Zaburi 30 - BIBLIA Maandiko Matakatifu Kwa Watu Wote 2002Maombi ya shukrani 1 Mashairi yanayoelekea muzinduo wa hekalu. Zaburi ya Daudi. 2 Ninakutukuza, ee Yawe, maana umeniokoa, wala haukuwaacha waadui zangu wanisimange. 3 Ee Yawe, Mungu wangu, nilikulilia, nawe ukaniponyesha. 4 Ee Yawe, umeniokoa kutoka kuzimu; umenipa tena uzima, umenitoa kutoka kati ya wafu. 5 Mumwimbie Yawe sifa, enyi waaminifu wake; mukumbuke utakatifu wake na kumushukuru. 6 Hasira yake inadumu muda kidogo tu, upendo wake unadumu milele. Kilio kinaweza kuwa usiku, lakini muchana kunatokea furaha. 7 Mimi nilipofanikiwa, nilisema: “Sitashindwa hata kidogo! 8 Kwa upendo wako, ee Yawe, umeniimarisha kama mulima mukubwa.” Lakini ukajificha mbali nami, nami nikafazaika. 9 Nilikulilia wewe, ee Yawe; nilikusihi, ee Yawe: 10 “Utapata faida gani nikikufa na kushuka mpaka katika shimo la wafu? Mavumbi ya wafu yanaweza kukusifu? Yanaweza kusimulia uaminifu wako? 11 Usikie, ee Yawe, unihurumie; ee Yawe, unisaidie!” 12 Wewe umegeuza malalamiko yangu kuwa ngoma ya furaha; umeniondolea huzuni yangu, ukanijaza furaha. 13 Mimi nitakusifu wala sitakaa kimya. Ee Yawe, Mungu wangu, nitakushukuru milele. |
Bible in Swahili Congo © Bible Society of the Democratic Republic of Congo (DRC), 2002.
Bible Society of the Democratic Republic of Congo