Zaburi 9 - BIBLIA Maandiko Matakatifu Kwa Watu Wote 2002Shukrani kwa Mungu 1 Kwa mukubwa wa waimbaji. Kwa mutindo wa wimbo “Kilio cha mwana.” 2 Nitakushukuru wewe Mungu kwa moyo wangu wote; nitayaeleza matendo yako yote ya ajabu. 3 Nitafurahi na kushangilia kwa ajili yako; nitaliimbia sifa jina lako, ewe Mungu Mukubwa. 4 Waadui zangu walirudi nyuma, walijikwaa na kuangamia mbele yako. 5 Umeitetea haki yangu katika maneno yangu; umeikaa katika kiti chako cha kifalme, wewe mwamuzi wa haki. 6 Umeyakaripia mataifa, umewaangamiza waovu; umeyafuta majina yao kwa milele. 7 Waadui wameangamia milele; umeiongoa miji yao, ukumbusho wao umetoweka. 8 Lakini Yawe anatawala milele; ameweka kiti chake cha kifalme, apate kuhukumu. 9 Anauhukumu ulimwengu kwa haki; anayaamua mataifa kama vile inavyofaa. 10 Yawe ni kikingio cha watu wanaoonewa; yeye ni kikingio katika nyakati za taabu. 11 Wanaojua jina lako, wanakutegemea, kwa maana wewe, ee Yawe, hauwatupi wanaokutafuta. 12 Mumwimbie sifa Yawe anayekaa Sayuni! Muyatangazie mataifa mambo aliyotenda! 13 Mungu analipiza kisasi cha damu iliyomwangwa; wala hasahau hata kidogo kilio cha wenye kuonewa. 14 Ee Yawe, wewe unayeniopoa kutoka nguvu za kifo, uangalie mateso wale wanaonichukia wanayoniletea na kunirehemu 15 kusudi nitangaze sifa zako mbele ya watu wa Sayuni, nipate kushangilia kwa sababu umeniokoa. 16 Mataifa yameanguka katika shimo walilochimba, miguu yao imenaswa kwenye wavu waliotega. 17 Yawe amejitambulisha; anatoa hukumu. Waovu wamenaswa kwa matendo yao wenyewe. 18 Waovu wataishia katika kuzimu; ndiyo mataifa yote yanayomusahau Mungu. 19 Lakini wakosefu hawatasahauliwa siku zote; tumaini la wamasikini halitapotea milele. 20 Ee Yawe, simama sasa mwanadamu asishinde! Uyakusanye sasa hivi mataifa mbele yako, uyahukumu. 21 Uyatie hofu, ee Yawe, watu wa mataifa watambue kwamba wao ni watu tu! |
Bible in Swahili Congo © Bible Society of the Democratic Republic of Congo (DRC), 2002.
Bible Society of the Democratic Republic of Congo