Siku moja, wakati wa mazishi, watu waliona moja kati ya makundi yale. Wakatupa maiti katika kaburi la Elisha na kukimbia. Mara tu maiti hiyo ilipogusa mifupa ya Elisha, ilifufuka na kusimama wima.
Bwana wetu Yawe atakiangamiza kifo milele! Atayafuta machozi katika nyuso za watu wote na kuondoa haya ya watu wake katika dunia yote. Yawe amesema hivyo.
Wafu wako wataishi tena, miili yao itafufuka. Wanaolala katika mavumbi wataamuka na kuimba kwa furaha! Mungu atapeleka umande wake wa uzima, nao wanaokuwa kwa wafu watatoka wazima.
Inanipasa kuwakomboa hawa watu kutoka kuzimu; sharti niwaokoe kutoka kifo! Ewe kifo, mapigo yako ni wapi? Ewe kuzimu, kuangamiza kwako ni wapi? Mimi sitawaonea tena huruma!