Zaburi 79 - BIBLIA Maandiko Matakatifu Kwa Watu Wote 2002Maombi kwa ajili ya hasara la taifa 1 Zaburi ya Asafu. Ee Mungu, watu wasiokujua wameshambulia inchi yako. Wamechafua hekalu lako takatifu, wameugeuza Yerusalema kuwa mabomoko. 2 Wameacha maiti za watumishi wako zikuliwe na ndege, wametoa miili ya watu wako kwa wanyama wa pori. 3 Damu yao imemwangwa kama maji katika Yerusalema, wamelazwa humo, wala hakuna wa kuwazika. 4 Tunazarauliwa na mataifa jirani, jirani zetu wanatuchekelea na kutusimanga. 5 Ee Yawe, utakasirika hata milele? Hasira yako itawaka kama moto hata wakati gani? 6 Uyamwangie mataifa yasiyokujua hasira yako, ndizo, tawala zote zisizoheshimu jina lako. 7 Maana wamemeza wazao wa Yakobo, wameteketeza kabisa makao ya taifa lako. 8 Usituazibu kwa sababu ya makosa ya babu zetu. Huruma yako itufikie haraka, maana tumegandamizwa sana! 9 Utusaidie, ee Mungu, mwokozi wetu kwa utukufu wa jina lako. Utuokoe na kutusamehe zambi zetu, kwa ajili ya jina lako. 10 Kwa nini mataifa yatuambie: “Mungu wenu yuko wapi?” Utujalie tuone jinsi utakavyowalipiza mataifa kisasi kwa ajili ya mauaji ya watumishi wako. 11 Kilio cha hao wafungwa kikufikie; kwa nguvu yako kubwa uwaokoe waliohukumiwa kufa. 12 Ee Bwana, uwalipize mataifa jirani mara saba kwa ajili ya matusi waliyokutukana. 13 Nasi watu wako, sisi kondoo wa kundi lako, tutakushukuru milele, na kukusifu nyakati zote. |
Bible in Swahili Congo © Bible Society of the Democratic Republic of Congo (DRC), 2002.
Bible Society of the Democratic Republic of Congo