Walawi 9 - BIBLIA Maandiko Matakatifu Kwa Watu Wote 2002Haruni anatoa sadaka 1 Siku ya nane kisha siku saba za kutakaswa, Musa akamwita Haruni na wana wake pamoja na wazee wa Israeli. 2 Musa akamwambia Haruni: Twaa mwana-ngombe dume kwa ajili ya sadaka ya kuondoa zambi na kondoo dume kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa, nyama wote wasikuwe na kilema. Kisha uwatoe sadaka mbele ya Yawe. 3 Uwaambie Waisraeli watwae beberu mumoja kwa ajili ya sadaka ya zambi, na mwana-ngombe mumoja na mwana-kondoo mumoja wote wa umri wa mwaka mumoja na wasiokuwa na kilema kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa, 4 ngombe dume mumoja na kondoo dume mumoja kwa ajili ya sadaka ya amani, wamutolee Yawe sadaka pamoja na sadaka ya unga uliochanganywa na mafuta kwa maana leo Yawe atawatokea. 5 Waisraeli wakaleta vyote hivyo mbele ya hema la mukutano kama vile Musa alivyowaamuru na wote pamoja wakaenda kusimama mbele ya Yawe. 6 Musa akawaambia: Hili ndilo jambo ambalo Yawe aliwaamuru mulifanye kusudi utukufu wake uonekane kwenu. 7 Halafu Musa akamwambia Haruni: Kwenda kwenye mazabahu, utolee pale sadaka yako kwa ajili ya zambi na sadaka ya kuteketezwa na kufanya ibada ya upatanisho kwa ajili yako na kwa ajili ya watu wa Israeli. Kisha tolea pale sadaka za watu na kuwafanyia ibada ya upatanisho kama vile Yawe alivyoamuru. 8 Basi, Haruni akakaribia mazabahu, akachinja yule mwana-ngombe aliyemutoa kuwa sadaka kwa ajili ya zambi yake mwenyewe. 9 Wana wake wakamuletea damu, naye akachovya kidole chake katika damu hiyo na kuipakaa kwenye pembe za mazabahu. Damu iliyobakia akaimwanga kwenye tako la mazabahu. 10 Lakini mafuta na figo akaviteketeza vyote juu ya mazabahu kama vile Yawe alivyomwamuru Musa. 11 Lakini nyama na ngozi akaviteketeza kwa moto inje ya kambi. 12 Kisha Haruni akamuchinja nyama wa sadaka ya kuteketezwa. Wana wake wakamuletea damu, naye akainyunyizia mazabahu pande zote. 13 Kisha wakamuletea sadaka ya kuteketezwa, kipande kimojakimoja, na kichwa, naye akaviteketeza juu ya mazabahu. 14 Akasafisha matumbotumbo na vikanyagio na kuviteketeza pamoja na ile sadaka ya kuteketezwa kwenye mazabahu. 15 Kisha, Haruni akaleta mbele sadaka ya watu. Akatwaa mbuzi wa sadaka ya watu kwa ajili ya zambi, akamuchinja na kumutoa sadaka kwa ajili ya zambi, kama vile alivyofanya kwa yule wa kwanza. 16 Kisha akaleta mbele ile sadaka ya kuteketezwa akatolea sadaka hiyo kulingana na agizo. 17 Kisha akaleta mbele sadaka ya unga akijaza mukono mumoja na kuiteketeza juu ya mazabahu pamoja na sadaka ya kuteketezwa ya kila asubui. 18 Halafu Haruni akamuchinja vilevile ngombe dume na yule kondoo dume wa sadaka za amani kwa ajili ya watu. Wana wake wakamuletea damu ambayo aliinyunyizia mazabahu pande zote. 19 Mafuta ya ngombe dume huyo na kondoo dume, mukia wa kondoo, mafuta yaliyofunika matumbotumbo, figo na sehemu bora ya maini 20 wakayaweka juu ya vilali, naye akaviteketeza kwenye mazabahu. 21 Lakini vile vilali na ule muguu wa nyuma wa kuume, Haruni akafanya navyo kitambulisho cha kumutolea Yawe, kama vile Musa alivyoamuru. 22 Haruni alipomaliza kutolea sadaka zote: sadaka kwa ajili ya zambi, sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani, akawainulia watu mikono, akawabariki, kisha akashuka chini. 23 Halafu Musa na Haruni wakaingia ndani ya hema la mukutano; walipotoka wakawabariki watu, nao utukufu wa Yawe ukaonekana kwa watu wote. 24 Yawe akawasha moto ukaiteketeza sadaka ya kuteketezwa na mafuta yaliyokuwa juu ya mazabahu. Watu wote walipoona huo moto wakapiga vigelegele na kuinama uso mpaka chini. |
Bible in Swahili Congo © Bible Society of the Democratic Republic of Congo (DRC), 2002.
Bible Society of the Democratic Republic of Congo