1 Kitabu cha habari za Tobiti, mwana wa Tobieli, mwana wa Ananieli, mwana wa Adueli, mwana wa Gabaeli, wa uzao wa Asieli, wa kabila ya Naftali. 2 Zamani za Shalmanesa, mfalme wa Waashuri, huyu alichukuliwa mateka kutoka Tisbe, ulioko upande wa kulia wa Kedesh-Naftali katika Galilaya, upande wa juu wa Asheri. TOBITI UHAMISHONI Maisha ya ujana wa Tobiti na ushindi wake3 Mimi, Tobiti, nimekwenda katika njia za kweli na haki siku zote za maisha yangu. Nikawakirimia ndugu zangu sadaka nyingi, pia na watu wa taifa langu waliokuja pamoja nami katika nchi ya Waashuri mpaka Ninawi. 4 Nami nilipokuwa nikikaa kwetu; katika nchi ya Israeli, nikiwa ningali kijana bado, kabila nzima ya Naftali, baba yangu, walijitenga na nyumba ya Yerusalemu; ambayo kwamba palichaguliwa katika kabila zote za Israeli, ili makusudi kabila zote watoe kafara huko; hata na hekalu la makao yake Aliye Juu likawekwa wakfu na kujengwa huko, kwa ajili ya vizazi vyote vya milele. 5 Basi kabila zote waliojitenga, pamoja na kabila ya Naftali, baba yangu, walimtolea kafara yule Baali, mtamba wa ng'ombe. 6 Bali mimi desturi yangu huenda peke yangu mara nyingi mpaka Yerusalemu wakati wa sikukuu, kama walivyoamriwa Waisraeli wote kuwa agizo la milele. Huchukua malimbuko, na zaka za mazao yangu, na manyoya ya kwanza ya kondoo, 7 nikawapa makuhani, wana wa Haruni, huko madhabahuni. Zaka ya mazao yangu yote niliwapa wana wa Lawi, waliohudumu huko Yerusalemu; 8 na zaka ya pili niliuza, nikaenda na kuitumia Yerusalemu kila mwaka; na ya tatu niliwapa watu waliohusika nayo; kama alivyoniagiza Debora, mama wa baba yangu. Yaani, niliachwa yatima na baba yangu. 9 Hata nilipopata kuwa mtu mzima nilimwoa Ana, aliyekuwa wa jamaa yetu; naye akanizalia Tobia. Uhamishoni Ninawi10 Nasi tulipochukuliwa mateka mpaka Ninawi, ndugu zangu wote nao wale waliokuwa wa jamaa yangu walikuwa wakila chakula cha mataifa. 11 Bali mimi nilijizuia nisile, 12 kwa sababu nilimkumbuka Mungu kwa moyo wangu wote, 13 Naye Aliye Juu akanijalia kuwa na neema na kibali machoni pa Shalmanesa, hata nikawa mnunuachakula wake. 14 Hivyo nikaenda mpaka Umedi, nikaweka amana kwake Gabaeli mwana wa Gabria talanta kumi za fedha, huko Rage, mji wa Umedi. 15 Hata ikawa, Shalmanesa alipokufa, mtoto wake Senakeribu alitawala mahali pake; ambaye wakati wake barabara zilichafuka, hata nisiweze kwenda tena mpaka Umedi. Tobiti azika waliokufa16 Zamani za Shalamanesa nilitoa sadaka nyingi, nikawakirimia ndugu zangu; 17 nikawapa wenye njaa chakula; nikawapa walio uchi nguo zangu; hata nikimwona mtu yeyote wa taifa letu amekufa na kutupwa kwenye kuta za Ninawi, nikamzika. 18 Vile vile iwapo Mfalme Senakeribu ameua watu, pale alipokuja amekimbia kutoka Yudea, niliwazika kwa siri; maana katika ghadhabu yake aliwaua wengi; lakini maiti zao hazikuonekana zilipotafutwa kwa amri ya mfalme. 19 Lakini mmojawapo wa Waninawi akaenda akanishtaki kwa mfalme, ya kwamba mimi nimewazika na kujificha; basi nilipotambua ya kuwa nilitafutwa ili niuawe nilijitenga kwa hofu. 20 Ndipo mali zangu zote zilipotwaliwa, wala sikubakizwa na kitu ila mke wangu Ana, na mwanangu Tobia. 21 Kumbe! Hazijapita siku hamsini na tano hata wanawe wawili walimwua baba yao, wakakimbilia kwenye milima ya Ararati. Naye Esar-hadoni mwanawe akatawala mahali pake; akaweka Akiakaro, mwana wa ndugu yangu Anaeli, juu ya takwimu zote za ufalme wake, na juu ya mambo yake yote. 22 Hivyo Akiakaro akaniombea, nikarudi tena mpaka Ninawi. Mradi huyu Akiakaro alikuwa mnyweshaji, na mlindamhuri, na wakili, na msimamizi wa hesabu; naye Esar-hadoni akamweka kuwa wa pili wake. Naye alikuwa mwana wa ndugu yangu. |
Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Bible Society of Kenya