Matayo 14 - BIBLIA Maandiko Matakatifu Kwa Watu Wote 2002Yesu anawaziwa kuwa Yoane Mubatizaji ( Mk 6.14-29 ; Lk 9.7-9 ) 1 Katika siku zile, Herode, liwali wa jimbo la Galilaya, akasikia habari za Yesu. 2 Halafu akawaambia wasimamizi waliokuwa chini yake: “Mutu huyu ni Yoane Mubatizaji aliyefufuka! Ni kwa sababu hii amepata uwezo wa kufanya miujiza.” 3 Herode alikuwa amemukamata Yoane akamufunga minyororo na kumutia ndani ya kifungo. Herode alifanya vile kwa sababu ya Herodia, muke wa ndugu yake Filipo. 4 Naye Yoane alikuwa amemwambia Herode kwamba hana sheria ya kumwoa yule muke wa ndugu yake. 5 Herode alitaka kumwua Yoane, lakini aliwaogopa watu kwa maana wote walimuhesabia Yoane kuwa nabii. 6 Na ilikuwa kwa sikukuu ya kuzaliwa kwa Herode, binti ya Herodia akacheza mbele ya wote walioalikwa. Binti yule akamupendeza Herode sana 7 hata akamwahidi kwa kiapo kwamba atamupa kitu chochote atakachomwomba. 8 Na kwa ajili ya kusukumwa na mama yake, yule binti akamwambia Herode: “Unipe hapa hapa ndani ya sahani kichwa cha Yoane Mubatizaji!” 9 Mutawala huyu akahuzunika, lakini kwa sababu ya viapo alivyotoa na kwa sababu ya waalikwa, akaamuru binti yule apewe kichwa kile. 10 Basi akaamuru waende kukata kichwa cha Yoane ndani ya kifungo. 11 Halafu wakaleta kile kichwa chake ndani ya sahani na kukitoa kwa yule binti, naye akakipeleka kwa mama yake. 12 Wanafunzi wa Yoane wakakuja kubeba maiti yake na kuizika. Nao wakaenda kumwelezea Yesu habari ile. Yesu anakulisha watu elfu tano ( Mk 6.30-44 ; Lk 9.10-17 ; Yn 6.1-14 ) 13 Yesu aliposikia habari hii, akaondoka pale ndani ya chombo, na kwenda peke yake kwa pahali penye ukiwa. Nayo makundi ya watu waliposikia vile, wakatoka katika miji yao na kumufuata Yesu kwa miguu. 14 Yesu alipotoka ndani ya chombo, akaona kundi kubwa la watu, naye akawasikilia huruma, akawaponyesha wale waliokuwa wagonjwa kati yao. 15 Na ilipokuwa magaribi, wanafunzi wake wakamufikia na kumwambia: “Hapa ni pori na sasa ni magaribi. Uage kundi hili kusudi waende katika vijiji kwa kujinunulia vyakula.” 16 Lakini Yesu akawajibu: “Si lazima waende; ninyi wenyewe muwape chakula.” 17 Lakini wao wakamujibu: “Hapa tuko tu na mikate mitano na samaki mbili.” 18 Yesu akawaambia: “Muvilete hapa.” 19 Kisha kuwaamuru watu waikae juu ya majani, Yesu akatwaa ile mikate mitano na samaki mbili, akainua macho mbinguni, akamushukuru Mungu. Akamega ile mikate, akawapa wanafunzi wake, nao wakaigawanya kwa kundi la watu. 20 Watu wote wakakula na kushiba. Kisha wanafunzi wakaokota vipande vya mikate vilivyobaki, wakajaza vitunga kumi na viwili. 21 Hesabu ya watu waliokula ilikuwa yapata wanaume elfu tano, pasipo kuhesabu wanawake na watoto. Yesu anatembea juu ya maji ( Mk 6.45-52 ; Yn 6.15-21 ) 22 Mara moja kisha mambo hayo, Yesu akawalazimisha wanafunzi wake waingie ndani ya chombo na kumutangulia ngambo ingine ya ziwa. Kwa wakati ule yeye alibaki akiaga lile kundi la watu. 23 Kisha kuagana nao, akapanda kwenye kilima peke yake kwa kuomba. Na giza lilipoingia, alikuwa angali kule peke yake, 24 lakini chombo kilikuwa kimekwisha kufika mbali sana na inchi kavu, kikirushwarushwa na zoruba, kwa maana upepo ulikuwa ukitokea mbele. 25 Ilipokuwa karibu na mapambazuko, Yesu akawafikia wanafunzi wake, akitembea juu ya maji. 26 Nao walipomwona akitembea juu ya maji wakashikwa na hofu, wakisema: “Ni muzimu!” Nao wakaanza kulalamika kwa ajili ya woga. 27 Lakini mara moja Yesu akasema nao, akiwaambia: “Mujipe moyo, ni mimi! Musiogope!” 28 Basi Petro akamwambia: “Bwana, ikiwa kweli ni wewe, utoe amri kusudi nifike pale unapokuwa, nikitembea juu ya maji.” 29 Naye Yesu akamujibu: “Kuja.” Halafu Petro akatoka ndani ya chombo, akaanza kutembea juu ya maji kumufikia Yesu. 30 Lakini alipoona upepo, akaogopa, na kwa vile alivyoanza kuzama ndani ya maji, akalalamika akisema: “Bwana, uniokoe!” 31 Mara moja Yesu akanyoosha mukono, akamushika na kumwambia: “Ee wewe mwenye imani ndogo! Kwa sababu gani uliona shaka?” 32 Nao wote wawili walipopanda ndani ya chombo, upepo ukatulizana. 33 Basi wanafunzi waliokuwa ndani ya chombo wakapiga magoti mbele ya Yesu, wakisema: “Kweli wewe ni Mwana wa Mungu!” Yesu anaponyesha wagonjwa ( Mk 6.53-56 ) 34 Walipokwisha kuvuka ziwa, wakafika pande za Genezareti. 35 Na watu wa kule walipomutambua Yesu, wakatuma habari katika sehemu zile zote. Halafu wakamuletea wagonjwa wote 36 na kumusihi awaruhusu waguse hata upindo wa nguo yake tu. Nao wote waliougusa walipona. |
Bible in Swahili Congo © Bible Society of the Democratic Republic of Congo (DRC), 2002.
Bible Society of the Democratic Republic of Congo