Biblia ya mtandaoni

Matangazo

Biblia nzima Agano la Kale Agano Jipya


Kutoka 17 - Swahili Revised Union Version - SRUVDC Swahili Revised Union Version - SRUVDC
Kutoka 17

Maji toka mwambani

1 Mkutano wote wa wana wa Israeli ukasafiri, kutoka bara ya Sini kwa safari zao, kama BWANA alivyowaagiza, wakatua Refidimu; napo hapakuwa na maji, watu wanywe.

2 Kwa hiyo hao watu wakamgombeza Musa, wakasema, Tupe maji tunywe. Musa akawaambia, Kwa nini mnanigombeza? Mbona mnamjaribu BWANA?

3 Watu wakawa na kiu huko; nao wakamnung'unikia Musa, wakasema, Mbona umetupandisha kutoka Misri, kutuua sisi na watoto wetu na wanyama wetu kwa kiu?

4 Musa akamlilia BWANA, akisema, Niwatendee nini watu hawa? Bado kidogo nao watanipiga kwa mawe.

5 BWANA akamwambia Musa, Pita mbele ya watu, ukawachukue baadhi ya wazee wa Israeli pamoja nawe; na ile fimbo yako ambayo uliupiga mto kwayo, uitwae mkononi mwako, ukaende.

6 Tazama, nitasimama mbele yako huko, juu ya lile jabali katika Horebu; nawe utalipiga jabali, na maji yatatoka, watu wapate kunywa. Musa akafanya hivyo mbele ya wazee wa Israeli.

7 Akapaita mahali pale jina lake Masa, na Meriba kwa sababu ya ugomvi wa wana wa Israeli, na kwa sababu walimjaribu BWANA, wakisema, Je! BWANA yu kati yetu au sivyo?

Waamaleki Washindwa na Waisraeli

8 Wakati huo Waamaleki wakatokea, wakapigana na Israeli huko Refidimu.

9 Musa akamwambia Yoshua, Tuchagulie watu, uende ukapigane na Waamaleki; kesho nitasimama juu ya kilele kile, na ile fimbo ya Mungu nitakuwa nayo mkononi mwangu.

10 Basi Yoshua akafanya kama Musa alivyomwambia, akapigana na Amaleki; na Musa na Haruni na Huri wakapanda juu ya kile kilima.

11 Ikawa, Musa alipouinua mkono wake, Israeli walishinda; na alipoushusha mkono wake, Amaleki walishinda.

12 Lakini mikono ya Musa ililegea; basi wakatwaa jiwe, wakaliweka chini yake akalikalia. Haruni na Huri wakaitengemaza mikono yake, mmoja upande huu na mmoja upande huu; mikono yake ikathibitika hata jua lilipokuchwa.

13 Yoshua akawaangamiza Amaleki na watu wake kwa ukali wa upanga.

14 BWANA akamwambia Musa, Andika habari hii katika kitabu iwe ukumbusho, kisha ihubiri masikioni mwa Yoshua; ya kuwa nitaufuta ukumbusho wa Amaleki kabisa, usiwe tena chini ya mbingu.

15 Musa akajenga madhabahu, akaiita jina lake Yahweh-nisi;

16 akasema, BWANA ameapa; BWANA atakuwa na vita na Amaleki kizazi baada ya kizazi.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.

Bible Society of Kenya