Biblia Todo Logo
Bìoball air-loidhne

- Sanasan -

Zaburi 119 - BIBLIA Maandiko Matakatifu Kwa Watu Wote 2002


Sheria ya Mungu

1 Heri watu wanaoishi katika ukamilifu, wanaofuata sheria ya Yawe.

2 Heri wanaoshika maagizo yake, wanaomutafuta kwa moyo wao wote,

3 watu wasiotenda uovu hata kidogo, lakini wanafuata siku zote njia zake.

4 Ee Mungu, umetupatia kanuni zako kusudi tuzishike kwa uangalifu.

5 Heri mwenendo wangu ungeimarika kwa kuyafuata masharti yako!

6 Nikichunguza amri zako zote, hapo kweli sitapata haya.

7 Nitakusifu kwa moyo wenye kunyooka, nikijifunza maamuzi yako ya haki.

8 Nitafuata masharti yako; usiniache hata kidogo.


Kutii sheria ya Mungu

9 Namna gani kijana ataweza kujichunga katika njia safi? Ni kwa kufuatilia neno lako.

10 Ninakutafuta kwa moyo wote; usiniachilie kugeuka mbali na amri zako.

11 Nimeshika neno lako ndani ya moyo wangu, kusudi nisikukosee.

12 Utukuzwe, ee Yawe! Unifundishe masharti yako.

13 Nitarudiliarudilia kwa sauti maamuzi yako yote uliyotoa.

14 Ninafurahi kufuata maagizo yako, kuliko kuwa na utajiri mwingi.

15 Ninafikiri juu ya kanuni zako, na kuangalia njia zako.

16 Ninafurahia masharti yako; sitasahau neno lako.


Kufurahia sheria ya Mungu

17 Unitendee mimi mutumishi wako kwa wema, nipate kuishi na kushika neno lako.

18 Uyafungue macho yangu, nipate kuona maajabu ya sheria yako.

19 Mimi ni mugeni tu hapa katika dunia; usinifiche amri zako.

20 Roho yangu inaugua kwa hamu kubwa ya kutaka kujua siku zote maamuzi yako.

21 Wewe unawakaripia wenye kiburi waliolaaniwa, ambao wanageuka mbali na amri zako.

22 Uniepushe na matusi na mazarau yao, maana ninafuata maagizo yako.

23 Hata kama wakubwa wananifanyia shauri baya, mimi mutumishi wako nitafikiri juu ya masharti yako.

24 Maagizo yako ndiyo furaha yangu; hayo ndio washauri wangu.


Kushika sheria ya Mungu

25 Ninagaagaa chini ndani ya mavumbi; unirudishie uzima sawa ulivyoahidi.

26 Nimeungama niliyotenda, nawe ukanijibu; unifundishe masharti yako.

27 Unifundishe namna ya kushika kanuni zako, nami nitafikiri juu ya matendo yako ya ajabu.

28 Ninalia kwa uchungu; unirudishie nguvu kama ulivyoahidi.

29 Uniepushe na njia za upotovu; unifundishe kwa huruma sheria yako.

30 Nimechagua njia ya uaminifu; nitafuatilia maamuzi yako.

31 Ninashikamana na maagizo yako, ee Yawe; usikubali nipatishwe haya!

32 Nitafuatilia amri zako, maana unanifungua akili zaidi.


Kuomba hekima

33 Ee Yawe, unifundishe kutii masharti yako, nami nitayashika mpaka mwisho.

34 Unieleweshe nipate kushika sheria yako, niifuate kwa moyo wangu wote.

35 Uniongoze katika njia ya amri zako, maana humo ninapata furaha yangu.

36 Uvute moyo wangu kufuata maagizo yako, na si kwa ajili ya kupata faida isiyofaa.

37 Uniepushe nisifuate mambo ya ovyo; unionyeshe njia yako, unipe uzima.

38 Unitimizie mimi mutumishi wako ahadi yako; ahadi unayowapa wale wanaokuheshimu.

39 Uniepushe na matusi ninayoogopa; maana maamuzi yako ni mema.

40 Ninatamani sana kutii kanuni zako; unirudishie uzima maana wewe ni wa haki.

41 Wema wako unifikie, ee Yawe; uniokoe kama ulivyoahidi.

42 Hapo nitaweza kuwajibu hao wanaonitukana, maana mimi ninatumainia neno lako.

43 Unijalie kusema ukweli wako siku zote, maana ninatumainia maamuzi yako.

44 Nitatii sheria yako siku zote, nitaishika milele na milele.

45 Nitaishi katika uhuru kamili, maana ninashugulika na kanuni zako.

46 Nitawatangazia wafalme maagizo yako, wala sitaona haya.

