Zaburi 65 - BIBLIA Maandiko Matakatifu Kwa Watu Wote 2002Wimbo wa shukrani 1 Kwa mukubwa wa waimbaji. Zaburi. Wimbo wa Daudi. 2 Ee Mungu, unastahili sifa huko Sayuni. Watu wanapaswa kukutimizia viapo vyao, 3 maana wewe unajibu maombi yetu. Wanadamu wote watakuja kwako wewe peke. 4 Tunapolemewa na makosa yetu, wewe mwenyewe unatusamehe. 5 Heri wale unaowachagua na kuwaleta karibu, waishi katika kiwanja chako. Sisi tutatoshelewa na mazuri ya nyumba yako, mazuri ya hekalu lako takatifu. 6 Kwa matendo yako makubwa unatuitikia na kutuokoa, ewe Mungu mwokozi wetu. Wewe ndiwe tumaini la viumbe vyote katika dunia yote na mbali katika bahari. 7 Kwa nguvu yako uliisimika milima pahali pake. Wewe una nguvu nyingi! 8 Unatuliza uvumi wa bahari na wa mawimbi yake, unakomesha fujo za watu. 9 Wakaaji wa miisho ya dunia wanashangazwa na vitambulisho vyako. Unasababisha furaha kila pahali, tokea mashariki hata magaribi. 10 Wewe unatunza udongo kwa kuunyeshea mvua, unaujalia mboleo na kuustawisha; muto wako umejaa maji tele, unaifanikisha inchi na kuipatia mavuno. Hivi ndivyo unavyotayarisha udongo. 11 Unanyeshea mashamba mvua kwa wingi, na kuyalowanisha kwa maji; unalainisha udongo kwa manyunyu, na kubariki mimea ichipuke. 12 Unakamilisha mwaka kwa kutupatia mazao mazuri; kila nafasi ulipopita kumejaa utajiri. 13 Mbuga za majani zimejaa mifugo, milima nayo imejaa furaha. 14 Mashamba ya kulishia nyama yamejaa kondoo, mabonde yamefunikwa na ngano. Kila kitu kinashangilia kwa furaha. |
Bible in Swahili Congo © Bible Society of the Democratic Republic of Congo (DRC), 2002.
Bible Society of the Democratic Republic of Congo