Yobu 28 - BIBLIA Maandiko Matakatifu Kwa Watu Wote 2002Sifa za hekima 1 Hakika kuna nafasi ya kuchimba feza, na pahali ambako zahabu inasafishwa. 2 Watu wanachimba chuma ndani ya udongo, wanayeyusha shaba kutoka mawe ya madini. 3 Wachimba madini wanaleta taa katika giza, wanatafutatafuta mpaka chini zaidi ya udongo, na kuchimbua mawe yenye madini katika giza. 4 Mwanadamu anachimba mashimo mbali na makao ya watu, mbali na watu pahali kusipofikiwa, wachimba madini wananinginia wakifungwa kamba. 5 Kutoka ndani ya udongo chakula kinapatikana, lakini chini yake kila kitu kinavurugwa kwa moto. 6 Katika mawe yake kunatoka mawe ya yakuti, na udongo wake una mavumbi ya zahabu. 7 Njia ya kwenda kule hakuna ndege mukula nyama anayeijua; na wala jicho la tai halijaiona. 8 Nyama wakali hawajaikanyaga wala simba mwenyewe hajapita ndani yake. 9 Mwanadamu anachimbua mawe magumu kabisa, anachimbua milima mpaka kwenye misingi yake. 10 Anapasua mifereji kati ya mawe makubwa, na jicho lake linaona mawe ya bei kali. 11 Anaziba chemichemi zisitiririke, na kufichua vitu vilivyofichwa. 12 Lakini hekima itapatikana wapi? Ni pahali gani panapopatikana maarifa? 13 Hakuna mutu anayejua bei ya hekima, wala hekima haipatikani katika inchi ya wanaokuwa wazima. 14 Vilindi vinasema: “Hekima haiko kwetu.” Bahari inasema: “Haiko kwangu.” 15 Hekima haiwezi kupatikana kwa zahabu, wala kwa kupima kiasi kingi cha feza. 16 Haiwezi kupimwa kwa zahabu ya Ofiri, wala kwa mawe ya sardoniki au ya yakuti samawi. 17 Zahabu au kioo havilingani nayo, wala haiwezi kubadilishwa na mawe ya zahabu safi. 18 Hekima ina bei kali kuliko mawe ya matumbawe na marijani, bei kali yake inashinda bei kali ya ushanga. 19 Topazi ya Etiopia haiwezi kulinganishwa nayo, wala haiwezi kupewa bei ya zahabu safi. 20 Basi, hekima inatoka wapi? Ni wapi panapopatikana maarifa? 21 Imefichwa mbali na macho ya viumbe vyote vyenye uzima, na ndege hawawezi kuiona. 22 Shimo la kuangamia na Kifo wanasema: “Tumesikia uvumi wake kwa masikio yetu.” 23 Mungu anajua njia ya hekima, anajua pahali inapopatikana. 24 Maana yeye anaona mpaka kwenye miisho ya dunia, anaona kila kitu chini ya mbingu. 25 Alipoupa upepo uzito wake na kuyapimia maji mipaka yake, 26 alipoamua mvua inyeshe wapi, umeme na radi vipite wapi, 27 pale ndipo alipoiona hekima na kuitangaza. Aliisimika na kuichunguza. 28 Kisha Mungu akamwambia mwanadamu: Sikia! Kumwogopa Bwana ndiyo hekima, na kujitenga na uovu ndiyo maarifa. |
Bible in Swahili Congo © Bible Society of the Democratic Republic of Congo (DRC), 2002.
Bible Society of the Democratic Republic of Congo