47 Furaha yangu ni kuzitii amri zako, ambazo mimi ninazipenda.

48 Ninaziheshimu na kuzipenda amri zako; nitafikiri juu ya masharti yako.


Kuaminia sheria ya Mungu

49 Ukumbuke ahadi yako kwangu mimi mutumishi wako, ahadi ambayo imenipa matumaini.

50 Hata katika taabu, inanituliza, maana ahadi yako inanipa uzima.

51 Wasiomujali Mungu wananizarau siku zote, lakini mimi sigeuki mbali na sheria yako.

52 Ninapokumbuka maamuzi yako ya tangu zamani, ninafarijika, ee Yawe.

53 Ninashikwa na hasira kali, ninapoona waovu wakivunja sheria yako.

54 Masharti yako yamekuwa wimbo wangu, nikikuwa huku kama mugeni.

55 Usiku ninakukumbuka, ee Yawe, na kushika sheria yako.

56 Hili ni pato langu, kwamba ninashika kanuni zako.


Heshima kwa sheria ya Mungu

57 Wewe, ee Yawe, ndiwe hitaji langu lote; ninaahidi kushika maneno yako.

58 Ninataka kukupendeza kwa moyo wangu wote; unionee huruma kama ulivyoahidi!

59 Nimefikiri juu ya mwenendo wangu, na nimerudi nifuate maagizo yako.

60 Bila kukawia ninafanya haraka kushika amri zako.

61 Waovu wametega mitego waninase, lakini mimi sisahau sheria yako.

62 Usiku kati ninaamuka kwa kukusifu, kwa sababu ya maamuzi yako ya haki.

63 Mimi ni rafiki ya wote wanaokuheshimu, rafiki ya wanaoshika kanuni zako.

64 Dunia imejaa wema wako, ee Yawe, unifundishe masharti yako.


Ukamilifu wa sheria ya Mungu

65 Umenitendea vizuri mimi mutumishi wako, kama ulivyoahidi, ee Yawe.

66 Unipe hekima na ufahamu, maana ninaaminia amri zako.

67 Mbele sijateswa nilikuwa nimepotea, lakini sasa ninashika neno lako.

68 Wewe ni muzuri na unatenda mazuri; unifundishe masharti yako.

69 Wenye kiburi wanasema uongo juu yangu, lakini mimi ninashika kanuni zako kwa moyo wote.

70 Mioyo yao inafungana sana, lakini mimi ninafurahia sheria yako.

71 Nimefaidika kutokana na taabu yangu, maana imeniwezesha kujifunza masharti yako.

72 Sheria uliyoweka ni bora kwangu, kuliko mali zote za dunia.


Ukamilifu wa sheria ya Mungu

73 Kwa mikono yako wewe mwenyewe uliniumba; unijalie akili nijifunze amri zako.

74 Wanaokuheshimu wataniona na kufurahi, maana tumaini langu liko katika neno lako.

75 Ninajua kwamba maamuzi yako ni ya haki, ee Yawe, na kwamba umeniazibu maana wewe ni mwaminifu.

76 Wema wako unifariji, kama ulivyoniahidi mimi mutumishi wako.

77 Unionee rehema nipate kuishi, maana sheria yako ni furaha yangu.

78 Wenye kiburi wafezeheke, maana wananisumbua na maneno ya uongo, lakini mimi nitafikiri juu ya kanuni zako.

79 Wote wanaokuheshimu wakuje kwangu, wapate kujua maagizo yako.

80 Moyo wangu ukuwe mukamilifu juu ya masharti yako, kusudi nisifezeheke.


Kuteswa

81 Ninachoka kwa kukungojea uniokoe; ninatumainia neno lako.

82 Macho yangu yanafifia nikingojea ulichoahidi. Ninauliza: “Utakuja wakati gani kunifariji?”

83 Nimekunjamana kama mufuko wa ngozi katika moshi, hata hivyo sijasahau masharti yako.

84 Mimi mutumishi wako nitavumilia mpaka wakati gani? Utawaazibu wakati gani wale wanaonitesa?

85 Wenye kiburi wamenichimbia mashimo, watu ambao hawafuati sheria yako.

86 Amri zako zote ni za kuaminiwa; watu wananitesa bila haki; unisaidie!

87 Walifikia karibu ya kuniangamiza, lakini mimi sikuvunja kanuni zako.

88 Kwa wema wako, unirudishie uzima, nipate kufuata maagizo uliyotangaza.


Sheria ya Mungu ni ya kutegemewa

89 Neno lako, ee Yawe, linadumu milele; linasimama imara mbinguni.

