Hesabu 2 - BIBLIA Maandiko Matakatifu Kwa Watu Wote 2002Kupangwa kwa makabila 1 Yawe akawapa Musa na Haruni, maagizo haya: 2 Waisraeli watapiga kambi zao, kila mumoja akikaa pahali penye bendera yake, penye vitambulisho vya ukoo wake. Watapiga kambi zao kuzunguka na kuelekea hema la mukutano. 3 Wale watakaopiga kambi upande wa mashariki watakuwa kikundi cha watu wanaokuwa chini ya bendera ya Yuda na kiongozi wao atakuwa Nasoni mwana wa Aminadabu. 4 Jeshi lake kulingana na hesabu ni wanaume elfu makumi saba na ine na mia sita. 5 Wale watakaofuata kupiga kambi nyuma ya watu wa Yuda watakuwa kabila la Isakari. Kiongozi wao atakuwa Netaneli mwana wa Suari. 6 Jeshi lake kulingana na hesabu ni wanaume elfu makumi tano na ine na mia ine. 7 Kisha kabila la Zebuluni, kiongozi wao akiwa Eliabu mwana wa Heloni, 8 jeshi lake kulingana na hesabu ni wanaume elfu makumi tano na saba na mia ine. 9 Jumla yote ya watu watakaokuwa katika kambi ya Yuda kulingana na jeshi lake ni watu elfu mia moja makumi nane na sita na mia ine. Hao ndio watakaotangulia kusafiri. 10 Kwa upande wa kusini, wale wanaokuwa chini ya bendera ya kundi la Rubeni kulingana na jeshi lake, kiongozi wao akiwa Elisuri mwana wa Sedeuri, 11 jeshi lake kulingana na hesabu ni wanaume elfu makumi ine na sita na mia tano. 12 Kisha wale watakaopiga kambi kando ya watu wa Rubeni watakuwa ni watu wa kabila la Simeoni, kiongozi wao akiwa Selumieli mwana wa Suri-Sadai, 13 jeshi lake kulingana na hesabu ni wanaume elfu makumi tano na tisa na mia tatu. 14 Halafu kabila la Gadi, kiongozi wao akiwa Eliasafu mwana wa Reueli, 15 jeshi lake kulingana na hesabu ni wanaume elfu makumi ine na tano mia sita na makumi tano. 16 Jumla ya wanaume watakaokuwa katika kambi ya Rubeni kulingana na jeshi lake ni watu elfu mia moja makumi tano na moja mia ine na makumi tano. Hawa ndio watakaokuwa katika kundi la pili. 17 Halafu, kambi ya kabila la Walawi likiwa katikati ya kambi zote nao wakibeba hilo hema la mukutano wataondoka; kila kundi likisafiri kwa kufuata nafasi yake kwa bendera. 18 Kwa upande wa magaribi, wale wanaokuwa chini ya bendera ya kundi la Efuraimu watapiga kambi kulingana na jeshi lake kiongozi wao akiwa Elisama mwana wa Amihudi, 19 jeshi lake kulingana na hesabu ni wanaume elfu makumi tatu na mbili na mia mbili. 20 Mara tu nyuma ya Waefuraimu litafuata kabila la Manase: kiongozi wake akiwa Gamalieli mwana wa Pedasuri, 21 jeshi lake kulingana na hesabu litakuwa watu elfu makumi tatu na mbili na mia mbili. 22 Kisha kabila la Benjamina: kiongozi wake ni Abidani, mwana wa Gideoni, 23 jeshi lake kulingana na hesabu ni wanaume elfu makumi tatu na tano na mia ine. 24 Jumla ya watu waliokuwa katika kambi ya Efuraimu kulingana na jeshi lake ni watu elfu mia moja na nane na mia moja. Hawa ndio watakaokuwa katika kundi la tatu. 25 Kwa upande wa kaskazini, watapiga kambi katika jeshi lake wale wanaokuwa chini ya bendera ya Dani, kiongozi wao atakuwa Ahiezeri, mwana wa Amishadai, 26 jeshi lake kulingana na hesabu litakuwa na watu elfu makumi sita na mbili na mia saba. 27 Kisha wale watakaopiga kambi nyuma yao watakuwa watu wa kabila la Aseri, kiongozi wao akiwa Pagieli mwana wa Okrani, 28 jeshi lake kulingana na hesabu litakuwa na watu elfu makumi ine na moja na mia tano. 29 Kisha watu wa kabila la Nafutali, kiongozi wake akiwa Ahira mwana wa Enani, 30 jeshi lake kulingana na hesabu, ni wanaume elfu makumi tano na tatu na mia ine. 31 Jumla ya watu waliokuwa katika kambi ya Dani kulingana na jeshi lake ni watu elfu mia makumi tano na saba na mia sita. Hawa ndio watakaokuwa katika kundi la mwisho nyuma ya bendera zao. 32 Hao ndio Waisraeli waliohesabiwa kulingana na ukoo zao, katika kambi na majeshi yao, wote walikuwa elfu mia sita na tatu na mia tano makumi tano. 33 Lakini Walawi hawakuhesabiwa kati ya watu wa Israeli kama vile Yawe alivyomwamuru Musa. 34 Hivi ndivyo, Waisraeli walivyofanya kila kitu kama vile Yawe alivyomwamuru Musa. Wakapiga kambi zao, kufuata bendera zao na wakasafiri kila mumoja akiandamana na jamaa yake kwa kufuata ukoo wake. |
Bible in Swahili Congo © Bible Society of the Democratic Republic of Congo (DRC), 2002.
Bible Society of the Democratic Republic of Congo