Yoshua 15 - BIBLIA Maandiko Matakatifu Kwa Watu Wote 2002Eneo watu wa Yuda walilopewa 1 Eneo la inchi watu wa kabila la Yuda walilopewa kwa kura kulingana na jamaa zake lilienea tangu kusini mashariki mpaka kwa mupaka wa Edomu. Sehemu ya kusini kabisa ilikuwa jangwa la Sini. 2 Mupaka wao upande wa kusini ulianzia kwenye pembe ya kusini ya bahari ya Chumvi, 3 ukaendelea kwa kusini mpaka kwenye mwinuko wa Akarabimu, ukapitia pembeni ya Sini, na kusini ya Kadesi-Barnea, ukipitia Hesironi hata Adari na kisha ukageuka kuelekea Karaka. 4 Kutoka hapo ulipita karibu na Asimoni na kufuata kijito cha Misri mpaka kufikia kwenye bahari ya Mediteranea. Hapo ndipo mupaka wa kusini wa Yuda ulipopita. 5 Mupaka wao wa upande wa mashariki ni bahari ya Chumvi mpaka pale muto Yordani unapoingilia katika bahari. Na mupaka wao upande wa kaskazini ulipita kutokea pembe ya bahari ya Chumvi pahali ambapo muto Yordani unaingilia katika bahari. 6 Mupaka huo ukapita Beti-Hogla na kaskazini ya Beti-Araba mpaka kwenye jiwe la Bohani mwana wa Rubeni. 7 Kutoka hapo, uliendelea mpaka Debiri kwenye bonde la Akori na kaskazini kuelekea Gilgali, karibu na mwinuko wa Adumimu ambao uko upande wa kusini wa kijito, kisha ukaelekea kwenye chemichemi za Eni-Semesi na kuishia Eni-Rogeli. 8 Kisha, mupaka huo ulipitia kwenye Bonde la Hinomu, upande wa kusini wa kilima cha Wayebusi, ni kusema Yerusalema, kuelekea kilele cha mulima unaokuwa upande wa magaribi wa bonde la Hinomu na kufika mwisho wa bonde la Refaimu. 9 Kutoka hapo, ulielekea kwenye mulima mpaka chemichemi za Nefutoa, mpaka kwenye miji ya mulima wa Efuroni. Hapo mupaka uligeuka na kuelekea Bala, ni kusema Kiriati-Yearimu, 10 ambako ulipinda upande wa magaribi kuelekea Seiri; ukapita kaskazini ya mulima wa Yerimu, ni kusema Kesaloni, na kuteremuka mpaka Beti-Semesi ambapo ulipita karibu na Timuna. 11 Kisha ukaendelea upande wa kaskazini wa Ekuroni, ukazunguka kuelekea Sikeroni ambapo ulipita karibu na mulima Bala mpaka Yabuneli ukaishia katika bahari ya Mediteranea. 12 Mupaka wa upande wa magaribi ulikuwa bahari ya Mediteranea. Ndivyo ilivyokuwa mipaka ya eneo walilopewa watu wa kabila la Yuda kulingana na ukoo zao. Watu wa Kalebu wananyanganya eneo la Hebroni 13 Kalebu mwana wa Yefune, alipewa sehemu ya inchi ya Yuda kama vile Yawe alivyomwamuru Yoshua. Alipewa Kiriati-Arba au muji wa Arba ambaye alikuwa babu wa Anaki. Muji huo sasa unaitwa Hebroni. 14 Kalebu alizifukuza kutoka muji huo ukoo tatu za Anaki, ni kusema ukoo wa Sesayi, ukoo wa Ahimani na ukoo wa Talmayi. 15 Kutoka Hebroni alikwenda kuwashambulia wakaaji wa Debiri, muji ambao zamani uliitwa Kiriati-Seferi. 16 Kalebu akatangaza kwamba atamwoesha binti yake Akisa kwa mwanaume yeyote atakayeuteka muji wa Kiriati-Seferi. 