90 Uaminifu wako unadumu kwa vizazi vyote, umeweka dunia pahali pake, nayo inadumu.

91 Kwa amri yako viumbe vyote viko leo, maana vitu vyote ni chini ya mamlaka yako.

92 Kama sheria yako isingekuwa furaha yangu, ningalikwisha kuangamia kwa taabu zangu.

93 Sitasahau hata kidogo kanuni zako, maana kwa njia yao unanirudishia uzima.

94 Mimi ni wako, uniokoe, maana nimejitoa kushika kanuni zako.

95 Waovu wananivizia wapate kuniua; lakini mimi ninafikiri juu ya maagizo yako.

96 Nimetambua kwamba kila kitu kina mwisho, lakini amri yako haina mupaka.


Kupenda sheria ya Mungu

97 Ninapenda sana sheria yako! Ninafikiri juu yake muchana kutwa!

98 Amri yako iko nami siku zote, inanipa hekima kuliko waadui zangu.

99 Ninaelewa kuliko walimu wangu wote, kwa sababu ninafikiri juu ya maagizo yako.

100 Ninawapita wazee kwa akili yangu, kwa sababu ninashika kanuni zako.

101 Ninajizuiza kufuata njia mbaya, kusudi nipate kushika neno lako.

102 Sikugeuka mbali na maamuzi yako, maana wewe mwenyewe ulinifundisha.

103 Maagizo yako ni matamu sana kwangu; ni matamu kuliko asali!

104 Kwa kanuni zako ninapata hekima, kwa hiyo ninachukia kila mwenendo mubaya.


Sheria ya Mungu ni mwangaza

105 Neno lako ni taa ya kuniongoza, na mwangaza katika njia yangu.

106 Nimeapa na kuhakikisha kiapo changu, kwamba nitashika maamuzi yako ya haki.

107 Ee Yawe, ninateseka sana; unirudishie uzima kama ulivyoahidi.

108 Ee Yawe, upokee maombi yangu ya shukrani, na kunielezea maamuzi yako.

109 Maisha yangu yako katika hatari siku zote, lakini sisahau sheria yako.

110 Waovu wamenitegea mitego, lakini sigeuki mbali na kanuni zako.

111 Maagizo yako ni urizi mukubwa kwangu milele; hayo ni furaha ya moyo wangu.

112 Nimekusudia kwa moyo wote kufuata masharti yako milele.


Usalama katika sheria ya Mungu

113 Ninachukia watu wanafiki, lakini ninapenda sheria yako.

114 Wewe ni ngao yangu, na kimbilio langu; ninaweka tumaini langu katika neno lako.

115 Muondoke kwangu, enyi waovu, kusudi nipate kushika amri za Mungu wangu.

116 Uniimarishe sawa ulivyoahidi, nami nitaishi; usikubali nifezeheke katika tumaini langu.

117 Unishike nipate kuwa salama, nikuwe siku zote musikilivu kwa masharti yako.

118 Unawakataa wote wanaogeuka mbali na masharti yako; mawazo yao maovu ni ya bure.

119 Unaona waovu wote kama vile takataka, kwa hiyo mimi ninapenda maagizo yako.

120 Ninatetemeka kwa kukuogopa wewe; nimejaa hofu kwa sababu ya maamuzi yako.


Utii wa sheria ya Mungu

121 Nimefanya mambo mema na ya haki; usiniache katika makucha ya waadui zangu.

122 Uhakikishe kunisaidia mimi mutumishi wako; usikubali wenye kiburi wanitese.

123 Macho yangu yanafifia nikingojea uniokoe, nikingojea utimize uliyoahidi.

124 Unitendee mimi mutumishi wako kadiri ya wema wako, unifundishe masharti yako.

125 Mimi ni mutumishi wako. Unipe akili nipate kujua maagizo yako.

126 Ee Yawe, sasa ni wakati wa kutenda kitu, kwa maana watu wanavunja sheria yako.

127 Kweli, ninapenda amri zako, kuliko hata zahabu safi kabisa.

128 Kwa hiyo, ninafuata kanuni zako zote; ninachukia kila njia ya upotovu.


Hamu ya kutii sheria za Mungu

129 Maagizo yako ni ya ajabu; kwa hiyo ninayashika kwa moyo wote.

130 Maelezo ya mafundisho yako yanaleta mwangaza; yanawapa akili wajinga.

131 Ninafungua kinywa kwa hamu kubwa, maana ninatamani sana amri zako.

132 Unigeukie na kunionea huruma, kama unavyowatendea wanaokupenda.

133 Uniimarishie hatua zangu kama ulivyoahidi; usikubali mimi nitawaliwe na uovu.

