Kuzaliwa na ujana wa Musa1 Mtu mmoja wa nyumba ya Lawi akaenda akaoa binti mmoja wa Lawi. 2 Yule mwanamke akachukua mimba akazaa mwana, na alipoona ya kuwa ni mtoto mzuri akamficha miezi mitatu. 3 Na alipokuwa hawezi kumficha tena, akamtengenezea kikapu cha mafunjo akakitaliza kwa sifa na lami, akamtia mtoto ndani yake, akakiweka kwenye nyasi kando ya mto. 4 Dada yake mtoto akasimama mbali ili ajue yatakayompata. 5 Basi binti Farao akashuka, aoge mtoni, na vijakazi wake wakatembea kando ya mto; naye akakiona kile kikapu katika nyasi, akamtuma kijakazi wake kwenda kukileta. 6 Akakifungua, akamwona mtoto, na tazama, mtoto yule analia. Basi akamhurumia, akasema, Huyu ni mmojawapo wa watoto wa Waebrania. 7 Basi dada yake mtoto akamwambia binti Farao, Je! Niende nikamwite mlezi katika wanawake wa Kiebrania, aje kwako, akunyonyeshee mtoto huyu? 8 Binti Farao akamwambia, Haya! Nenda. Yule kijana akaenda akamwita mama yake yule mtoto. 9 Binti Farao akamwambia, Mchukue mtoto huyu, ukaninyonyeshee, nami nitakupa mshahara wako. Yule mwanamke akamtwaa mtoto, akamnyonyesha. 10 Mtoto akakua, naye akamleta kwa binti Farao, akawa mwanawe. Akamwita jina lake Musa. Musa akimbilia Midiani11 Hata siku zile, Musa alipokuwa mtu mzima, akatoka kuwaendea ndugu zake, akatazama mizigo yao. Akamwona Mmisri anampiga Mwebrania, mmojawapo wa ndugu zake. 12 Basi akatazama huku na huko, na alipoona ya kuwa hapakuwapo mtu, akampiga na kumwua Mmisri yule, akamfukia mchangani. 13 Akatoka siku ya pili, na tazama, watu wawili wa Waebrania walikuwa wakipigana. Akamwambia yule aliyemdhulumu mwenzake, Mbona unampiga mwenzako? 14 Yule akasema, Ni nani aliyekuweka wewe kuwa mkuu wetu, na mwamuzi juu yetu? Je! Wataka kuniua kama ulivyomwua yule Mmisri? Musa akaogopa, akasema, Kumbe! Jambo lile limejulikana. 15 Basi Farao alipopata habari, akataka kumwua Musa; lakini Musa akakimbia kutoka kwa Farao, akakaa katika nchi ya Midiani; akaketi karibu na kisima. 16 Basi kuhani wa Midiani alikuwa na binti saba, nao wakaja wakateka maji, wakazijaza birika maji, wapate kunywesha kundi la baba yao. 17 Wachungaji wakaja wakawafukuza; lakini Musa akasimama, akawasaidia, akalinywesha kundi lao. 18 Walipofika kwa Reueli baba yao, akasema, Imekuwaje hata mkarejea mapema leo? 19 Wakasema, Mmisri mmoja alituokoa katika mikono ya wachungaji, tena zaidi ya hayo, akatutekea maji, akalinywesha kundi. 20 Akawaambia binti zake, Yuko wapi basi? Mbona mmemwacha mtu huyo? Mwiteni, ale chakula. 21 Musa akawa radhi kukaa kwake mtu yule, naye akampa Musa binti yake, Sipora. 22 Huyo akamzalia mtoto wa kiume, akamwita jina lake Gershomu, maana alisema, Nimekuwa mgeni katika nchi ya ugeni. 23 Na kisha baada ya muda, yule mfalme wa Misri akafa; wana wa Israeli wakaugua kwa sababu ya ule utumwa, wakalia; kilio chao kikafika juu kwa Mungu kwa sababu ya ule utumwa. 24 Mungu akasikia kuugua kwao, Mungu akakumbuka agano lake alilolifanya na Abrahamu na Isaka na Yakobo. 25 Mungu akawaona wana wa Israeli, na Mungu akawaangalia. |
Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Bible Society of Kenya