Agano kuwafikia watiifu wote1 BWANA asema hivi, Shikeni hukumu, mkatende haki; kwa maana wokovu wangu uko karibu kuja, na haki yangu kufunuliwa. 2 Heri afanyaye haya, na mwanadamu ayashikaye sana; azishikaye sabato asizivunje, auzuiaye mkono wake usifanye uovu wowote. 3 Wala mgeni, aambatanaye na BWANA, asiseme hivi, Hakika yake BWANA atanitenga na watu wake; wala towashi asiseme, Mimi ni mti mkavu. 4 Kwa maana BWANA awaambia hivi matowashi, wanaozishika sabato zangu, na kuyachagua mambo yanipendezayo, na kulishika sana agano langu; 5 Nitawapa hawa nyumbani mwangu, na ndani ya kuta zangu, kumbukumbu na jina, lililo jema kuliko kuwa na watoto wa kiume na wa kike; nitawapa jina lidumulo milele, lisilokatiliwa mbali. 6 Na wageni, walioandamana na BWANA ili wamhudumu, na kulipenda jina la BWANA, kuwa watumishi wake; kila aishikaye sabato asiivunje, na kulishika sana agano langu; 7 Nitawaleta hao nao hadi katika mlima wangu mtakatifu, na kuwafurahisha katika nyumba yangu ya sala; makafara yao na dhabihu zao zitakubaliwa juu ya madhabahu zangu; kwa maana nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala kwa mataifa yote. 8 Bwana MUNGU, akusanyaye waliofukuzwa katika Israeli asema, Pamoja na hayo nitamkusanyia na wengine, zaidi ya hao walio wake waliokusanywa. Ufisadi wa watawala wa Israeli9 Enyi wanyama wote wa porini njoni Mle, enyi wanyama wote wa porini. 10 Walinzi wake ni vipofu, wote pia hawana maarifa; wote ni mbwa walio bubu, hawawezi kulia; huota ndoto, hulala, hupenda usingizi. 11 Naam, mbwa hao wana uchu sana, hawashibi kamwe; na hao ni wachungaji wasioweza kufahamu neno; wote pia wamegeuka upande, wazifuate njia zao wenyewe, kila mmoja kwa faida yake, toka pande zote. 12 Husema, Njooni, nitaleta divai, Na tunywe sana kileo; Na kesho itakuwa kama leo, Sikukuu kupita kiasi. |
Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Bible Society of Kenya