Zaburi 61 - BIBLIA Maandiko Matakatifu Kwa Watu Wote 2002Kuomba ulinzi 1 Kwa mukubwa wa waimbaji. Kwa vyombo vyenye nyuzi. Zaburi ya Daudi. 2 Usikie kilio changu, ee Mungu, usikilize maombi yangu. 3 Ninakulilia kutoka miisho ya dunia, nikikuwa nimevunjika moyo. Uniongoze juu kwenye mulima ambako siwezi kujifikisha. 4 Wewe ndiwe kimbilio langu, boma langu lenye nguvu la kukimbilia waadui. 5 Ninaomba nikae katika nyumba yako milele, nipate kukimbilia chini ya mabawa yako. 6 Ee Mungu, umesikia viapo vyangu, umenijalia sehemu yangu unayowapa wale wanaokuabudu. 7 Umujalie mufalme maisha marefu, miaka yake ikuwe ya vizazi vingi. 8 Atawale milele mbele yako, ee Mungu; wema na uaminifu wako vimulinde. 9 Hivyo nitakuimbia nyimbo za sifa, nikitimiza viapo vyangu kila siku. |
Bible in Swahili Congo © Bible Society of the Democratic Republic of Congo (DRC), 2002.
Bible Society of the Democratic Republic of Congo