Biblia ya mtandaoni

Matangazo

Biblia nzima Agano la Kale Agano Jipya


2 Wakorintho 6 - Swahili Revised Union Version - SRUVDC Swahili Revised Union Version - SRUVDC
2 Wakorintho 6

1 Nasi tukitenda kazi pamoja naye twawasihi msiipokee neema ya Mungu bure.

2 (Kwa maana asema, Kwa wakati uliokubalika nilikusikia, Na katika siku ya wokovu nilikusaidia; tazama, wakati uliokubalika ndio sasa; tazama, siku ya wokovu ndiyo sasa.)

3 Tusiwe kwazo la namna yoyote katika jambo lolote, ili utumishi wetu usilaumiwe;

4 bali katika kila neno tujipatie sifa njema, kama watumishi wa Mungu; katika subira nyingi, katika mateso, katika shida, katika matatizo;

5 katika mapigo, katika vifungo, katika fitina, katika taabu, katika kukesha, katika kufunga;

6 katika kuwa safi, katika elimu, katika uvumilivu, katika utu wema, katika Roho Mtakatifu, katika upendo usio unafiki;

7 katika neno la kweli, katika nguvu ya Mungu; kwa silaha za haki za mkono wa kulia na za mkono wa kushoto;

8 kwa utukufu na aibu; kwa kunenwa vibaya na kunenwa vema; kama wadanganyao, bali tu watu wa kweli;

9 kama wasiojulikana, bali wajulikanao sana; kama wanaokufa, kumbe tu hai; kama wanaorudiwa, bali wasiouawa;

10 kama wenye huzuni, bali siku zote tu wenye furaha; kama maskini, bali tukitajirisha wengi; kama wasio na kitu, bali tu wenye vitu vyote.

11 Vinywa vyetu vimefumbuliwa kwenu, enyi Wakorintho; mioyo yetu imekunjuliwa.

12 Hamsongwi ndani yetu, bali mwasongwa katika mioyo yenu.

13 Basi, ili mlipe kadiri ile mliyopewa (nasema nanyi kama na watoto), nanyi pia mkunjuliwe mioyo.

Hekalu la Mungu aliye hai

14 Msifungiwe nira pamoja na wasioamini, kwa jinsi isivyo sawasawa; kwa maana pana urafiki gani kati ya haki na uasi? Tena pana shirika gani kati ya nuru na giza?

15 Tena pana ulinganifu gani kati ya Kristo na Beliari? Au yeye aaminiye ana sehemu gani pamoja na yeye asiyeamini?

16 Tena pana mapatano gani kati ya hekalu la Mungu na sanamu? Kwa maana sisi tu hekalu la Mungu aliye hai; kama Mungu alivyosema, ya kwamba, Nitakaa ndani yao, na kati yao nitatembea, nami nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu.

17 Kwa hiyo, Tokeni kati yao, Mkatengwe nao, asema Bwana, Msiguse kitu kilicho kichafu, Nami nitawakaribisha.

18 Nitakuwa Baba kwenu, Nanyi mtakuwa kwangu wanangu wa kiume na wa kike, asema Bwana Mwenyezi.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.

Bible Society of Kenya