambia Mika, Una nini wewe, hata ukaja na mkutano namna hii?

24 Akasema, Ninyi mmeichukua miungu niliyoifanya, na huyo kuhani, nanyi mmekwenda zenu, nami nina nini tena? Basi imekuwaje ninyi kuniuliza, Una nini wewe?

25 Hao wana wa Dani wakamwambia, Hiyo sauti yako isisikike kati yetu, wasije walio na hasira wakakupiga, nawe ukapotewa na uhai wako, pamoja na uhai wa watu wa nyumbani mwako.

26 Basi wana wa Dani wakaenda zao; naye Mika alipoona ya kuwa wanamzidi nguvu, akageuka akarudi nyumbani kwake.

Wadani wafanya makao katika Laisha

27 Nao wakakitwaa hicho alichokuwa amekifanya Mika, na kuhani aliyekuwa naye nao wakafika Laisha, kwa watu waliokuwa watulivu na wasioshuku, wakawapiga kwa makali ya upanga; wakauteketeza kwa moto mji wao.

28 Wala hakukuwa na mwokozi, kwa sababu huo mji ulikuwa mbali sana na Sidoni, nao hawakutangamana na watu wowote wale; na mji huo ulikuwa katika hilo bonde lililo karibu na Bethrehobu. Nao wakaujenga huo mji na kukaa humo.

29 Wakauita mji jina lake Dani, kwa kulifuata jina la baba yao Dani, aliyezaliwa na Israeli; lakini jina la mji huo hapo awali lilikuwa Laisha.

30 Kisha wana wa Dani wakajisimamishia hiyo sanamu ya kuchonga; na Yonathani mwana wa Gershomu, mwana wa Musa, yeye na wanawe walikuwa ni makuhani katika kabila la Wadani hadi siku nchi hiyo ilipochukuliwa mateka.

31 Basi wakaiabudu hiyo sanamu ya kuchonga aliyotengeneza Mika, wakati wote ile nyumba ya Mungu ilipokuwako huko Shilo.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.

Bible Society of Kenya