Biblia ya mtandaoni

Matangazo

Biblia nzima Agano la Kale Agano Jipya


Mathayo 9 - Swahili Revised Union Version - SRUVDC Swahili Revised Union Version - SRUVDC
Mathayo 9

1 Akapanda katika mashua, akavuka, akafika mjini kwao.

Yesu amponya mtu aliyepooza

2 Na tazama, wakamletea mtu mwenye kupooza, akiwa amelala kitandani; naye Yesu, alipoiona imani yao, alimwambia yule mwenye kupooza, Jipe moyo mkuu, mwanangu, umesamehewa dhambi zako.

3 Na tazama, baadhi ya waandishi wakasema nafsini mwao, Huyu anakufuru.

4 Naye Yesu, hali akijua mawazo yao, akasema, Mbona mnawaza maovu mioyoni mwenu?

5 Kwa maana rahisi ni lipi, ni kusema, Umesamehewa dhambi zako, au ni kusema, Ondoka, uende?

6 Lakini mpate kujua ya kwamba Mwana wa Adamu anayo amri duniani ya kusamehe dhambi, (amwambia yule mwenye kupooza) Inuka, ujitwike kitanda chako, uende nyumbani kwako.

7 Akaondoka, akaenda zake nyumbani kwake.

8 Makutano walipomwona, walishikwa na hofu, wakamtukuza Mungu, aliyewapa watu amri ya namna hii.

Kuitwa kwa Mathayo

9 Naye Yesu alipokuwa akipita kutoka huko aliona mtu ameketi forodhani, aitwaye Mathayo, akamwambia, Nifuate. Akaondoka, akamfuata.

10 Ikawa alipoketi nyumbani ale chakula, tazama, watoza ushuru wengi na wenye dhambi walikuja wakaketi pamoja na Yesu na wanafunzi wake.

11 Mafarisayo walipoona, waliwaambia wanafunzi wake, Mbona mwalimu wenu anakula pamoja na watoza ushuru na wenye dhambi?

12 Naye aliposikia, aliwaambia, Wenye afya hawahitaji tabibu, bali walio wagonjwa.

13 Lakini nendeni, mkajifunze maana yake maneno haya, Nataka rehema, wala si sadaka; kwa maana sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi.

Swali kuhusu kufunga

14 Wakati ule wanafunzi wake Yohana wakamwendea, wakasema, Kwa nini sisi na Mafarisayo tunafunga, bali wanafunzi wako hawafungi?

15 Yesu akawaambia, Walioalikwa arusini wawezaje kuomboleza, muda bwana arusi akiwapo pamoja nao? Lakini siku zitakuja watakapoondolewa bwana arusi; ndipo watakapofunga.

16 Hakuna mtu atiaye kiraka cha nguo mpya katika vazi kuukuu; maana kile kilichotiwa huondoa kipande cha lile vazi, na pale palipotatuka huzidi.

17 Wala watu hawatii divai mpya katika viriba vikuukuu; na kama wakitia, vile viriba hupasuka, divai ikamwagika, na viriba vikaharibika; bali hutia divai mpya katika viriba vipya, vikahifadhika vyote.

Msichana arejeshewa uhai na mwanamke kuponywa

18 Alipokuwa akiwaambia hayo, tazama, akaja kiongozi mmoja, akamsujudia, akisema, Binti yangu sasa hivi amekufa; lakini njoo, uweke mkono wako juu yake, naye ataishi.

19 Yesu Akaondoka, akamfuata, pamoja na wanafunzi wake.

20 Na tazama, mwanamke aliyekuwa na ugonjwa wa kutoka damu muda wa miaka kumi na miwili, alikuja kwa nyuma, akaugusa upindo wa vazi lake.

21 Kwa maana alisema moyoni mwake, Nikigusa tu upindo wa vazi lake nitapona.

22 Yesu akageuka, akamwona, akamwambia, Jipe moyo mkuu, binti yangu; imani yako imekuponya. Yule mwanamke akapona tangu saa ile.

23 Yesu alipofika nyumbani kwa yule kiongozi, aliona wapiga filimbi, na makutano wakifanya maombolezo,

24 akawaambia, Ondokeni; kwa maana msichana hakufa, amelala tu. Wakamcheka sana.

25 Lakini makutano walipoondoshwa, aliingia, akamshika mkono; yule msichana akasimama.

26 Habari hizi zikaenea katika nchi ile yote.

Yesu awaponya vipofu wawili

27 Yesu alipokuwa akipita kutoka huko, vipofu wawili wakamfuata wakipaza sauti, wakisema, Uturehemu, Mwana wa Daudi.

28 Naye alipofika nyumbani, wale vipofu walimwendea; Yesu akawaambia, Mnaamini kwamba naweza kufanya hili? Wakamwambia, Naam, Bwana.

29 Ndipo alipowagusa macho, akasema, Kwa kadiri ya imani yenu na itendeke kwenu.

30 Macho yao yakafumbuka. Naye Yesu akawaagiza kwa nguvu, akisema, Angalieni hata mtu mmoja asijue.

31 Lakini wakatoka, wakaeneza habari zake katika nchi ile yote.

Yesu amponya bubu

32 Na hao walipokuwa wakiondoka, tazama, walimletea mtu bubu mwenye pepo.

33 Na pepo alipotolewa, yule bubu alinena, makutano wakastaajabu, wakasema, Haijaonekana hivi katika Israeli wakati wowote.

34 Lakini Mafarisayo wakasema, Kwa nguvu za mkuu wa pepo atoa pepo.

Mavuno ni mengi, wafanya kazi ni wachache

35 Naye Yesu alikuwa akizunguka katika miji yote na vijiji, akifundisha katika masinagogi yao, na kuihubiri Habari Njema ya ufalme, na kuponya magonjwa yote na udhaifu wa kila aina.

36 Na alipowaona makutano, aliwahurumia, kwa sababu walikuwa wamechoka na kutawanyika kama kondoo wasio na mchungaji.

37 Ndipo alipowaambia wanafunzi wake, Mavuno ni mengi, lakini wafanya kazi ni wachache.

38 Basi mwombeni Bwana wa mavuno, atume wafanya kazi katika mavuno yake.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.

Bible Society of Kenya