Zaburi 92 - BIBLIA Maandiko Matakatifu Kwa Watu Wote 2002Wimbo wa kumusifu Mungu 1 Zaburi. Wimbo wa Siku ya Sabato. 2 Ni vizuri kukushukuru, ee Yawe, kuliimbia jina lako sifa, ee Mungu Mukubwa. 3 Ni vizuri kutangaza wema wako asubui, na uaminifu wako kwa wakati wa usiku, 4 kwa muziki wa zeze na kinubi, kwa sauti tamu ya zeze. 5 Ee Yawe, matendo yako makubwa yananifurahisha; nitashangilia kwa sababu ya mambo yote uliyotenda. 6 Matendo yako, ee Yawe, ni makubwa sana! Mawazo yako hayatambulikani! 7 Mutu mupumbafu hawezi kufahamu, wala mujinga hajui jambo hili: 8 kwamba waovu wanaweza kustawi kama majani, watenda maovu wote wanaweza kufanikiwa, lakini mwisho wao ni kuangamia milele. 9 Lakini wewe, ee Yawe, ni mukubwa kwa milele. 10 Hao waadui zako, ee Yawe, hao waadui zako, hakika wataangamia; wote wanaotenda maovu, watatawanyika! 11 Wewe umenipa nguvu kama mbogo; umenimimia mafuta kwa kunifurahia. 12 Kwa macho yangu, nimeona waadui zangu wameshindwa; kwa masikio yangu, nimesikia kilio cha wanaotenda maovu. 13 Watu wa haki wanastawi kama mingazi; wanakomaa kama mierezi ya Lebanoni! 14 Kama miti iliyopandwa katika nyumba ya Yawe, wanastawi katika viwanja vya Mungu wetu; 15 inaendelea kuzaa matunda hata katika uzee; siku zote wamejaa utomvu na wabichi, 16 wapate kutangaza kwamba Yawe ni wa usawa. Yeye ni kikingio changu. Kwake hakuna upotovu. |
Bible in Swahili Congo © Bible Society of the Democratic Republic of Congo (DRC), 2002.
Bible Society of the Democratic Republic of Congo