Mukuje basi enyi wabinti wa Sayuni, mumwone mufalme Solomono. Amevaa taji aliyovalishwa na mama yake, siku alipofanya ndoa yake, siku ambayo moyo wake ulijaa furaha.
Bwana wetu Yawe atakiangamiza kifo milele! Atayafuta machozi katika nyuso za watu wote na kuondoa haya ya watu wake katika dunia yote. Yawe amesema hivyo.
Enyi watu wa Sayuni, enyi watu wa Yerusalema, hakika ninyi hamutaomboleza tena. Kweli Mungu atawahurumia; mara tu atakaposikia kilio chenu atawaitikia.
Waliokombolewa na Yawe watarudi, watakuja Sayuni wakipiga vigelegele. Watakuwa wenye furaha ya milele, watajaliwa furaha na shangwe; huzuni na kilio vitatoweka kabisa.
Watu wako uliowakomboa, ee Yawe, watarudia, watakuja Sayuni wakiimba; watajaa furaha ya milele, watapata furaha na shangwe. Huzuni na maombolezo vitatoweka kabisa.
Mimi Yawe nitaufariji Sayuni, nitatengeneza pahali pake pote palipoharibika. Nitazifanya mbuga zake kama shamba la Edeni, jangwa yake kama bustani ya Yawe. Ndani yake kutapatikana furaha na shangwe, na nyimbo za shukrani zitasikilika humo.
Mwangaza wako muchana hautatua kama jua, wala mwangaza wako usiku kufifia kama mbalamwezi; maana Yawe ni mwangaza wako milele, nazo siku zako za kuomboleza zitakoma.
Watakuja na kuimba kwa sauti juu ya mulima Sayuni, watapata utukufu juu ya wema wangu mimi Yawe, kwa ajili ya ngano, divai na mafuta ninavyowapa, kwa ajili ya kondoo na ngombe vilevile; maisha yao yatakuwa kama bustani iliyotiliwa maji, wala hawataregea tena.
Yawe, Mungu wako, yuko pamoja nawe. Yeye ni shujaa anayekuletea ushindi. Yeye atakufurahia kwa furaha kubwa. Kwa upendo wake atakujalia uzima mupya. Atakufurahia kwa wimbo wa sauti kubwa,
Kwa maana Mwana-Kondoo anayekuwa katikati ya kiti cha kifalme, atawachunga na kuwaongoza kwenye chemichemi ya maji ya uzima. Naye Mungu atawapanguza machozi yao yote.”