17 Basi, Otinieli mwana wa Kenazi, ndugu ya Kalebu, akauteka muji huo, naye Kalebu akamupa binti yake. 18 Katika siku yao ya arusi, Akisa akamwambia Otinieli amwombe Kalebu shamba. Akisa alikuwa amepanda juu ya punda, na alipokuwa anashuka chini, Kalebu akamwuliza: “Unataka nikupe nini?” 19 Akisa akamujibu: “Unipe zawadi. Unipe sehemu yenye maji kwa sababu kule Negebu ulikonipa ni jangwa.” Basi, Kalebu akamupa chemichemi za maji zilizokuwa upande wa juu na chini. 20-62 Hii ndiyo inchi watu wa kabila la Yuda waliyopewa kulingana na ukoo zake. Miji iliyokuwa upande wa kusini kabisa wa inchi ya Yuda kuelekea mupaka wa Edomu ilikuwa: Kabuseli, Ederi, Yaguri, Kina, Dimona, Adada, Kedesi, Hazori, Itinani, Zifu, Telemu, Bealoti, Hazori-Hadata, Kerioti-Hesironi (ni kusema Hazori), Amamu, Sema, Molada, Hazari-Gada, Hesimoni, Beti-Peleti, Hazari-Suali, Beri-Seba, Biziotia, Bala, Iyimu, Ezemi, Eltoladi, Kesili, Horma, Ziklagi, Madimana, Sanisana, Lebaoti, Silhimu, Aini na Rimoni. Jumla ya miji makumi mbili na tisa pamoja na vijiji vyake. Miji iliyokuwa kwenye mabonde ilikuwa: Estaoli, Zora, Asina, Zanoa, Eni-Ganimu, Tapua, Enamu, Yarmuti, Adulamu, Soko, Azeka, Sarayimu, Aditaimu, Gedera na Gederotaimu. Jumla ya miji kumi na mine pamoja na vijiji vyake. Zenani, Hadaza, Migidali-Gadi, Dilani, Misipe, Yokiteli, Lakisi, Bozikati, Eguloni, Kaboni, Lamani, Kitilisi, Gederoti, Beti-Dagoni, Nama na Makeda. Jumla ya miji kumi na sita pamoja na vijiji vyake. Libuna, Eteri, Asani, Ifita, Asina, Nesibu, Keila, Akizibu na Maresa. Jumla ya miji tisa pamoja na vijiji vyake. Ekuroni pamoja na miji yake midogo na vijiji, Miji yote na vijiji vilivyokuwa karibu na Asidodi kati ya Ekuroni na bahari, Asidodi na Gaza pamoja na miji na vijiji vyake, mpaka kijito cha Misri mpaka pembeni ya bahari ya Mediteranea. Miji iliyokuwa kwenye eneo la milima ni: Samiri, Yatiri, Soko, Dana, Kiriati-Sana (au Debiri), Anabu, Estemoa, Animu, Goseni, Holoni na Gilo. Jumla ya miji kumi na mumoja pamoja na vijiji vyake. Arabu, Duma, Esani, Yanimu, Beti-Tapua, Afeka, Humuta, Kiriati-Arba (au Hebroni) na Siori. Jumla ya miji tisa pamoja na vijiji vyake. Maoni, Karmeli, Zifu, Yuta, Yezereheli, Yokidamu, Zanoa, Kaina, Gibea na Timuna. Jumla ya miji kumi pamoja na vijiji vyake. Halihuli, Beti-Zuri, Gedori, Marati, Beti-Anoti na Eltekoni. Jumla ya miji sita pamoja na vijiji vyake. Kiriati-Bali, unaoitwa tena Kiriati-Yearimu, na Raba. Jumla ya miji miwili pamoja na vijiji vyake. Miji ya jangwa ilikuwa: Beti-Araba, Midini, Sekaka, Nibusani, Muji wa Chumvi na Engedi. Jumla ya miji sita pamoja na vijiji vyake. 63 Lakini watu wa Yuda hawakuweza kuwafukuza Wayebusi, ambao ndio waliokuwa wenyeji wa Yerusalema, na mpaka leo Wayebusi wangali wanaishi katika muji ule pamoja na watu wa Yuda. |
Bible in Swahili Congo © Bible Society of the Democratic Republic of Congo (DRC), 2002.
Bible Society of the Democratic Republic of Congo