Zaburi 102 - BIBLIA Maandiko Matakatifu Kwa Watu Wote 2002Maombi katika taabu 1 Maombi ya mutu anayekuwa katika taabu ambaye anamutolea Yawe malalamiko yake. 2 Ee Yawe, usikie maombi yangu, na kilio changu kikufikie. 3 Usijifiche mbali nami wakati wa taabu! Unitegee sikio lako, unijibu upesi wakati ninapokuomba! 4 Siku zangu zinapita kama moshi; mifupa yangu inaungua kama katika furu. 5 Nimepondekana kama majani na kunyauka; sina hata hamu ya chakula. 6 Kutokana na kuugua kwangu, nimebaki mifupa na ngozi. 7 Nimekuwa kama ndege katika jangwa, kama bundi kwenye matongo. 8 Ninalala macho wazi, kama ndege anayekuwa peke yake juu ya paa. 9 Muchana kutwa waadui zangu wananisimanga, wanaonichekelea wanatumia jina langu kwa kulaani. 10 Majivu yamekuwa chakula changu, machozi yanachangana na kinywaji changu, 11 kwa sababu ya kasirani na hasira yako, maana umeniokota na kunitupilia mbali. 12 Maisha yangu ni kama kivuli cha magaribi; ninanyauka kama majani. 13 Lakini wewe, ee Yawe, unatawala milele; jina lako linakumbukwa katika vizazi vyote. 14 Wewe utasimama na kurehemu Sayuni, maana wakati umefika wa kuuhurumia, wakati wake uliopangwa umefika. 15 Watumishi wako wanapenda muji ule, ijapokuwa ni mabomoko sasa; wanauonea huruma, ingawa umeharibika kabisa. 16 Mataifa yataheshimu jina la Yawe; wafalme wote katika dunia wataogopa utukufu wake. 17 Yawe atajenga upya Sayuni, na kuonyesha utukufu wake. 18 Atakubali maombi ya mukosefu; wala hatakataa maombi yao. 19 Andika jambo hili kwa ajili ya vizazi vinavyokuja kusudi watakaozaliwa kisha wamusifu Yawe, 20 kwamba alichungulia chini kutoka katika pahali pake patakatifu. Yawe aliangalia dunia kutoka mbinguni, 21 akasikia malalamiko ya wafungwa, akawaachilia huru waliohukumiwa kuuawa. 22 Watu watatangaza jina la Yawe kule Sayuni; sifa zake zitatangazwa kule Yerusalema, 23 wakati mataifa yatakapokusanyika pamoja na falme zitakapokutana kumwabudu Yawe. 24 Mungu amenipunguzia nguvu ningali kijana; amefupisha maisha yangu. 25 Ee Mungu wangu, usinihamishe sasa wakati ningali bado kijana. Ee Yawe, wewe unadumu milele. 26 Wewe uliumba dunia tokea zamani, mbingu ni kazi ya mikono yako. 27 Vitatoweka na kuchakaa kama nguo, lakini wewe utabaki. Utavibadilisha kama nguo, navyo vitapita. 28 Lakini wewe unabaki sawasawa, na maisha yako hayana mwisho. 29 Watoto wa watumishi wako watakaa salama; wazao wao wataimarishwa mbele yako. |
Bible in Swahili Congo © Bible Society of the Democratic Republic of Congo (DRC), 2002.
Bible Society of the Democratic Republic of Congo