Biblia ya mtandaoni

Matangazo

Biblia nzima Agano la Kale Agano Jipya


Isaya 35 - Swahili Revised Union Version - SRUVDC Swahili Revised Union Version - SRUVDC
Isaya 35

Kurudi Sayuni kwa waliokombolewa

1 Nyika na mahali palipo ukiwa patafurahi; jangwa litashangilia na kuchanua maua kama waridi.

2 Litachanua maua mengi, na kufurahi, naam, kwa shangwe na kuimba; litapewa uzuri wa Lebanoni, utukufu wa Karmeli na Sharoni; watauona utukufu wa BWANA, ukuu wa Mungu wetu.

3 Itieni nguvu mikono iliyo dhaifu, yaimarisheni magoti yaliyolegea.

4 Waambieni walio na moyo wa hofu, Jipeni moyo, msiogope; tazama, Mungu wenu atakuja na kisasi, na malipo ya Mungu; atakuja na kuwaokoa ninyi.

5 Ndipo macho ya vipofu yatafumbuliwa, na masikio ya viziwi yatazibuliwa.

6 Ndipo mtu aliye kilema atarukaruka kama kulungu, na ulimi wake aliye bubu utaimba; maana katika nyika maji yatabubujika; na vijito jangwani.

7 Na mchanga ung'aao mfano wa maji utakuwa ziwa la maji, na nchi yenye kiu itakuwa chemchemi za maji; katika makao ya mbweha, walipokuwa wamelala, patakuwa na majani, pamoja na mianzi na manyasi.

8 Na hapo patakuwa na njia kuu, na njia, nayo itaitwa, Njia ya utakatifu; wasio safi hawatapita juu yake; bali itakuwa kwa ajili ya watu hao; wasafirio, wajapokuwa wajinga, hawatapotea katika njia hiyo.

9 Hapo hapatakuwa na simba, wala mnyama mkali hatapanda juu yake; hawataonekana hapo; bali waliokombolewa watakwenda katika njia hiyo.

10 Na hao waliokombolewa na BWANA watarudi, watafika Sayuni wakiimba; na furaha ya milele itakuwa juu ya vichwa vyao; nao watapata kicheko na furaha, huzuni na kuugua zitatoweka.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.

Bible Society of Kenya