134 Unikomboe kutoka mateso ya wanadamu, kusudi nipate kushika kanuni zako.

135 Uniangazie uso wako kwa wema, unifundishe masharti yako.

136 Macho yangu yanatiririka machozi kama muto, kwa sababu watu hawaishiki sheria yako.


Ukamilifu wa sheria ya Mungu

137 Ee Yawe, wewe ni wa haki; na hukumu zako ni za usawa.

138 Umetoa maagizo yako, kwa haki na uaminifu.

139 Upendo wangu kwako unanifanya niwake hasira, maana waadui zangu hawajali maneno yako.

140 Ahadi yako ni hakika kabisa, nami mutumishi wako ninaipenda.

141 Mimi ni mudogo na ninazarauliwa; hata hivyo sisahau kanuni zako.

142 Haki yako ni haki ya milele; sheria yako ni ya kweli.

143 Taabu na huzuni vimenipata, lakini amri zako ndizo furaha yangu.

144 Maagizo yako ni ya haki siku zote; unijalie akili nipate kuishi.


Kuomba usalama

145 Ninakulilia kwa moyo wangu wote; unijibu, ee Yawe, nifuate masharti yako.

146 Ninakulilia, uniokoe nipate kushika maagizo yako.

147 Ninaamuka mbele ya mapambazuko na kukuomba musaada; ninaweka tumaini langu katika maneno yako.

148 Ninakaa macho wazi usiku kucha, kusudi nifikiri juu ya ahadi zako.

149 Kwa wema wako, ee Yawe, unisikilize; kwa haki yako, unirudishie uzima.

150 Wale wanaonitesa vibaya wanakaribia, hao wako mbali kabisa na sheria yako.

151 Lakini wewe ni karibu nami, ee Yawe, na amri zako zote ni za kuaminiwa.

152 Tangu zamani, nimejifunza maagizo yako ambazo umeziweka hata zidumu milele.


Kuomba musaada

153 Uangalie mateso yangu, uniokoe, kwa maana sikusahau sheria yako.

154 Unitetee na kunikomboa; unirudishie uzima kama ulivyoahidi.

155 Waovu hawataokolewa hata kidogo, maana hawajali juu ya masharti yako.

156 Rehema yako ni kubwa, ee Yawe, unirudishie uzima kama ulivyoahidi.

157 Waadui na watesaji wangu ni wengi, lakini mimi sigeuki mbali na maagizo yako.

158 Ninapowaona waasi hao ninachukizwa sana, kwa sababu hawashiki amri zako.

159 Angalia, ee Mungu, ninavyopenda kanuni zako! Unirudishie uzima kadiri ya wema wako.

160 Kifungo cha neno lako ni ukweli, maamuzi yako yote ya haki yanadumu milele.

161 Wakubwa wananitesa bila sababu, lakini mimi ninaheshimu maneno yako kwa moyo wote.

162 Ninafurahi kwa sababu ya neno lako, kama mutu aliyekuta kitu cha bei kali.

163 Ninachukia kabisa uongo, lakini ninapenda sheria yako.

164 Ninakusifu mara saba kila siku, kwa sababu ya maamuzi yako ya haki.

165 Wanaopenda sheria yako wana amani kubwa; hakuna kinachoweza kuwaangusha.

166 Ee Yawe, ninakungojea uniokoe; mimi ninatimiza amri zako.

167 Ninashika maagizo yako; ninayapenda kwa moyo wote.

168 Ninashika kanuni na maagizo zako; wewe unaona mwenendo wangu wote.


Kuomba musaada

169 Kilio changu kikufikie, ee Yawe! Unijalie akili kama ulivyoahidi.

170 Ombi langu likufikie; uniokoe kama ulivyoahidi.

171 Midomo yangu itatangaza sifa zako, maana unanifundisha masharti yako.

172 Nitaimba juu ya neno lako, maana amri zako zote ni za haki.

173 Ukuwe siku zote tayari kunisaidia, maana nimeamua kufuata kanuni zako.

174 Ninatamani sana uniokoe, ee Yawe; sheria yako ndiyo furaha yangu.

175 Unijalie kuishi nipate kukusifu; na maamuzi yako yanisaidie.

176 Ninatangatanga kama kondoo aliyepotea; ukuje kunitafuta mimi mutumishi wako, maana sikusahau amri zako.

Bible in Swahili Congo © Bible Society of the Democratic Republic of Congo (DRC), 2002.

Bible Society of the Democratic Republic of Congo
Lean sinn:



Sanasan