Hesabu 36 - BIBLIA Maandiko Matakatifu Kwa Watu Wote 2002Urizi wa wanawake walioolewa 1 Viongozi wa jamaa katika ukoo wa Gileadi mwana wa Makiri, mwana wa Manase mwana wa Yosefu, wakakwenda kuzungumuza na Musa na viongozi wengine wa ukoo za Waisraeli. 2 Wakasema: Yawe alikuamuru kuwagawanyia watu wa Israeli inchi kwa kura kuwa urizi wao; alikuamuru vilevile uwape wabinti za Selofehadi ndugu yetu urizi wa baba yao. 3 Lakini wao wakiolewa na Waisraeli wa makabila mengine, urizi wao utatoka kwetu na kuwaendea watu wa kabila watakamoolewa; kwa hiyo urizi wetu sisi utapunguka. 4 Katika sikukuu ya ukumbusho urizi wao utahesabiwa pamoja na ule wa kabila watakamoolewa na hivyo kabila letu halitapata urizi huo tena. 5 Basi, Musa akawapa Waisraeli agizo lile kutoka kwa Yawe, akawaambia: Watu wa ukoo wa kabila la Yosefu wamesema ukweli. 6 Na hivi ndivyo Yawe anavyoamuru juu ya wabinti za Selofehadi; wako huru kuolewa na mutu yeyote wanayemupenda, lakini waolewe katika kabila lao, 7 kusudi urizi wa Waisraeli usihamishiwe kwa kabila lingine; kila Mwisraeli atabakia na urizi wa kabila lake. 8 Mwanamuke yeyote mwenye urizi katika kabila moja la Israeli anapaswa kuolewa na mutu wa kabila lake, kusudi kila Mwisraeli abakie na urizi wa babu zake. 9 Hivyo hakutakuwa urizi wowote utakaohamishwa kutoka kabila moja kwa lingine. Kila kabila la Waisraeli litashikilia urizi wake. 10 Wabinti za Selofehadi wakafanya kama vile Yawe alivyomwamuru Musa. 11 Wote: Mala, Tirsa, Hogla, Milka na Noa wakaolewa na binamu zao. 12 Wakaolewa katika jamaa za ukoo wa Manase mwana wa Yosefu, na urizi wao ukabaki katika kabila la baba yao. 13 Hizo ndizo amri na maagizo ambayo Yawe aliwapa Waisraeli kwa njia ya Musa katika mabonde ya Moabu, ngambo ya muto Yordani karibu na muji wa Yeriko. |
Bible in Swahili Congo © Bible Society of the Democratic Republic of Congo (DRC), 2002.
Bible Society of the Democratic Republic of Congo