Isaya 15 - BIBLIA Maandiko Matakatifu Kwa Watu Wote 2002Mungu ataiangamiza Moabu 1 Ujumbe wa Mungu juu ya inchi ya Moabu. Muji wa Ari katika inchi ya Moabu umeangamizwa usiku; muji wa Kiri katika inchi ya Moabu umeangamizwa usiku. 2 Watu wa Diboni wamepanda katika hekalu pahali pa juu kwa kuomboleza, watu wa Moabu wanalia kwa ajili ya Nebo na Medeba; vichwa vyote vimenyolewa upaa, ndevu zao zote zimekatwa kabisa. 3 Wanapita katika njia wakivaa magunia. Kwenye paa za nyumba na viwanja vya muji watu wanalia na kukauka kwa machozi. 4 Watu wa Hesiboni na Eleale wanalia, sauti zao zinasikilika mpaka Yasa. Hata waaskari wa Moabu wanalia kwa sauti; mioyo yao inatetemeka. 5 Moyo wangu unaugua kwa ajili ya inchi ya Moabu; wakimbizi wake wanakimbilia Zoari, wanakimbia mpaka Egilati-Selisiya. Wanapanda njia ya kwenda Luhiti wakilia, katika njia kwenda Horonaimu wanatoa kilio cha maangamizi. 6 Kijito cha Nimurimu kimekauka; nyasi zimekauka, majani mabichi yamenyauka, hakuna chochote kinachoota hapo. 7 Wakimbizi wanavuka kijito cha Mierebi; wamebeba mali yao yote waliyopata, na kila kitu walichojiwekea kama akiba. 8 Kilio kimesikilika pote katika inchi ya Moabu, maombolezo yao yamefika Eglaimu, yamefika hata mpaka Beri-Elimu. 9 Maji ya Dimoni yamejaa damu, lakini Mungu ataongeza musiba wa Dimoni. Hao wachache watakaobaki wazima na kukimbia kutoka Moabu, watapelekewa simba wa kuwaua. |
Bible in Swahili Congo © Bible Society of the Democratic Republic of Congo (DRC), 2002.
Bible Society of the Democratic Republic of Congo