Zaburi 27 - BIBLIA Maandiko Matakatifu Kwa Watu Wote 2002Kwa Mungu kuna usalama 1 Zaburi ya Daudi. Yawe ni mwangaza wangu na wokovu wangu, ni nani nitakayemwogopa? Yawe ni mulinzi wa maisha yangu, sitamwogopa mutu yeyote. 2 Waovu wakinishambulia, na kutaka kuniangamiza, hao wapinzani wangu watajikwaa na kuanguka. 3 Hata jeshi likinizunguka, moyo wangu hautaogopa kitu; hata nikishambuliwa kwa vita, sitakata tumaini. 4 Jambo moja nimemwomba Yawe, ninatafuta hili tu: nikae ndani ya nyumba ya Yawe siku zote za maisha yangu, niuone uzuri wa Yawe, na kutafuta maongozi yake ndani ya hekalu lake. 5 Siku ya taabu atanificha ndani ya nyumba yake; atanificha katika hema lake, atanilinda salama juu ya mulima. 6 Nami nitawaangalia kwa majivuno waadui zangu wanaonizunguka. Nitamutolea Yawe sadaka kwa shangwe, ndani ya hekalu lake, nitaimba na kumushangilia. Musaada unapatikana kwa Mungu 7 Usikie, ee Yawe, ninapokulilia, unionee huruma na kunijibu. 8 Moyo wangu unaniambia: “Kuja umutafute Mungu!” Basi, ninakutafuta, ee Yawe. 9 Usinigeuzie mugongo, usinikatae kwa hasira mimi mutumishi wako. Wewe umekuwa siku zote musaada wangu. Usinitupe wala usiniachilie, ee Mungu Mwokozi wangu. 10 Hata kama wazazi wangu wakinitupa, Yawe atanipokea kwake. 11 Unifundishe njia yako, ee Yawe. Uniongoze katika njia inayokuwa sawa kwa sababu ya waadui zangu. 12 Usiniache waadui wanitendee wanavyopenda; maana washuhuda wa uongo wananiinukia, nao wanatoa vitisho vyao vikali. 13 Ninaamini kwamba nitauona uzuri wa Yawe katika makao ya wazima. 14 Umutegemee Yawe! Ujitie moyo, ukuwe hodari! Umutegemee Yawe! |
Bible in Swahili Congo © Bible Society of the Democratic Republic of Congo (DRC), 2002.
Bible Society of the Democratic Republic of Congo