Kuuawa kwa wanaoabudu sanamu1 Kisha akalia kwa sauti kuu masikioni mwangu, akisema, Waamuru wale wanaousimamia mji wakaribie, kila mmoja na awe na silaha ya kuangamiza mkononi mwake. 2 Na tazama, watu sita wakaja, wakitokea kwa njia ya lango la juu, lielekealo upande wa kaskazini, kila mmoja akiwa na silaha yake ya kuua mkononi; na mtu mmoja kati yao akiwa amevaa bafta, naye ana kidau cha wino cha mwandishi kiunoni. Wakaingia, wakasimama karibu na madhabahu ya shaba. 3 Na huo utukufu wa Bwana wa Israeli ulikuwa umepanda juu kutoka kwa kerubi, ambaye ulikuwa juu yake, mpaka kizingiti cha nyumba; akamwita mtu yule aliyekuwa amevaa bafta, mwenye kidau cha wino cha mwandishi kiunoni. 4 BWANA akamwambia, Pita kati ya mji, kati ya Yerusalemu, ukatie alama katika vipaji vya nyuso vya watu wanaopiga kite na kulia kwa sababu ya machukizo yote yanayofanyika kati yake. 5 Na hao wengine aliwaambia, nami nilisikia, Piteni kati ya mji nyuma yake, mkapige; jicho lenu lisiachilie, wala msione huruma; 6 Waueni kabisa, wazee, na viijana, na wasichana, na watoto wachanga, na wanawake; lakini msimkaribie mtu yeyote mwenye hiyo alama; tena anzeni katika patakatifu pangu. Basi, wakaanza kwa wazee waliokuwa mbele ya nyumba. 7 Akawaambia, itieni nyumba unajisi, mkazijaze nyua mizoga ya hao waliouawa; haya, nendeni. Wakaenenda, wakaua watu katika mji. 8 Tena ikawa, walipokuwa wakiwaua, nami nikaachwa, nilianguka kifudifudi, nikalia, nikasema, Ee Bwana MUNGU! Utaangamiza mabaki yote ya Israeli, wakati wa kumwaga ghadhabu yako juu ya Yerusalemu? 9 Ndipo akaniambia, Uovu wa nyumba ya Israeli na Yuda ni mwingi sana, nayo nchi imejaa damu, nao mji umejaa kupotosha hukumu; maana husema, BWANA ameiacha nchi hii, naye BWANA haoni. 10 Nami, jicho langu halitaachilia, wala sitakuwa na huruma; lakini nitaleta njia yao juu ya vichwa vyao. 11 Na tazama, mtu yule aliyevaa bafta, mwenye kidau cha wino kiunoni, akaleta habari, akisema, Nimefanya kama ulivyoniamuru. |
Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Bible Society of Kenya