Biblia ya mtandaoni

Matangazo

Biblia nzima Agano la Kale Agano Jipya


Kutoka 4 - Swahili Revised Union Version - SRUVDC Swahili Revised Union Version - SRUVDC
Kutoka 4

Musa afanya miujiza

1 Musa akajibu akasema, Lakini, tazama, hawataniamini, wala hawataisikia sauti yangu; maana watasema, BWANA hakukutokea.

2 BWANA akamwambia, Ni nini hiyo uliyo nayo mkononi mwako? Akasema, Ni fimbo.

3 Akamwambia, Itupe chini; akaitupa chini, nayo ikawa nyoka; Musa akakimbia kutoka mbele yake.

4 BWANA akamwambia Musa, Nyosha mkono wako, kamshike mkia; (akaunyosha mkono wake akamshika, naye akageuka kuwa fimbo mkononi mwake;)

5 ili kwamba wapate kusadiki ya kwamba BWANA, Mungu wa Abrahamu, Mungu wa Isaka, Mungu wa Yakobo, amekutokea.

6 BWANA akamwambia tena, Sasa tia mkono wako kifuani mwako. Akautia mkono wake kifuani mwake; naye alipoutoa, kumbe! Mkono wake ulikuwa una ukoma, umekuwa mweupe kama theluji.

7 Akasema, Tia mkono wako kifuani mwako tena. Akautia mkono wake kifuani mwake tena, na alipoutoa kifuani mwake, kumbe! Umerudia hali ya mwili wake.

8 Basi itakuwa, wasipokusadiki, wala kuisikiliza sauti ya ishara ya kwanza, wataisikiliza sauti ya ishara ya pili.

9 Kisha itakuwa wasipoamini hata ishara hizo mbili, wala kuisikiliza sauti yako, basi, yatwae maji ya mtoni uyamwage juu ya nchi kavu, na yale maji uyatwaayo mtoni yatakuwa damu juu ya nchi kavu.

10 Musa akamwambia BWANA Ee Bwana, mimi si msemaji, tokea zamani, wala tokea hapo uliposema na mtumishi wako; maana mimi si mwepesi wa kusema, na ulimi wangu ni mzito.

11 BWANA akamwambia, Ni nani aliyekifanya kinywa cha mwanadamu? Au ni nani afanyaye mtu kuwa bubu au kiziwi, au mwenye kuona, au kuwa kipofu? Si mimi, BWANA?

12 Basi sasa, nenda, nami nitakuwa pamoja na kinywa chako, na kukufundisha utakalolinena.

13 Akasema, Ee Bwana, nakuomba, tuma kwa mkono wake huyo utakayemtuma.

14 Hasira ya BWANA ikawaka juu ya Musa, akasema, Je! Hayuko Haruni, ndugu yako, Mlawi? Najua ya kuwa yeye aweza kusema vizuri. Pamoja na hayo, tazama, anakuja kukulaki; naye atakapokuona, atafurahi moyoni mwake.

15 Nawe utasema naye, na kuyatia maneno kinywani mwake; nami nitakuwa pamoja na kinywa chako, na pamoja na kinywa chake, na kuwafundisheni mtakayofanya.

16 Naye atakuwa msemaji wako kwa watu, hata yeye atakuwa mfano wa kinywa kwako, nawe utakuwa mfano wa Mungu kwake.

17 Nawe utatwaa fimbo hii mkononi mwako, na kwa hiyo utazifanya zile ishara.

Musa arudi Misri

18 Basi Musa akaenda na kurejea kwa Yethro mkwewe, na kumwambia, Nipe ruhusa niende, nakusihi, niwarudie hao ndugu zangu walioko Misri, nipate kuwaona kwamba wako hai hata sasa. Yethro akamwambia Musa, Haya, nenda kwa amani.

19 BWANA akamwambia Musa huko Midiani, Haya, nenda, rudi Misri; kwa kuwa wale watu wote walioutaka uhai wako wamekwisha kufa.

20 Basi Musa akamchukua mkewe na wanawe, na kuwapandisha juu ya punda, naye akarudi mpaka nchi ya Misri; na Musa akaichukua ile fimbo ya Mungu mkononi mwake.

21 BWANA akamwambia Musa, Hapo utakaporudi Misri, angalia ukazifanye mbele ya Farao zile ajabu zote nilizozitia mkononi mwako; lakini nitaufanya mgumu moyo wake, naye hatawapa ruhusa hao watu waende zao.

22 Nawe umwambie Farao, BWANA asema hivi, Israeli ni mwanangu mimi, mzaliwa wa kwanza wangu;

23 nami nimekuambia, Mpe mwanangu ruhusa aende, ili apate kunitumikia, nawe umekataa kumpa ruhusa aende; angalia basi, mimi nitamwua mwanao, mzaliwa wa kwanza wako.

24 Ndipo walipokuwa njiani mahali pa kulala, BWANA akakutana naye, akataka kumwua.

25 Ndipo Sipora akashika jiwe gumu lenye makali na kulikata govi ya zunga la mwanawe, na kulibwaga miguuni pa Musa akasema. Hakika wewe ni bwana arusi wa damu kwangu.

26 Basi akamwacha. Ndipo huyo mkewe akanena, U bwana arusi wa damu wewe, kwa ajili ya kutahiri.

27 BWANA akamwambia Haruni, Nenda jangwani uonane na Musa. Naye akaenda, akamkuta katika mlima wa Mungu, akambusu.

28 Musa akamwambia Haruni hayo maneno yote ya BWANA ambayo alimtuma aende nayo, na ishara hizo zote alizomwagiza.

29 Musa na Haruni wakaenda, wakawakusanya wazee wote wa watu wa Israeli.

30 Haruni akawaambia maneno yote BWANA aliyonena na Musa akazifanya zile ishara mbele ya watu.

31 Watu wakaamini, na waliposikia ya kuwa BWANA amewajia wana wa Israeli, na ya kuwa ameyaona mateso yao, wakainamisha vichwa vyao wakasujudu.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.

Bible Society of Kenya