Nehemia 12 - BIBLIA Maandiko Matakatifu Kwa Watu Wote 2002Majina ya makuhani na Walawi 1-7 Haya ndiyo majina ya makuhani na Walawi waliorudi toka katika uhamisho pamoja na Zerubabeli mwana wa Saltieli, na Kuhani Mukubwa Yesua. Makuhani walikuwa: Seraya, Yeremia, Ezra, Amaria, Maluku, Hatusi, Sekania, Rehumu, Meremoti, Ido, Ginetoni, Abiya, Miyamini, Madia, Bilga, Semaya, Yoyaribu, Yedaya, Salu, Amoki, Hilkia na Yedaya. Hao walikuwa ni wakubwa wa makuhani na wandugu zao wakati wa Yesua. 8 Walawi walikuwa: Yesua, Binui, Kadimieli, Serebia, Yuda na Matania, ambaye alishugulika na usimamizi wa nyimbo za shukrani akishirikiana na ndugu zake. 9 Nao Bakubukia na Uno warafiki zao, walisimama wakielekeana nao katika ibada. Wazao wa Kuhani Mukubwa Yesua 10-11 Yesua alizaa Yoyakimu, Yoyakimu alizaa Eliasibu, Eliasibu alizaa Yoyada, Yoyada alizaa Yonatani, Yonatani alizaa Yadua. Wakubwa wa ukoo za makuhani 12-21 Yoyakimu alipokuwa Kuhani Mukubwa, makuhani hawa walikuwa wakubwa wa ukoo zao: ukoo wa Seraya: Meraya; ukoo wa Yeremia: Hanania; ukoo wa Ezra: Mehulamu; ukoo wa Amaria: Yehohanani; ukoo wa Maluku: Yonatani; ukoo wa Sebania: Yosefu; ukoo wa Harimu: Adina; ukoo wa Meraioti: Helkayi; ukoo wa Ido: Zakaria; ukoo wa Ginetoni: Mesulamu; ukoo wa Abiya: Zikiri; ukoo wa Miniamini: ukoo wa Moadia: Piltai; ukoo wa Bilga: Samua; ukoo wa Semaya: Yehonatani; ukoo wa Yoaribu: Matenayi; ukoo wa Yedaya: Uzi; ukoo wa Salayi: Kalayi; ukoo wa Amoki: Eberi; ukoo wa Hilkia: Hesabia; ukoo wa Yedaya: Netaneli. Jamaa za makuhani na Walawi 22 Wakati wa Eliasibu, Yoyada, Yohanani na Yadua wakubwa wa jamaa za Walawi waliandikwa; vilevile wakati wa utawala wa mufalme Dario wakubwa wa jamaa za makuhani waliandikwa. 23 Wakubwa wa jamaa za ukoo wa Lawi walioandikwa katika kitabu cha Mambo ya Siku mpaka wakati wa Yohanani mujukuu wa Eliasibu. Utaratibu wa kazi katika hekalu 24 Viongozi wa Walawi Hasabia, Serebia, Yesua mwana wa Kadimieli walisimama kuelekeana na wandugu zao walipangwa kwa kuimba nyimbo za kusifu na kushukuru, kufuatana na amri ya mufalme Daudi, mutu wa Mungu. 25 Walinzi wa milango walikuwa: Matania, Bakubukia, Obadia, Mesulamu, Talmoni na Akubu; vilevile hao walikuwa walinzi wa gala. 26 Watu hao waliishi wakati wa Yoyakimu mwana wa Yesua mujukuu wa Yosadaki na vilevile wakati wa Nehemia aliyekuwa liwali wa jimbo; na hata wakati wa Ezra kuhani na mwandishi. Nehemia anazindua ukuta 27 Kisha wakati wa kuzindua ukuta wa Yerusalema Walawi wakatafutwa kila pahali walipokaa kwa kuja Yerusalema kusherehekea kwa furaha pamoja na shukrani na nyimbo, wakitumia matoazi, vinubi na zeze. 28 Wazao wa waimbaji wakakusanyika kutoka vijiji vya Yerusalema na vijiji vya Wanetofati, 29 vilevile kutoka Beti-Gilgali, eneo la Geba na Azimaweti, kwa sababu waimbaji walikuwa wamejijengea vijiji kandokando ya Yerusalema. 30 Makuhani na Walawi wakajitakasa, vilevile wakatakasa watu, milango na ukuta. 