Walawi 7 - BIBLIA Maandiko Matakatifu Kwa Watu Wote 2002Sadaka za malipo ya kosa Sadaka za kuondoa zambi 1 Hii ndiyo sheria ya ibada kuelekea sadaka kwa ajili ya kosa. Sadaka hiyo ni takatifu kabisa. 2 Nyama wa sadaka kwa ajili ya kosa atachinjiwa pahali wanapochinjiwa nyama wa sadaka za kuteketezwa kwa moto na damu yake itanyunyizwa juu ya mazabahu pande zake zote. 3 Mafuta yake yote: mafuta ya mukia na yale yanayofunika matumbotumbo yatatolewa na kuteketezwa 4 pamoja na zile figo mbili pamoja na mafuta yake na ile sehemu bora ya maini. 5 Kuhani ataviteketeza juu ya mazabahu kama vile sadaka Yawe anayotolewa kwa moto. Hiyo ni sadaka kwa ajili ya kosa. 6 Wanaoruhusiwa kula sadaka hiyo ni wanaume wa ukoo wa makuhani peke yao; ni sadaka takatifu kabisa. Itakuliwa katika Pahali Patakatifu. 7 Sheria ni moja kuelekea sadaka kwa ajili ya kosa na sadaka kwa ajili ya zambi. Kuhani anayefanya ibada ya upatanisho ndiye atakayeitwaa. 8 Kuhani anayetolea sadaka ya kuteketezwa ya mutu yeyote, atatwaa ngozi ya nyama aliyetolewa. 9 Sadaka yoyote ya ngano iliyopikwa juu ya mafika katika chungu au katika kikaango itakuwa mali ya kuhani anayeitolea. 10 Kila sadaka ya ngano, ikuwe imechanganywa na mafuta au kavu, itakuwa ya wazao wa Haruni na wote wagawanyiwe kwa usawa. Sadaka za amani 11 Hii ndiyo sheria ya ibada kuelekea sadaka za amani ambazo mutu anaweza kumutolea Yawe. 12 Ikiwa mutu anatoa sadaka hiyo kwa kumushukuru Mungu, basi, ataitoa pamoja na maandazi yasiyotiwa chachu yaliyopakwa mafuta, mikate myembamba iliyopakwa mafuta na maandazi ya unga laini uliochanganywa na mafuta. 13 Pamoja na sadaka yake hiyo ya amani ya kumushukuru Mungu, ataleta maandazi yaliyotiwa chachu. 14 Kutokana na maandazi hayo, atamutolea Yawe andazi moja kutoka kila sadaka. Maandazi hayo yatakuwa ya kuhani anayenyunyizia mazabahu damu ya sadaka za amani. 15 Nyama ya sadaka hiyo ya amani ya kumushukuru Mungu itakuliwa siku hiyohiyo inapotolewa. Hataacha hata sehemu yake mpaka asubui. 16 Lakini kama sadaka hiyo ya amani ni ya kutimiza kiapo au ya mapenzi mema, itakuliwa siku hiyohiyo inapotolewa na sehemu ingine inaweza kukuliwa kesho yake. 17 Lakini nyama yoyote ya sadaka hiyo inayobaki mpaka kwa siku ya tatu itateketezwa. 18 Kama nyama yoyote ya sadaka ya amani inakuliwa kwa siku ya tatu, mutu aliyeitoa hatakubaliwa, wala hiyo sadaka haitapokelewa kwa faida yake. Nyama hiyo ni chukizo na mutu atakayeikula atabeba lazima ya uovu wake. 19 Nyama yoyote inayogusa kitu kinachohesabiwa kuwa kichafu isikuliwe. Nyama hiyo itateketezwa kwa moto. Wote wanaohesabiwa kuwa safi wanaweza kula nyama 20 iliyotolewa sadaka ya amani kwa Yawe. Lakini mutu yeyote anayehesabiwa kuwa muchafu akikula nyama hiyo, atatengwa na watu wake. 21 Mutu yeyote anayegusa kitu chochote kinachohesabiwa kuwa kichafu, au kitu cha mutu kinachohesabiwa kuwa kichafu, au nyama anayehesabiwa kuwa muchafu, au kitu chochote kinahesabiwa kuwa kichafu ambacho ni chukizo, akikula nyama ya sadaka ya amani Yawe aliyotolewa, mutu huyo atatengwa na watu wake. 22 Yawe akamwambia Musa: 23 Uwaambie Waisraeli hivi: Musikule mafuta ya ngombe au ya kondoo au ya mbuzi. 24 Mafuta ya nyama yoyote aliyekufa mwenyewe au ya nyama aliyeuawa na nyama wa pori yanaweza kuwekwa kwa matumizi mengine, lakini musiyakule. 25 Mutu yeyote akikula mafuta ya nyama aliyetolewa kwa Yawe kwa moto, atatengwa na watu wake. 26 Tena, musikule damu yoyote, ikuwe ya ndege au ya nyama pahali popote munapoishi. 27 Mutu yeyote akikula damu yoyote, atatengwa na watu wake. 28 Yawe akamwambia Musa: 29 Uwaambie watu wa Israeli hivi: Mutu yeyote akitoa sadaka ya amani, atamupa Yawe sehemu ya sadaka hiyo. 30 Atamuletea kwa mikono yake mwenyewe kama vile sadaka ya kuteketezwa kwa moto. Ataleta mafuta yake pamoja na kilali ambacho atafanya nacho kitambulisho cha kumutolea Yawe. 31 Kuhani atateketeza mafuta yote juu ya mazabahu, lakini kilali kitakuwa cha Haruni na wana wake makuhani. 32 Muguu wa kuume wa nyuma wa nyama wa sadaka zenu za amani mutamupa kuhani. 33 Muguu huo utakuwa mali ya kuhani anayekuwa muzao wa Haruni anayetolea damu ya sadaka za amani na mafuta yake. 34 Yawe amewaagiza watu wa Israeli watenge kilali hicho na muguu huo wa nyama wa sadaka zao za amani, wamupe kuhani Haruni na wazao wake, maana sehemu hiyo imewekewa kwa hao makuhani milele. 35 Hiyo ndiyo sehemu iliyotengwa kwa ajili ya Haruni na wana wake kutoka katika sadaka Yawe anazotolewa kwa moto, tangu siku walipowekwa kuwa makuhani wa Yawe. 36 Walipotakaswa kwa kupakwa mafuta, Yawe aliamuru Waisraeli wawape sehemu hiyo ya sadaka; hiyo itakuwa siku zote haki yao. 37 Basi, hii ndiyo sheria kuelekea sadaka ya kuteketezwa, sadaka ya vyakula, sadaka kwa ajili ya zambi, sadaka kwa ajili ya kosa, kuelekea kutakaswa na kuelekea sadaka ya amani. 38 Yawe akamupa Musa amri hizi juu ya mulima Sinai siku ile alipowaamuru Waisraeli wamuletee sadaka zao, kule katika jangwa la Sinai. |
Bible in Swahili Congo © Bible Society of the Democratic Republic of Congo (DRC), 2002.
Bible Society of the Democratic Republic of Congo