Maana kwa siku sita mimi Yawe niliumba mbingu na inchi, bahari na vyote vinavyokuwa ndani yake, kisha nikapumzika siku ya saba. Kwa hiyo mimi Yawe nilibariki siku ya Sabato, nikaitakasa.
Ni nani anayeweza kupima maji ya bahari katika kitanga cha mukono wake, na kuzipima mbingu kwa mikono yake? Ni nani anayeweza kuutia udongo wa dunia katika kikombe; kuipima milima kwa mizani au vilima kwa kipimo cha uzito?
Dunia iliumbwa na yule anayeikaa juu ya mbingu; kutoka huko wakaaji wa dunia ni kama mapanzi! Yeye ametandika mbingu kama pazia, na kuzikunjua kama hema la kuishi ndani yake.
Muinue macho yenu juu mbinguni! Ni nani aliyeziumba nyota hizo? Ni yule anayeziongoza kama jeshi lake, anayeijua hesabu yake yote, anayeziita kila moja kwa jina lake. Kwa sababu yeye ni mwenye nguvu nyingi, hakuna hata moja inayokosekana.
Hivi ndivyo anavyosema Yawe aliyeumba mbingu na kuzitandika kama hema, aliyeifanya dunia na vyote vinavyokuwa ndani yake, anayewapa watu wanaokaa ndani yake uzima, na kuwajalia uzima wote wanaoishi ndani yake:
Hivi ndivyo anavyosema Yawe aliyeumba mbingu, ndiye Mungu aliyeipa dunia umbo na kuifanya na kuiimarisha. Hakuiumba kusudi ibaki ukiwa, lakini aliipa umbo kusudi iikaliwe na viumbe vyake: Mimi ni Yawe, wala hakuna mwingine.
Wewe umenisahau mimi Yawe Muumba wako, niliyezitandaza mbingu, na kuiweka misingi ya dunia! Kwa sababu ya kasirani ya yule anayekutesa, unaendelea kuogopa siku zote kwamba yuko tayari kukuangamiza! Lakini hasira yake itafikia wapi?
Ni sawa vile inavyoandikwa katika Maandiko Matakatifu: “Nimekuweka kuwa babu wa mataifa mengi.” Abrahamu alimwamini Mungu, kwa hiyo yeye ni baba yetu mbele yake. Ni yeye Mungu anayewafufua wafu na kuamuru vitu visivyokuwa vipate kuwa.