31 Nikawakusanya viongozi wote wa Yuda kwenye ukuta na kutenga waimbaji katika makundi mawili makubwa yaliyoimba nyimbo za shukrani wakiwa katika maandamano. Kundi moja lilielekea upande wa kuume wa ukuta mpaka kwenye Mulango wa Takataka. 32 Waimbaji hao walifuatwa na Hosaya akiwa pamoja na nusu ya viongozi wa Yuda. 33 Pamoja naye walikwenda Azaria, Ezra, Mesulamu, 34 Yuda, Benjamina, Semaya na Yeremia. 35 Wazao hawa wa makuhani walikuwa na baragumu: Zakaria, mwana wa Yonatani mujukuu wa Semaya aliyekuwa mwana wa Matania mwana wa Mikaya mwana wa Zakuri mwana wa Asafu. 36 Ndugu zake hawa waliimba kwa ala za muziki za mufalme Daudi, mutu wa Mungu, ni kusema Semaya, Azareli, Milalayi, Gilalayi, Maayi, Netaneli, Yuda na Hanani, wakatanguliwa na Ezra mwandishi. 37 Kwenye Mulango wa Chemichemi walipanda ngazi kuelekea muji wa Daudi, wakapita nyumba ya kifalme ya Daudi, na kuelekea nyuma kwenye ukuta mpaka kwenye Mulango wa Maji, upande wa mashariki wa muji. 38 Kundi lingine lililoimba nyimbo za shukrani lilielekea upande wa kushoto juu ya ukuta. Mimi nikafuatana na kundi hili pamoja na nusu ya watu. Tukapitia kwenye Munara wa Furu mpaka kwenye Ukuta Mupana. 39 Na kutoka pale, tukapitia kwenye Mulango wa Efuraimu, Mulango wa Yesana, Mulango wa Samaki, Munara wa Hananeli, Munara wa Mia moja mpaka kwenye Mulango wa Kondoo. Tulimalizia maandamano yetu kwenye Mulango wa Walinzi. 40 Hivyo, makundi yote mawili yaliyokuwa yanaimba nyimbo za shukrani yakasimama katika nyumba ya Mungu, pamoja nami na nusu ya viongozi; 41 hata na makuhani waliokuwa na baragumu: Eliakimu, Maseya, Miniamini, Mikaya, Eliyoenayi, Zakaria na Hanania. 42 Hao walifuatwa na Maseya, Semaya, Eleazari, Uzi, Yehohanani, Malkiya, Elamu na Ezeri. Waimbaji waliimba wakiongozwa na Yesirahia. 43 Siku hiyo, watu wakatoa sadaka nyingi na kufurahi maana Mungu aliwafanya kuwa na furaha kubwa. Vilevile wanawake na watoto, wote wakafurahi. Vigelegele vya furaha toka katika Yerusalema vikasikilika mbali. Matoleo ya ibada katika hekalu 44 Wakati ule wakachagua watu wa kuchunga vyumba vya gala ambamo matoleo kwa ajili ya hekalu yaliwekwa, malimbuko ya kwanza, zaka na kuyakusanya kutoka katika mashamba ya miji, kwa ajili ya makuhani na Walawi kama ilivyotakiwa na Sheria. Watu wote wakafurahia makuhani na Walawi waliotumika, 45 kwa sababu walifanya ibada ya Mungu wao na ibada ya utakaso, kama vile waimbaji walivyoimba hata walinzi wa milango kulingana na agizo la mufalme Daudi na mwana wake Solomono. 46 Tangu wakati wa mufalme Daudi na Asafu kulikuwa kiongozi wa waimbaji, na kulikuwa nyimbo za sifa na shukrani kwa Mungu. 47 Watu wote wa Israeli, tangu wakati wa Zerubabeli na Nehemia, walitoa matoleo ya kila siku kwa ajili ya waimbaji na walinzi wa milango. Zaidi ya yote, watu wa Israeli wakatoa matoleo kwa ajili ya Walawi, nao Walawi wakatenga sehemu kwa ajili ya wazao wa Haruni. |
Bible in Swahili Congo © Bible Society of the Democratic Republic of Congo (DRC), 2002.
Bible Society of the Democratic Republic of Congo